Waziri Mkuu awaonya waliopewa dhamana ya tehama serikalini

Muktasari:

  • Akizungumza katika uzinduzi wa mifumo ya Tehama serikalini jana jijini hapa, Majaliwa aliwaagiza watendaji, wakuu wa taasisi za umma, wataalamu kusimamia mifumo hiyo vyema ili iweze kutoa tija kwa Watanzania.

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaonya watu waliopewa dhamana ya kusimamia mifumo ya tehama Serikalini kutowakwaza Watanzania kwa kisingizio kuwa mitandao haiko vizuri.

Akizungumza katika uzinduzi wa mifumo ya Tehama serikalini jana jijini hapa, Majaliwa aliwaagiza watendaji, wakuu wa taasisi za umma, wataalamu kusimamia mifumo hiyo vyema ili iweze kutoa tija kwa Watanzania.

“Mifumo hii isitumike kukwamisha watu, shughuli za Serikali…Na kwa sababu ni teknolojia, tusiwakwaze wananchi kwa kuwaambia sijui mtandao umeshuka hapana,” alisema.

Aliwataka wananchi kutumia mifumo hiyo kwa sababu haina urasimu na wala hawatadaiwa rushwa katika utoaji wa huduma.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Ndetiye alisema kwa kushirikiana na wadau wanakamilisha uandaaji wa Mkakati wa Taifa wa Usalama wa Mtandao wa mwaka 2018.

“Pia tupo katika hatua ya kuomba ridhaa ya kutunga sheria ya kulinda taarifa binafsi,” alisema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Gorge Mkuchika aliitaja mifumo ambayo ilizinduliwa jana kuwa ni mfumo wa malipo wa Serikali.

Mifumo mingine ni wa usajili wa vifo na vizazi, taarifa za kitabibu, taarifa za ununuzi, kumbukumbu za kieletroniki, ofisi mtandao, barua pepe Serikalini na vibali vya kusafiria.

Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini, Justina Kagange alisema bado kuna mambo mengi yanahitajika ili Tanzania iingie kikamilifu katika zama za kidigitali na kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na uwezo wa kutumia fursa na huduma ambazo zinaweza kupatikana mtandaoni.

“Kupitia ubia na Serikali ya Tanzania, nina furaha kuwaarifu kwamba mwaka huu tumehitimisha majadiliano ya miradi mitatu mipya itakayogharimu jumla ya Dola za Marekani milioni 955 kwa ajili ya mazingira, maji na umeme,” alisema.

Alisema benki hiyo pia imetenga Dola za Marekani bilioni 1.7 wakati miradi mingine ikitayarishwa ili kuwezesha vipaumbele vya miradi ya maendeleo ambayo Tanzania imejiwekea.