Waziri Tax awapa ujumbe wa kujiajiri Wanadiplomasia

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax
Muktasari:
Waziri wa Mambo ya Nje, Uhusiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax amewataka wahitimu wa Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam, kutumia ujuzi vipaji na elimu waliyoipata kuibua fursa za kujiajiri kwa mtu mmoja mmoja au kikundi.
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje, Uhusiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax amewataka wahitimu wa Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam, kutumia ujuzi vipaji na elimu waliyoipata kuibua fursa za kujiajiri kwa mtu mmoja mmoja au kikundi.
Ametolea mfano kwamba wahitimu hao wanaweza kuwa watoa mihadhara kuhusu diplomasia na stadi za kimkakati, kuibua fursa za uwekezaji au kufanya shughuli mbalimbali zinazoendana na taaluma yao.
Dk Tax ametoa wito huo leo Jumamosi Disemba 3, 2022 katika mahafali ya 25 ya Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam, ambapo jumla ya wanafunzi 991 wa ngazi mbalimbali ikiwemo astashahada na hadi shahada walihitimu masomo yao.
Dk Tax ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), amewataka wahitimu hao kujiwekea malengo makubwa yatakayowapa uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa katika maeneo mbalimbali.
"Kuhitimu kwenu leo ni mwanzo wa safari mpya na kunawafungulia milango ya kuajiriwa au kujiajiri, lakini kama mnavyofahamu Serikali haina uwezo wa kuajiri wahitimu wote.
"Kwa kutambua changamoto hii, ndio maana Serikali imeendelea kujenga mazingira ili sekta binafsi ikue na kutoa mchango wa kijamii na kiuchumi katika taifa letu ikiwemo kutoa ajira," amesema Dk Tax.
Dk Tax amesema katika masomo yao wahitimu hao wamejengewa uwezo kuhusu ujasiriamali na uchumi, akisema maarifa hayo ni mtaji kwao utakaowapa mwanga wa kutumia fursa za ndani na nje ya nchi katika kuanzisha shughuli mbalimbali.
"Elimu mlioipata iwe daraja la kuwapatia hamasa ya kuongeza elimu na maarifa zaidi na kuitumia vema ili kuliletea Taifa maendeleo letu na maendeleo yenu, kuhitimu kwenu leo ni mwanzo wa safari mpya bado mna safari ndefu," amesema Dk Tax.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Diplomasi, Balozi Ramadhan Mwinyi amesema chuo hicho ni muhimu katika kujenga na kukuza uhusiano wa kidiplomasia katika mataifa mbalimbali. Hata hivyo,maeneo ya mafunzo kama hayo hayatolewi na chuo hicho bali taasisi nyingi za kitaaluma zinatoa huduma hiyo.
"Hali hii imesababisha kuwepo kwa ushindani naweza kusema usio na tija, ndio maana Serikali imetuelekeza kujikita katika kutekeleza kutoa majukumu ya msingi, maana iwe taasisi ya kitaalamu badala ya kuvutika kibiashara zaidi.
"Jukumu letu sasa ni kujibadilisha kutoka katika taasisi ya kawaida na kuwa taasisi ya kitaaluma na kimkakati, utekelezaji wa suala hili umeshaanza kwa kupitoa upya sera na kanuni zinazotuongoza pamoja kuweka muundo mpya unaokisi malengo tuliopewa," amesema Balozi Mwinyi.
Mmoja wa wahitimu wa chuo hicho, ngazi ya shahada, Cosmas Kimila amesema, " Dk Tax amezungumza vizuri na kutupa moyo na kutusisitiza kuyatumia maarifa na ujuzi tulioupata katila utekelezaji wa majukumu yetu," amesema Kimila.