Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

WHO: Vifo vya ajali barabarani vyapungua duniani, Afrika vyaongezeka

Muktasari:

  • Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema vifo vinavyotokana na ajali za barabarani duniani vimepungua kwa asilimia 21 kati ya mwaka 2011 na 2025 licha ya ongezeko kubwa la magari, lakini Afrika imeenda kinyume na mwelekeo huo kwa kurekodi ongezeko la asilimia 17 ya vifo.

Dar es Salaam. Licha ya ongezeko la zaidi ya magari bilioni moja duniani, vifo vinavyotokana na ajali za barabarani vinatajwa kupungua kwa asilimia 21 kati ya mwaka 2011 na 2025.

Hiyo ni kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) hivi karibuni.

Pamoja na hatua hiyo, nchi za Afrika zinatajwa kushuhudia ongezeko la vifo vinavyotokana na ajali za barabarani kwa asilimia 17.

Takwimu hizo zimetolewa wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio jipya la maendeleo kuhusu usalama barabarani, likilenga kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya kupunguza kwa asilimia 50 vifo na majeraha makubwa yatokanayo na ajali za barabarani ifikapo mwaka 2030, ikilinganishwa na viwango vya mwaka 2021.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema mafanikio yaliyopatikana duniani yanaonesha uwekezaji katika mifumo salama ya usalama barabarani una matokeo chanya.

Amesisitiza vifo vyote vya ajali za barabarani vinaweza kuzuilika na hakuna kifo kinachopaswa kukubalika.

Aidha, amesema azimio jipya linalenga kuhakikisha sera na miundombinu ya usafiri inaweka usalama wa watu mbele badala ya kuzingatia magari pekee.

Kupitia azimio hilo, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimehimizwa kutekeleza mikakati ya kitaifa ya usalama barabarani yenye malengo, muda wa utekelezaji na bajeti maalumu.

Hatua nyingine ni kuanzisha taasisi zinazosimamia usalama barabarani, kuboresha ukusanyaji wa takwimu, kuimarisha sheria na usimamizi wake pamoja na kuhakikisha barabara, magari na miundombinu vinazingatia viwango vya kimataifa vya usalama. serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia, taasisi za elimu na Umoja wa Mataifa pia zimetakiwa kushirikiana katika utekelezaji wa juhudi hizo.

WHO imeeleza ongezeko la watu wanaoishi mijini na matumizi makubwa ya huduma za usafiri kupitia programu za kidijitali yamechangia kuongezeka kwa matumizi ya pikipiki duniani.

Idadi ya pikipiki imeongezeka zaidi ya mara tatu kati ya mwaka 2011 na 2025, huku karibu theluthi moja ya vifo vyote vya ajali za barabarani vikihusisha waendesha pikipiki.

Shirika hilo linasema matumizi ya kofia bora za usalama yanaweza kupunguza hatari ya kufa katika ajali kwa zaidi ya mara sita.

Mkurugenzi wa Idara ya Viashiria vya Afya, Uhamasishaji na Kinga wa WHO, Dk Etienne Krug, amesema zaidi ya nusu ya wanaofariki dunia katika ajali za barabarani si madereva wa magari, bali ni watembea kwa miguu, waendesha baiskeli na waendesha pikipiki.

Amesisitiza sheria madhubuti, utekelezaji wake, miundombinu salama, magari salama pamoja na kudhibiti mwendokasi na uendeshaji chini ya ushawishi wa vilevi vinaweza kuokoa maisha mengi.

Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Usalama Barabarani Tanzania (Tarsi), Malik Barongo, amesema tatizo kubwa Afrika si ukosefu wa sera au miongozo, bali ni utekelezaji wake.

Amesema Umoja wa Mataifa uliweka lengo la kupunguza kwa asilimia 50 vifo na majeruhi wa ajali ifikapo mwaka 2030, lakini baadhi ya nchi za Afrika bado hazijatekeleza kikamilifu nguzo tano za usalama barabarani zinazohusisha usimamizi wa usalama, barabara salama, vyombo vya moto salama, watumiaji salama wa barabara na huduma bora baada ya ajali.

Barongo amesema baadhi ya miradi ya ujenzi wa barabara haizingatii kikamilifu viwango vya usalama, ikiwamo miundombinu kwa watembea kwa miguu na waendesha baiskeli, alama za barabarani na maeneo salama ya kuvukia.

Pia amesisitiza umuhimu wa ukaguzi wa usalama wa barabara katika hatua zote za ujenzi ili kubaini mapungufu yanayoweza kusababisha ajali.

Aidha, amesema huduma za dharura baada ya ajali bado ni changamoto kubwa katika nchi nyingi za Afrika kutokana na kuchelewa kwa uokoaji na usafirishaji wa majeruhi hospitalini.