Waziri Mkuu awachorea ma-DPP ramani mpya ya vita dhidi ya uhalifu EAC
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza leo Jumatatu, Mei 4, 2026, wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa 11 na Kongamano la Chama cha Waendesha Mashtaka Afrika Mashariki (EAAP), unaofanyika katika Ukumbi wa Blue Sapphire, jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Umoja wa Waendesha Mashtaka katika ukanda wa Afrika Mashariki na nchi jirani unajadili mbinu za kuimarisha matumizi ya teknolojia, kuharakisha upatikanaji wa ushahidi wa kimataifa na kuweka mikakati ya pamoja ya kupambana na uhalifu unaovuka mipaka.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba, ameuhimiza Umoja wa Waendesha Mashtaka wa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki kuimarisha ushirikiano katika kubaini na kufuatilia mitandao ya uhalifu wa kimataifa na kusisitiza matumizi ya teknolojia kama silaha ya kukabiliana na wahalifu.
Akifungua mkutano mkuu wa 11 wa mwaka wa umoja huo ulioanza leo, Jumatatu, Mei 4, 2026, ukishirikisha mataifa 14, Dk Mwigulu amesema tafiti zinaonesha uhalifu mwingi hivi sasa hupangwa kidijitali, kufadhiliwa kwa njia za kielektroniki na kuratibiwa kuvuka mipaka ya nchi, hali inayofanya mapambano dhidi yake kuhitaji mbinu za kisasa zaidi.
Katika mkutano huo wenye kaulimbiu ya ‘matumizi ya teknolojia katika kukabiliana na uhalifu wa wanyamapori na uhalifu wa kimataifa’, wajumbe, pamoja na mambo mengine, wanajadili mbinu za kuimarisha matumizi ya teknolojia, kuharakisha upatikanaji wa ushahidi wa kimataifa na kuweka mikakati ya pamoja ya kupambana na uhalifu unaovuka mipaka.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza leo Jumatatu, Mei 4, 2026, wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa 11 na Kongamano la Chama cha Waendesha Mashtaka Afrika Mashariki (EAAP), unaofanyika katika Ukumbi wa Blue Sapphire, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwenye ufunguzi huo, Waziri Mkuu amesema namna ambavyo uhalifu wa kimataifa hauna mipaka na kubainisha kwamba ni lazima pia juhudi za kupambana nao ziwe za pamoja, hasa katika maeneo ya msaada wa kisheria wa pamoja na urejeshaji wa wahalifu.
Amesema ni vigumu kupambana kwa ufanisi na uhalifu wa kimataifa bila kutumia teknolojia kama nyenzo muhimu katika upelelezi na uendeshaji wa mashtaka.
Akizungumzia uhalifu wa wanyamapori, Dk Mwigulu amesema biashara haramu ya rasilimali hizo ni tishio kubwa kwa uchumi, mazingira na usalama wa mataifa, huku ikichangia kupungua kwa rasilimali za asili sanjari na kuathiri utulivu wa nchi, na kueleza namna unavyohitajika ushirikiano wa karibu kati ya mataifa hayo ili kuudhibiti kwa ufanisi.
“Tanzania imechukua hatua mbalimbali za kisheria ili kukabiliana na changamoto hizo, ikiwemo kufanya mapitio ya sheria za msaada wa kisheria ili kupanua wigo wa ushirikiano na nchi nyingine,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Wajumbe wakiwa katika mkutano mkuu wa 11 wa Umoja wa Waendesha Mashtaka wa Afrika Mashariki na nchi jirani, unaojadili mbinu za kuimarisha matumizi ya teknolojia, kuharakisha upatikanaji wa ushahidi wa kimataifa na kuweka mikakati ya pamoja ya kupambana na uhalifu unaovuka mipaka.
Awali, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wa Tanzania, Sylvester Mwakitalu, amesema kasi ya matumizi ya teknolojia na wahalifu, ikiwemo wizi wa fedha kwa njia za kielektroniki na udukuzi wa mifumo ya benki, ni changamoto kubwa kwa sasa.
Amesema hivi sasa ni ngumu kwa wahalifu kwenda na bunduki benki, bali wanatumia teknolojia kufanya uhalifu.
“Kuna kesi moja ambayo wahalifu walitengeneza mfumo wa kadi za ATM na wakapanga majira ya saa moja pesa zikatolewa katika nchi hizo kwa wakati mmoja. Hivyo, changamoto iliyopo ni namna ya kukabiliana na uhalifu huo,” amesema.
Akizungumzia changamoto ya ucheleweshaji wa kesi, amesema unachangiwa na ukusanyaji wa ushahidi uliopo nje ya nchi.
“Zipo kesi za mazao ya misitu yanayokamatwa hapa, lakini yanaingizwa kutoka Congo. Sasa, ili kuweza kuendesha kesi yako lazima upate ushahidi kutoka Congo na Malawi. Changamoto ni mfumo wa kupata ushahidi huo unachelewesha. Hivyo, mkutano huu unakwenda kujadili namna ya kupata ushahidi kabla ya taarifa rasmi za njia za kidiplomasia kukamilika,” amesema na kufafanua.
“Kwa mujibu wa sheria zetu, mtu anayepokea mabadilishano ya ushahidi hapa nchini ni DPP, lakini kwa nchi nyingine ni Waziri au Mwanasheria Mkuu wa Serikali. DPP A akiwa na uhusiano na DPP mwenzie atamsaidia,” amesema.
Kuhusu matumizi ya teknolojia, amesema kwa Tanzania wanaendelea vizuri, kwani kwa sasa wanasajili mashtaka yao bila kushika karatasi na yanapokelewa kwa njia za kidijitali.
Naye DPP wa Kenya, Renson Ingonga, amesema ni lazima nchi za ukanda wa Afrika ziungane ili kukabiliana na uhalifu ambao mwingi unafanyika kwa njia ya mtandao.
“Utakuta mtu yupo Tanzania anafanya uhalifu Kenya, hivyo Ofisi za Mashtaka katika kila nchi zitumie teknolojia kukabiliana na uhalifu,” amesema.