Waziri Mwambe aeleza sababu ya kushuka uchumi
Muktasari:
- Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Geofrey Mwambe amesema lengo la serikali ni kukuza uchumi na kufikia asilimia 8 kutoka 4.6 ya sasa na kwamba lengo la asilimia 8 halikufikiwa kutokana na janga la corona.
Chato. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Geofrey Mwambe amesema lengo la serikali ya Tanzania ni kukuza uchumi na kufikia asilimia 8 kutoka 4.6 ya sasa na kwamba lengo la asilimia 8 halikufikiwa kutokana na janga la corona.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa tamasha la utalii na maonyesho ya biashara Chato leo Agosti 12,2021, Waziri Mwambe amesema mikakati iliyopo sasa na ilikufikia lengo hilo ni lazima kuongeza fursa za ajira, ukuzaji wa biashara.
Kwa mujibu wa Mwambe, mwaka huu 2021, serikali imelenga kukuza uchumi hadi kufikia asilimia 5.5 hadi 6 na kwamba bado mchango wa mapato yatokanayo na sekta ya utalii hayakidhi ikilinganishwa na vivutio vilivyopo nchini.
Amesema licha ya kuwa na hifadhi 22 za taifa, hadi sasa watalii wanaozitembelea ni milioni 1.5 pekee na kuitaka jamii kujenga utamaduni wa kutembelea na kutunza mbuga za wanyama zilizopo kwa maslahi ya sasa na vizazi vijavyo.
Akizungumzia maonyesho hayo, Waziri alisema tatizo kubwa linalowakabili wafanyabiashara hasa wadogo ni kutoungana na kuwa na bidhaa nyingi jambo ambalo linawafanya washindwe kumudu kwenye soko na kufikia malengo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dk Mederd Kalemani amesema wilaya hiyo ina uwekezaji katika sekta ya utalii, uvuvi na kilimo hivyo ni fursa kwa Watanzania kwenda na kuwekeza ili kukuza uchumi.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Chato, Martha Mkupasi, alisema tamasha hilo ambalo limefanyika kwa mara ya kwanza wanatarajia litasaidia kuhamasisha wawekezaji lakini pia wananchi kutumia fursa zilizopo kwenye sekta ya utalii hasa kisiwa cha Rubondo na hifadhi ya Burigi Chato.