Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri Ummy: Ugonjwa wa Marburg umedhitiwa, Tanzania ni salama

Dk Mahona Nduru, mmoja wa wataalamu wa afya katika Kituo cha Afya Maruku Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera waliopata maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Marburg baada ya kuhudumia wagonjwa wenye maambukizi akipokea cheti cha uthibitisho wa kupona maradhi hayo kutoka kwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu. Picha na Alodia Dominick

Muktasari:

Virusi vya Marburg, ambavyo kwa asilimia kubwa ni sawa na virusi hatari vya ebola, viligunduliwa kwa mara ya kwanza baada ya watu 31 kuambukizwa na  saba kati yao kufariki mnamo 1967 huko Marburg na Frankfurt Ujerumani na Belgrade huko Serbia.

Bukoba. Serikali ya Tanzania imetangaza kudhibitiwa na kumalizika kwa maambukizi ya ugonjwa wa Marburg ulioukumba Mkoa wa Kagera na kusababisha vifo vya watu sita mwezi Machi, mwaka huu.

Tangazo la kudhibitiwa na kumalizika kwa ugonjwa huo limetolewa mjini Bukoba leo Juni 2, 2023 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuhitimisha kampeni maalum ya kupambana na mlipuko wa ugonjwa wa Marburg mkoani Kagera, Waziri Ummy amesema wataalam wa afya wamejiridhisha kuwa hakuna tena maambukizi wala mgonjwa wa Marburg siyo tu mkoani Kagera, bali pia Tanzania kwa ujumla.

"Ushirikiano wa dhati wa wananchi, Serikali, watumishi wa sekta ya afya na wadau kutoka ndani na nje ya nchi ndio siri ya mafanikio katia maambano dhidi ya mlipuko wa ugonjwa huu….. leo natangaza kuwa ugonjwa huu umeisha. Mkoa wa Kagera na Tanzania ni salama,’’ amesema Waziri Ummy

Hata hivyo, Waziri huyo mwenye dhamana ya afya amesihi Watanzani popote walipo kutobweteka kwa kuendelee kuzingatia maelekezo ya kitaalam ya kujikinga dhidi ya maradhi ya kuambukizi ikiwemo kanuni ya kunawa mikono na kutoa taarifa kwa mamlaka wanapoona dalili za maradhi yasiyoelewa.

Mlipuko wa ugonjwa wa Marburg uliripotiwa kwa mara ya kwanza Machi 19, 2023 katika Kata za Maruku na Kanyangereko Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera baada ya watu kuugua na watu sita kati yao kupoteza maisha.

Kubainika kwa ugonjwa huo kulitokana na uchunguzi wa kitabibu baada ya vifo vya watu hao vilivyotokea Machi 16, 2023; mwanzoni, vifo vya watu hao vilidaiwa kusababishwa na ugonjwa usiojulikana.

Miongoni mwa dalili za ugonjwa huo unaoambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine au kutoka kwa mnyama kwenda kwa binadamu ni pamoja homa, kuumwa kichwa, misuli kuuma, kokohozi, maumivu ya viungo, kuhara na kutapika na kutokwa damu sehemu mbalimbali za mwili.

Kati ya waliopoteza maisha ni mmoja wa watumishi wa sekta ya afya katika Kituo cha Afya Maruku, Amos Kasumuni aliyeambukizwa baada ya kuhudumia wagonjwa

Wengine waliofariki kwa ugonjwa huo ni mtoto mwenye umri wa miezi 18 na watu wengine wanne wa familia moja.

Kutokana na vifo hivyo, Serikali ilichukua hatua kadhaa ikiwemo kutenga eneo maalum la kuwahudumia wagonjwa na wote waliochangamana nao kwa lengo la kuepuka maambukizi zaidi ambapo zaidi ya watu 200 waliwekwa karantini.

Katika hatua nyingine, Serikali imetoa ubani wa Sh5 milioni kwa familia ya mtumishi huyo wa afya aliyefariki akitimiza wajibu na kiapo chake cha kuokoa maisha.

Waziri Ummy ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuiangalia na kuisaidia familia ya mtumishi huyo ikiwemo kusaidia masuala mbalimbali ya kijamii na familia kama ada za watoto wake wanne.

Mmoja wa wafanyakazi wa Kituo cha Afya Maruku, Dk Mahona Nduru ambaye ni miongoni mwa waliougua ugonjwa huo ameishukuru Serikali kwa kuhakikisha watu wote walioambukizwa wanatibiwa na kupona.

Kutokana na Mkoa wa Kagera kupakana na baadhi ya Mataifa yenye magonjwa ya milipuko, Katibu Tawala Mkoa, Toba Nguvila ameiomba Serikali kujenga kituo cha kudhibiti na kuhudumia magonjwa ya milipuko mkoani humo.

Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Tumain Nagu amesema upatikanaji wa haraka wa taarifa za uwepo wa ugonjwa huo ni miongoni mwa siri ya mafanikio katika udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa huo.

‘’Tunawashukuru wadau wetu wa ndani na nchi ya nchi ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), UNICEF, US CDC na Africa CDC kwa ushirikiano uliotuwezesha kuudhibiti ugonjwa huu,’’ amesema Dk Nagu

Historia ya Marburg

Virusi vya Marburg, ambavyo kwa asilimia kubwa ni sawa na virusi hatari vya ebola, viligunduliwa kwa mara ya kwanza baada ya watu 31 kuambukizwa na  saba kati yao kufariki mnamo 1967 huko Marburg na Frankfurt Ujerumani na Belgrade huko Serbia.

Miongoni mwa mataifa ya Afrika ambayo yamewahi kukumbwa na ugonjwa huu ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kenya, Afrika Kusini, Uganda, Zimbabwe na Angola.