Wivu wa mapenzi wadaiwa kuchangia kumuua mkewe kwa visu

Muktasari:

  • Inadaiwa ugomvi wa wanandoa hao ulianza baada ya mtuhumiwa kuhisi mkewe anatongozwa na mwanaume ambaye yeye (mtuhumiwa) anamtongoza mkewe.

Mwanza. Mkazi wa Mwamanyili Halmashauri ya Buchosa mkoani Mwanza, Jackson Kalamji (49) anadaiwa kumuua mkewe, Mariam Bulacha (42) kwa kumchoma visu sehemu mbalimbali mwilini, baada ya kumtilia shaka kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbroad Mutafungwa akizungumza na Mwananchi Digital Jumamosi Aprili 13, 2024, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo.

Hata hivyo, akizungumza tena leo Aprili 16, 2024 kuhusiana na tukio hilo baada ya kupigiwa simu, Kamanda Mutafungwa amesema mwili wa marehemu Mariamu bado umehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Sengerema kwa uchunguzi zaidi na baada ya kukamilika utakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko.


Jinsi tukio lilivyotokea.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwamanyili, Dominiko Kashonele akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Aprili 16, 2024 amesema ugomvi wa wenza hao ulianzia kwenye kilabu cha pombe.

Amedai wawili hao kila mmoja alikuwa akimtuhumu mwenzake kuwa na uhusiano wa nje ya ndoa.

“Mke alikuwa anakunywa pombe, na yule bwana naye alikuwa anakunywa…ikasadikika kuwa mtuhumiwa alikuwa anamtongoza mke wa pale walipokuwa wanakunywa pombe…yule naye ikabidi amfuatilie mke wa mtuhumiwa ndipo ugomvi ukaanzia pale. Wakaambiwa na watu wengine waliokuwa eneo hilo waondoke pale waende nyumbani kwao na wakaondoka.

“Walifika nyumbani kwao saa 3 usiku wakaingia ndani ili walale..kumbe huyu mtuhumiwa alikuwa amejipanga amfanyie madhara mkewe kwa kumchoma kisu, alivyomchoma kisu, yeye (Mariam) akatoka ndani akakimbilia kwa majirani kuomba msaada huku akivuja damu, hatua kama 20 kutoka nyumbani kwake akaanguka chini.

“Mtuhumiwa naye alikuwa anamfuata alipomkuta ameanguka akendelea kumchoma kisu maeneo mbalimbali ya mwili wake,”amedai Kashonele.

Akisimulia zaidi mkasa huo, Kashonele amedai wakati tukio hilo linaendelea, hakuna mtu kijijini hapo aliyekuwa na taarifa hadi mtuhumiwa alipoamua kujisalimisha mwenyewe kituo cha polisi cha Kata ya Nyakalilo baada ya kufanya tukio hilo.

Baadaye Polisi walipiga simu Serikali ya kijiji kuwataka waende kuangalia hali ilivyo nyumbani kwa mtuhumiwa.

“Askari ndio wakatupigia simu twende kwenye mji wa mtuhumiwa kuangalia kuna nini, tukaenda, kweli tukamkuta yule mama ameanguka chini anavuja damu, tukaanza kufanya mawasiliano.”


Hata hivyo, amedai kuwa marehemu hakubahatika kuzaa mtoto na mtuhumiwa huyo, licha ya kuwa alikuwa na watoto saba aliozaa na mwanaume mwingine kabla ya kuolewa naye ambao walikuwa wakilelewa nyumbani kwao.

Mkazi wa kijiji hicho, Hadija Masunzi amedai licha ya kuishi kijiji kimoja na Jackson hakuwahi kufikiri anaweza kufanya kitendo hicho kwa jinsi alivyokuwa akiishi.


 Nini kifanyike kukomesha mauaji?

