Wenyeviti wa vijiji, vitongoji Songwe waonywa kutokuwa chanzo cha migogoro

Muktasari:
- Katibu wa CCM Mkoa, Silvester Mbanga, awahimiza kutumia mafunzo ya sensa kubuni vipaumbele vya maendeleo na kutatua changamoto za wananchi.
Songwe. Viongozi wa vitongoji, vijiji na serikali za mitaa mkoani Songwe waliochaguliwa hivi karibuni wameonywa kutokuwa chanzo cha migogoro kwenye maeneo yao na kwamba watakaobainika wataondolewa.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu, Desemba 23, 2024 na Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe, Silvester Mbanga alipozungumza kwenye mafunzo ya siku moja ya matokeo ya sensa ya watu na makazi yaliyoandaliwa na mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Mbanga amesema migogoro mingi kwenye vijiji na vitongoji husababishwa na viongozi ambao wamekuwa wakitumia madaraka vibaya, tofauti na matakwa ya wananchi waliowachagua.
"Miongoni mwa migogoro ni pamoja na uuzaji holela wa ardhi kwa manufaa yenu, hivyo kama chama hakitawavumilia mkiendekeza vitendo hivyo na mtaondolewa kwenye nafasi hizo mara moja.
"Ninyi viongozi mliochaguliwa acheni kusababisha migogoro ya ndoa kwa kutongoza wake za watu na waume za watu kwa kutumia nafasi zenu, tukikubaini kama chama hatutawaacha salama. Tutawaondoa na kuitisha uchaguzi mdogo," amesisitiza Mbanga.
Amewataka viongozi hao kuzingatia mafunzo waliyoyapata yakawe chachu ya mfano kubuni vipaumbele vya maendeleo yanayohitajika kwa wananchi kulingana na idadi ya wananchi iliyopatikana kipindi cha sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Kwa upande wake, Hasunga amesema mafunzo hayo yamehusisha watu zaidi ya 1,300 wakiwepo wenyeviti wa vitongoji na vijiji yamelenga kuwasaidia kuwajengea uwezo viongozi hao ambao wamekuwa wakilalamikiwa kusababisha migogoro kwenye maeneo yao, ikiwemo ya ardhi.
Hasunga amesema mafunzo hayo yatawasaidia kujua umuhimu wa takwimu ya sensa ya watu na makazi kwa kuibua vipaumbele vya maendeleo sambamba na kupata mafunzo ya kusuluhisha migogoro na kuwa faraja kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe, Radiwelo Mwampashi amewataka viongozi wa vijiji na vitongoji kutumia mafunzo hayo kwenda kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na kutatua changamoto za wananchi.
Mwakilishi wa Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Benedicti Mgambi amesema kwa mujibu wa takwimu ya sensa ya watu na makazi mkoa wa Songwe una wakazi milioni 1.34 huku wilaya ya Mbozi ikiwa na zaidi ya wananchi 500,000 sambamba na mkoa kuwa na asilimia 50.7 ya watoto chini ya miaka 18.
"Tumieni matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa maendeleo ya uchumi kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata, wilaya, mkoa na Taifa, kwani ndio msaada wa kutengeneza mipango ya maendeleo kulingana na idadi ya wananchi kwenye maeneo husika" amesema Mgambi.
Joilasi Kajange, mwenyekiti wa kijiji cha Senjelel Wilaya ya Mbozi amesema mafunzo yatawasaidia kuwaongoza wananchi kwa uadilifu na kuondoa migogoro ya ardhi hususani kwenye kijiji chake.
"Mimi nitatumia mafunzo haya kuondoa migogoro y ardhi kwenye kijiji changu ambacho kwa muda mrefu imekuwa ikisababishwa na viongozi walionitangulia, na pia nitawatumikia wananchi kutatua changamoto zinazowakabili," amesema Kajange.