Wiki ya Abaya, Hina, Kanzu maandalizi ya Eid EL Fitri
Katibu Mkuu wa Bakwata, Alhaj Nuhu Mruma ndiye aliyetoa taarifa hiyo iliyoeleza pia kuwa Swala ya Eid El- Fitri mwaka huu itafanyika kitaifa jijini Dar es Salaam katika Msikiti wa Mfalme Mohamed Vi Bakwata.
Mbali na swala hiyo, Baraza la Eid El- Fitri litafanyika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere kuanzia saa nane mchana, mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Zimesalia siku tatu kabla ya kukamilika kwa mwezi mtukufu na kuifikia siku hiyo ya sikukuu, katika maeneo mbalimbali tayari zimeanza hekaheka za maandalizi ya sikukuu hiyo kubwa kwa Waislamu ambayo huisherehekea baada ya kukamilisha siku 30 za mfungo.
Moja ya maandalizi makubwa na maarufu ambayo hufanywa ni manunuzi ya nguo, viatu ili kuvaa siku hiyo, wapo wanaoandaa kuanzia mavazi ya kwenda kuswalia ibada na kwa mitoko katika sehemu mbalimbali.
Licha ya kuwa wanaume pia husherehekea sikukuu hii, mara nyingi wanawake huhusika zaidi kwenye maandalizi kuanzia namna ya kusherehekea na mwonekano wa wanafamilia.
Hapa ndipo utasikia habari za abaya, baibui na vijora kwa wanawake, kwa upande wa wanaume ni kanzu, vilemba na kofia, maarufu kama barakashia na watoto ni nguo na viatu.
Huko mitaani na mitandaoni habari ya mjini kwa sasa ni abaya, kila mwanamke wa Kiislamu anayekwenda na wakati anataka atupie vazi hilo katika sikukuu ya Eid.
Vazi hili ambalo lina mwonekano kama baibui linapendwa zaidi katika kipindi cha sikukuu kutokana na umaalumu wake ambao kwa kiasi kikubwa husababishwa na gharama.
“Sio lazima uvae halafu ukatembee kama ilivyo kwa watoto, inapendeza siku hiyo mwanamke kuonesha utofauti wako na siku za kawaida. Unaweza ukavaa abaya lako ukiwa unaandaa mahanjumati ya sikukuu, jambo la muhimu hapa ni kupendeza katika vazi hili la stara.
Kama mtu mwezi mzima umejistiri kwa madera, vijora na magauni angalau siku ya Eid uvae nguo ya nzuri ambayo bado itakuacha na stara yako, ndiyo maana kila kona utasikia watu wanataka abaya,” anasema Miriam Mbonde, mfanyabiashara wa nguo za kike.
Ukiachana na mavazi, maandalizi mengine yanayowagusa wanawake wenyewe ni uchoraji wa piko na hina, urembo huu huchukua nafasi kubwa katika 10 la mwisho.
Hilo linathibitishwa na mchora piko, Nusrati Nurdin ambaye anaeleza kuwa kazi hiyo huchangamka kwa kiasi kikubwa katika msimu huu wa sikukuu.
“Hiki ndicho kipindi ambacho wanawake wengi hupaka hina na kuchora piko kama sehemu ya urembo na kuvutia machoni kwa watu. Kwetu sisi ni fursa ya kutengeneza pesa, kwani hadi sasa nina oda ya watu 20.
“Gharama za uchoraji inategemea na ua ambalo mtu anataka kuchora, ila mara nyingi inaanzia Sh5,000 hadi Sh20,000 na wengi hupendelea kuchora mikononi na miguuni,” anasema Nusrati.
Tabia Suleiman anasema sikukuu ya Eid bila kupaka piko bado haiwezi kuwa na maana kwake, hivyo miongoni mwa maandalizi anayoyapa kipaumbele ni urembo huo.
“Hina katika dini ya Kiislamu ni suna na kuchora piko ni pambo la mwanamke, nimeshaweka oda kabisa, ni lazima nichore mikono na miguu, nikishavaa na abaya, hapo sasa ndiyo najiona nimesherehekea sikukuu,” anasema Tabia.
Kwa upande wa wafanyabiashara wa kanzu na vitambaa vya kichwani kwa jinsia ya kiume Sinza, wanaeleza maandalizi ya sikukuu yamepokewa vizuri na baadhi ya maduka kutokana na wateja wengi kutafuta nguo hizo kwa ajili ya kwenda katika swala ya Eid.
“Biashara ya kanzu katika msimu huu imekubali, hata hela naiona, hii ni kutokana na wanaume wengi kununua kanzu na vitambaa vya kichwani kwa ajili ya kwenda kuswalia, inafika wakati unatamani mwaka mzima uwe na mwezi wa Ramadhan,” anasema Khalfan Said.