Waziri Ummy aibana MSD upungufu wa dawa

Muktasari:

  •  Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameihoji Bohari ya Dawa (MSD) sababu ya upungufu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini wakati Januari mpaka Desemba mwaka 2021 Serikali iliipatia taasisi hiyo kiasi cha Sh315 bilioni.


Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameihoji Bohari ya Dawa (MSD) sababu ya upungufu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini wakati Januari mpaka Desemba mwaka 2021 Serikali iliipatia taasisi hiyo kiasi cha Sh315 bilioni.

Amesema kiasi hicho cha fedha kilichowasilishwa hakiendani na huduma ambayo taasisi hiyo imekuwa ikitoa kwa wananchi kwani kumekuwa na malalamiko ya kukosekana kwa dawa zikiwemo ‘antibiotic’, dawa za maji ‘syrup’ na panadol.

Waziri Ummy ameyasema hayo jana Ijumaa Januari 21, 2022 alipofanya ziara ya ukaguzi katika taasisi hiyo iliyoambatana na kikao cha ndani cha menejimenti.

“Wananchi wanalalamika hakuna dawa, tangu Januari mpaka Desemba 2021 Serikali imetoa kiasi cha Sh315 bilioni kwa MSD. Ninapokagua hapa nyaraka naona mahitaji ya zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, mikoa mpaka taifa jumla ya mahitaji ni Sh519 bilioni kwa mwaka lakini ninyi uwezo wenu ni bilioni 160 bado sijaelewa hapa,” amesema Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy ameitaka taasisi hiyo kuhakikisha inatumia makisio yaliyopo kuhifadhi dawa za muda mrefu ili hata itakapotokea dharura nchi inakuwa na dawa za kutosha.

“Malalamiko ya wananchi ni makubwa na nilishasema kitu cha kwanza nitakachoanza nacho ni ubora wa huduma ambao unajumuisha muda wa wagonjwa kukaa hospitali, kupata vipimo vyote na kupata dawa zote anazoandikiwa na daktari ndani ya hospitali,” amesema.

Akijibu hoja hiyo Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Meja Jenerali Gabriel Mhidze ametaja sababu zilizochelewesha dawa kufika nchini na hivyo kuwa na upungufu katika vituo vya afya.

Amesema katika kipindi cha Uviko-19 uzalishaji wa dawa ulipungua duniani na baadhi ya nchi zinazozalisha dawa zilizuia kuuza bidhaa nje ikiwemo mashine za kusaidia kupumua ‘ventilators’.

“Meli zinazosafirisha mizigo pia zilikuwa chache na mchakato ulikuwa mrefu hiyo pia ilisababisha ucheleweshaji wa dawa kufika nchini lakini kwa sasa katika maghala yetu tayari dawa zimeanza kujaa hivyo kwa kipindi kifupi kijacho tatizo hili litatatuliwa,” amesema Dk Mhidze.