Waziri Ummy ataka NIMR kutafiti tiba asili ya BP

What you need to know:

  • Hatua ya uchunguzi huo imefikiwa na Serikali kutokana na ongezeko la wagonjwa wa Shinikizo la juu la damu nchini.

Dodoma. Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ameiagiza Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kufanya uchunguzi wa dawa za tiba asili na mbadala zinazodaiwa kutibu Shinikizo la juu la damu ili zitumike kudhibiti ugonjwa huo.

Hatua hiyo imefikiwa na Serikali kutokana na ongezeko la wagonjwa wa Shinikizo la juu la damu nchini kutoka wagonjwa 688,901 mwaka 2017 hadi wagonjwa 1,345,847 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 95.4.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 17, 2023 Waziri Ummy amesema uchunguzi huo ukifanyika utawezesha kuiambia jamii ikiwa dawa hizo zinatibu au laa.

“Wataalamu wangu wameniambia pamoja na kuwepo kwa dawa za asili na mbadala lakini hazijathibitishwa, nawataka wataalamu tuzithibitishe kwasababu nimesikia baadhi ya watu zimewasaidia kwahiyo Taasisi ya NIMR itufanyie tafiti.

Hao wanaojitapa dawa hii inatibu Shinikizo la juu la damu tuzifanyie tathmini ya kisayansi ili tuwaambie watanzania kwamba dawa hizi zinatibu au hazitibu”amesema Waziri Ummy.

Aidha Ummy amesema katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kuanzia mwaka 2015 hadi Aprili 2023 kati ya wagonjwa 619,102 waliotibiwa, asilimia 66 ya wagonjwa hao walikuwa na Shinikizo la juu la damu.

Ili kuepuka magonjwa hayo Ummy amesema ni vizuri kupunguza matumizi ya chumvi, sukari, mafuta, kufanya mazoezi, kuepuka matumizi ya tumbaku na vilevi, kuacha tabia bwete na kunywa maji angalau lita 1.5 kwa siku.

Ummy amesema ugonjwa huo ambao tishio hasa kwa watu wenye umri mkubwa, husababisha madhara kama kiharusi, shambulio la moyo, moyo kutanuka, uharibifu wa chujio za figo na kupunguza nguvu za kiume.

Katika upande wa magonjwa yasiyoambukiza Ummy amesema takwimu kutoka Mfumo wa ukusanyaji taarifa za Afya (DHIS2) zinaonesha wagonjwa 2,535,281 walitibiwa magonjwa yasiyoambukiza kwenye vituo vya afya mwaka 2017 na hadi kufikia mwaka 2021 idadi hiyo iliongezeka kufikia wagonjwa 3440,708 sawa na asilimia 9.4.