WHO: Vifo vya Malaria vyapungua

Muktasari:

Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) imeonyesha licha ya athari zinazoendelea za Uviko19, vifo vya wagonjwa wa malaria vimepungua kutoka watu 625,000 mwaka 2020 hadi vifo 619 mwaka 2021, huku Bara la Afrika likiwa na asilimia 95 ya vifo vyote.

Dar es Salaam. Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), imeonyesha kulikuwa na vifo vilivyotokana na ugonjwa wa malaria vinavyokadiriwa kufikia 619,000 duniani kote mwaka 2021 ikilinganishwa na 625,000 mwaka 2020 huku Bara la Afrika likibeba idadi ya asilimia 95 ya vifo vyote.

Takwimu hizo mpya zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) jana Desemba 8, 2022 zinaashiria kuwa nchi zote duniani kwa kiasi kikubwa zilijikita katika huduma za kinga, upimaji na matibabu ya ugonjwa huo.

Mnamo mwaka wa 2019, kabla ya janga hilo kutokea, idadi ya vifo ilisimama kwa 568,000.

Maambukizi ya malaria yaliendelea kuongezeka kati ya mwaka 2020 na 2021, lakini kwa kiwango kidogo ambapo idadi ya wagonjwa wa malaria duniani ilifikia milioni 247 mwaka 2021, ikilinganishwa na milioni 245 mwaka 2020 na milioni 232 mwaka 2019.

"Kufuatia ongezeko kubwa la wanaougua ugonjwa wa malaria na vifo katika mwaka wa kwanza wa janga la Uviko19, nchi zilizoathiriwa na ugonjwa wa malaria ziliongeza juhudi zao na kuweza kupunguza athari mbaya zaidi kwa huduma za malaria,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom na kuongeza;

"Tunakabiliwa na changamoto nyingi, lakini kuna sababu nyingi za matumaini. Kwa kuimarisha mwitikio, kuelewa na kupunguza hatari, kujenga uthabiti na kuharakisha utafiti, kuna kila sababu ya kuwa na ndoto ya mustakabali usio na malaria.”


Ripoti hiyo imetahadharisha kuwa licha ya mafanikio hayo, juhudi zinakabiliwa na changamoto nyingi, haswa katika Kanda ya Afrika, ambayo ilibeba takriban 95 ya idadi ya vifo duniani kwa mwaka 2021.

"Licha ya maendeleo, kanda ya Afrika inaendelea kuathirika zaidi na ugonjwa huu hatari," amesema Dk Matshidiso Moeti ambaye ni Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika.

"Dhana mpya na ufadhili wa kupeleka hizi-zinahitajika kwa haraka ili kutusaidia kuishinda malaria."

Jumla ya ufadhili kwa ajili ya malaria mwaka 2021 ilikuwa dola za Marekani bilioni 3.5, ongezeko kutoka miaka miwili iliyopita lakini chini ya makadirio ya dola za Marekani bilioni 7.3 zinazohitajika duniani kote ili kukabiliana na ugonjwa wa huo.