Wivu wa mapenzi wateketeza baba, mama na watoto Mbeya

Muktasari:

Wivu wa kimapenzi umetoa uhai wa wanandoa ambao ni walimu wa Shule ya Msingi Ikuti na watoto wao wawili baada ya kudaiwa kunywa sumu inayotumika kuwekewa katika mimea ya mboga mashambani.

Dar es Salaam. Watu wanne wa familia moja katika kijiji cha Kibumbe, Kata ya Kiwira wilayani Rungwe wamefariki dunia baada ya kudaiwa kunywa sumu inayotumika katika mimea ya mbogamboga shambani kwa kile kilichoelezwa ni wivu wa mapenzi.

Watu hao akiwamo baba, mama ambao ni walimu wa Shule ya Msingi Ikuti na watoto wao wawili walibainika waamefariki baada ya harufu kali kuanza kutoka ndani ya nyumba yao waliyokuwa wakiishi.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Septemba 14, 2022 jijini Mbeya na kaka wa marehemu George Mjaka ambaye amesema familia hiyo ya Adam Mtambo imeteketea wakati matukio ya mauaji ya familia yakiendelea kuongezeka wilayani humo.

Amesema wawili hao walikuwa na ugomvi wa kimapenzi ambapo wote wawili walikuwa walimu wa Shule ya Msingi Ikuti.

“Dada yangu Furtunata mumewe na watoto wao wawili tuliwakuta wamefariki. Tulipoingia tuliona mapanga chini, nyundo na ndani tukaona sumu yaani dawa za kumwagilia mboga na kikombe na kijiko.

"Kabla tulikuja huku tukaona kuna harufu inatoka ndiyo tukavunja mlango baada ya polisi kutupatia ruhusa ya kufanya hivyo,” amesema George.

Naye Mwenyekiti wa kitongoji cha Kibumbe, Ulimboka Mwakyenja amesema mauaji yanayoendelea ya kutisha katika kitongoji hicho Serikali inapaswa kuingilia kati, “Naomba Serikali isiichoke kuendelea kutoa elimu kila mahali ikiwemo kanisani.”

Diwani wa Kiwira, Michael Mwamembe amesema, “Kwa taarifa zilizopo kulikuwa na migogoro ya ndoa ambayo wamesuluhisha kwa muda mrefu, kila siku kuna haja ya Serikali kuliangalia suala hili kwa umakini mkubwa.”

Mkuu wa wilaya ya Rungwe, Dk Vicent Anei ametoa onyo na rai kwa wananchi kutochukua maamuzi hayo yakiwemo mauaji yanayosababishwa na imani za kishirikina.

“Kujitoa uhai ni jambo gumu sana lakini watu wanajitoa uhai na wanaua familia zao pia kwakweli Serikali tutafanya utafiti tuone namna gani tutapambana na janga hili kwa kuwa ni kubwa, changamoto binadamu tunazimaliza lakini si kwa kuamua namna hii, huyu kaua watoto wasio na hatia malaika wa Mungu inaumiza sana.”

Baadhi ya majirani wamesema wanandoa hao walikuwa na migogoro ya muda mrefu kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.