Wezi waiba silaha ofisi za Takukuru

Muktasari:

Watu wasiojulikana wamevunja mlango wa ofisi ya Kamanda wa Takukuru wilayani Handeni na kuiba bastola mbili zilizokuwa na jumla ya risasi 21.


Tanga. Watu wasiojulikana wamevunja mlango wa ofisi ya Kamanda wa Takukuru wilayani Handeni na kuiba bastola mbili zilizokuwa na jumla ya risasi 21.

Habari zilizolifikia Mwananchi jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga, Henry Mwaibambe zinasema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana, baada ya watu hao kutumia funguo bandia kufungua mlango wa mbele wa jengo hilo, kabla ya kuingia ndani na kuvunja mlango na sefu iliyokuwa imehifadhi bastola hizo aina ya Beretta, moja ikiwa na risasi 16 na nyingine tano.

“Wafanyakazi walipofika ofisini, wakakuta mlango uko wazi na ofisini kwa kamanda kumevunjwa, walipoingia ndani wakakuta kasiki (sefu) ya kuhifadhia fedha ikiwa wazi na silaha hizo zimechukuliwa,” kilisema chanzo chetu ambacho hakikutaka kutajwa gazetini.

Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake, Kamanda Mwaibambe alisema tayari ametuma maofisa wake kufuatilia hatua kwa hatua tukio hilo.

“Wameiba bastola mbili zote aina ya Beretta, moja ikiwa na risasi tano na nyingine ikiwa na risasi 16, ndani kulikuwa na silaha nyingine aina ya shotgun, lakini hawakuichukua,” alisema Mwaibambe.

Hata hivyo, alisema tayari wanamshikilia mlinzi wa mgambo aliyekuwa akilinda jengo hilo, ambaye polisi wamegundua hakuwa mwajiriwa wa Takukuru, bali alimshikia mlinzi halisi ambaye yupo likizo.

“Bado timu yangu ipo Handeni ikiongozwa na msaidizi wangu (mkuu wa upelelezi wa mkoa) inafanya uchunguzi wa tukio hili, tutalitolea taarifa rasmi baada ya uchunguzi,” alisema Kamanda huyo.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Takukuru mkoani Tanga, Zainab Bakari alishindwa kukataa wala kukubali kutokea kwa tukio hilo, bali alisema kwa mujibu wa taratibu zao, hapaswi kulizungumzia.

“Kama unavyojua taratibu za vyombo vya usalama, mimi bado sitakiwi kueleza chochote na sina taarifa kamili, nitakapokuwa na taarifa baada ya ziara ya mkuu wa mkoa, basi nitazitoa au zitatolewa na mkurugenzi wetu,” alisema kamanda huyo ambaye alidai yupo kwenye ziara ya mkuu wa mkoa wa Tanga, Omary Mgumba.

Mwananchi lilimtafuta Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru nchini, Salum Hamduni ambaye alisema suala hilo linazungumziwa na polisi kwa sababu “matukio ya uhalifu wa silaha yanaangukia Jeshi la Polisi. Tukio la kihalifu wenye mamlaka ni polisi.”

Alipoulizwa nani wanalinda ofisi za Takukuru, Hamduni alisema, “zinalindwa na walinzi, sasa ni kutoka wapi ni suala la mfumo.”