Mwanasaikolojia wa kujitegemea jijini Mwanza, Jacilita Ndaki amesema ili kukomesha mauaji katika jamii ni lazima uwezo wa kujiamini uanze kujengwa kwa mtoto tangu utotoni, ili kuondoa mashaka na kujihami pale linapotokea tatizo.

“Ni lazima tuanzie kwenye mzizi wa awali kuwajengea watoto uwezo wa kujiamini kwa sababu mtu yoyote ambaye hajiamini anajipa mashaka na anajihami na anaweza kufanya mambo yote mabaya… Lakini tuwape elimu ya stadi za maisha na hii si watoto tu maana yake kwa watoto, vijana na watu waziama,”amesema na kuongeza;

“La tatu ni suala la elimu ya mahusiano katika ngazi mbalimbali, mahusiano yapi? Kwa sababu elimu ya mahusiano ni pana, inamfundisha mtu namna ya kutawala hisia, taarifa za kusikia, za kuona lakini pamoja ndani yake watu watajua sasa namna ya kuenenda na mahusiano.

“…jambo lingine watu wafundishwe kuanzia utoto mpaka kukua haki za msingi za binadamu ikiwemo haki ya kuishi kwa sababu huyu anavyoamua kuyatoa maisha yake na mwenzake  manayake aoni yule ana haki ya kuishi na haki ya kuishi inakuwa imekiukwa,” amesema.


Ametoa wito kwa jamii ijenge utamaduni wa kukutana na wataalamu wa saikolojia akidai si lazima wakati wana matatizo tu, bali mtu atenge muda wa kupata elimu na taarifa nini anaweza kufanya ikiwa anakabiliwa na jambo gumu.

Amesema kwa kufanya hivyo inaweza kusaidia kupunguza mauaji kama si kuyamaliza kabisa kwenye jamii.

Naye Askofu wa Kanisa la IEAGT Shinyanga mjini Kambi ya Waebrania, David Mabushi amewashauri wanandoa wanaopitia hali za kutoelewana au hisia za kupeana maumivu ni vizuri watafute msaada mapema akidai migogoro inapopuuzwa au kuachwa kutatuliwa mapema inaleta madhara makubwa ikiwemo vifo.

 “Hatua ya kwanza mnaweza mkashauriwa, lakini kama hamtapata usuluhishi mapema migogoro inaweza ikafika mahali msiwe tena tayari kushauriwa kama msipotoa nafasi hiyo mapema,”amesema na kuongeza;

“Njia zinazoweza kusababisha migogoro hiyo wakati mwingine ni mtu wa tatu anapojitokeza kati ya hao wawili hii inaweza kuwa moja ya sababu ya tatizo kwa hiyo ni lazima tuweke tahadhari kwa kuishi katika ndoa kwa kutoruhusu kuingiliwa na mtu mwingine wa tatu.”

Amesema mauji ya wanandoa mara nyingi yanasababishwa na mazingira ikiwemo wivu na visasi akiwataka kuepuka visasi hasa pale mmoja kwenye ndoa anapokosea ili kuondoa migogoro huku akitaja changamoto ya malezi na imani za ushirikina kuchangia migogoro kwenye ndoa.

“Mauaji mengi yanatokana wakati mwingine na wivu au kisasi..kunapotokea wivu mtu anaamua kulipa kisasi sasa hiyo inachochea badala ya kurekebisa, jambo lingine ni kukosa uelewa kwahiyo wanandoa wengi wanakuwa si waelewa ndio maana hata kunapotokea kutoelewana hawajui wafanye nini ,” amesema askofu huyu.

Amesema ulevi pia unachangia migogoro huku akishauri wanandoa kuachana na mambo ya ulevi aliosema ni chanzo cha migogoro.

“Lakini jambo kubwa ambalo ningelishauri nikushugulika na migogoro mapema, matatizo yanapotutokea tuwaone viongozi wetu wa kiimani kabla moto haujawaka, lakini hata wazazi wanaweza kusaidia,” amesema.