Wezi waiba nyumbani kwa Mkurugenzi wa Mashtaka

Wezi waiba nyumbani kwa Mkurugenzi wa Mashtaka

Muktasari:

Watu wasiojulikana wamevunja na kuiba vitu mbalimbali nyumbani kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) nchini Kenya, Noordin Haji anayeishi eneo la Riverside, Nairobi.

Nairobi. Watu wasiojulikana wamevunja na kuiba vitu mbalimbali nyumbani kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) nchini Kenya, Noordin Haji anayeishi eneo la Riverside, Nairobi.
Tukio hilo limetokea jana, Alhamisi Agosti 4, 2022 na limezua mijadala mikubwa kwakuwa nyumba hiyo inalindwa na askari polisi.
Licha ya ulinzi wa askari kwenye nyumba hiyo, wezi hao walifanikiwa kuiba kompyuta, viatu na vifaa mbalimbali vya kieletroniki bila polisi waliokuwa wakilinda kujua.
Hata hivyo mtoto wa DDP, ndiye aliyebaini wizi huo baada kutoviona vitu hivyo nyumbani kwao hali iliyomfanya atoe taarifa ya tukio hilo.
Kutokana na tukio hilo, Polisi wameanza uchunguzi huku Waziri wa Mambo ya Ndani, Fred Matiang’i amesema timu maalumu ndiyo imepewa jukumu la kuchunguza.
Ofisi ya DPP kupitia akaunti yake ya mtandao wa twitter imethibitisha kutokea kwa tukio hilo na imewaomba Wakenya wasilichukulie kisiasa kwa kuwa ni la kihalifu.
“DPP angependa kufafanua kuwa kuna tukio la ujambazi kwenye makazi yake na sio ofisini kwake, na uchunguzi unaendelea. DPP haikusanyi au kuhifadhi ushahidi wa aina yoyote. Wananchi na vyombo vya habari wanahimizwa kutoingiza siasa kwenye tukio hili,” ilisema taarifa hiyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Nairobi James Mugera, ametembelea eneo la tukio na kusema bado wanawatafuta wahalifu na watawahoji polisi wote waliokuwa wakilinda nyumbani kwa DPP.