Waziri Ummy alia na vijana kutofanya mazoezi
Muktasari:
- Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema, tayari atawasilisha changamoto ya watu wanaofanya mazoezi barabarani kupoteza maisha kwa ajali za bodaboda ili Serikali iangalie namna ya kutengeneza miundombinu rafiki kwa wanaofanya mazoezi barabarani.
Dar es Salaam. Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema watu wanaofanya mazoezi kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza changamoto wanayopitia ni kupoteza maisha wanapofanya mazoezi pembezoni mwa barabara huku akilia na vijana kutopenda mazoezi.
Amesema jambo lisilowezekana mtu kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza akapoteza maisha kwa ajali ya bodaboda hivyo changamoto hiyo ameiwasilisha kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ili barabara zinazojengwa ziwe rafiki kwa kufanya mazoezi na watu kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Takwimu za Taasisi ya Mifupa Muhimbili MOI zinaonyesha kwa mwezi majeruhi 280 wanapokelewa kwa ajali za bodaboda.
Waziri Ummy ameitoa kauli hiyo leo Septemba 29,2023 kwenye maadhimisho ya siku ya moyo duniani yaliyofanyika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete tawi la Dar Group.
"Niwapongeze wazee sasa tumeona mwamko wa watu wazima kufanya mazoezi, kufanya mazoezi sio lazima kukimbia unaweza kutembea, changamoto ipo kwa vijana hawafanyi mazoezi.
Kwenye ufanyaji wa mazoezi changamoto tumeona Watanzania wakipata ajali wanagongwa na bodaboda na tumepeleke kwa Waziri Mkuu kuhakikisha barabara zinazojengwa ni rafiki na watu wanazingatia sheria za usalama barabarani," amesema.
Akizungumzia ongezeko la magonjwa ya moyo nchini, Waziri Ummy amesema shinikizo la juu la damu limekuwa na mchango mkubwa ongezeko la magonjwa ya moyo.
"Mwaka 2017 tulikuwa na wagonjwa milioni 2.5 na mwaka 2022 wakafikia milioni 3.4 wenye matatizo ya moyo, pia shinikizo la damu na kisukari ni magonjwa yanayoongezeka katika kila Watanzania 100 watu 12 wana kisukari na 25 ndio wana shinikizo la damu," amesema.
Vihatarishi vya magonjwa ya moyo ambayo alivitaja Waziri huyo ni matumizi ya sukari kupita kiasi, chumvi pamoja na mafuta.
Pia ametoa ushauri ili kuepukana na matatizo ya moyo amesisitiza watu kufanya mazoezi, kula mboga za majani, kupunguza matumizi makubwa ya chumvi, sukari na mafuta.
Amesema utafiti uliofanyika hivi karibuni unaonyesha, asilimia tatu pekee ya Watanzania ndio wanatumika mbogamboga za majani kwa usahihi akionya kupika mboga mpaka zinaungua ni tatizo linaloikabili jamii.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa JKCI, Dk Angela Mhozya amesema matatizo ya moyo yanaongezeka kwa asilimia 25 kila mwezi kwenye taasisi hiyo.
Amesema katika kila wananchi 25 hadi 30 wanaofika kwenye taasisi hiyo kufanya uchunguzi wa moyo wanabainika kuwa na tatizo hilo.
Naye Rais wa Chama cha Madaktari wa moyo, Dk Robert Mvungi amesema asilimia 13 ya vifo vinavyotokea nchini vinachangia na matatizo ya moyo.
Amesema watu milioni 20 wanapoteza maisha duniani kutokana na matatizo ya moyo.
Maadhimisho ya siku ya moyo mwaka huu yamefanyika yakiwa na kaulimbiu ya Utumie moyo, utambue moyo.