Wizara ya Afya: Bado kuna upungufu wa damu salama

Baadhi ya wananchi wakichangia damu kwenye mkutano wa baraza la mashirika yasiyo ya kiserikali (NACONGO) Jijini Dodoma. Picha na Rachael Chibwete

Muktasari:

  • Serikali imeupongeza Mkoa wa Dodoma kuvuka lengo la kukusanya damu salama kwa kufikisha asilimia 110 huku wakihimiza Mikoa mingine kuweka juhudi na kufikisha asilimia 85 hadi 90.

Dodoma. Wizara ya Afya imesema Tanzania bado inakabiliwa na upungufu wa damu salama, hivyo imezitaka hospitali za mikoa nchini, kuhakikisha zinafikia lengo la ukukusanyaji wa damu hiyo kwa asilimia 85 hadi 90.

Maagizo hayo yametolewa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ziada Selaleo Jumanne Oktoba 3, 2023, jijini Dodoma wakati akizindua zoezi la uchangiaji damu, kwa wajumbe wa baraza la mashirika yasiyo ya kiserikali (Nacongo), ambalo linalokutana kwa siku tatu.

Amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wajawazito, watoto wachanga na watu waliopata ajali, kwani ndiyo makundi makubwa ambayo huwa yanahitaji damu kwa wakati.

Aidha Kaimu Katibu Mkuu huyo ameupongeza Mkoa wa Dodoma kwa kuvuka lengo la kukusanya damu kwa asilimia 110 na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuokoa maisha kwa watu wenye uhitaji wa damu.

"Tunajua kuwa hakuna kiwanda cha kutengeneza damu wala haiuzwi hivyo niwaombe wananchi wajitokeze kwa wingi kuchangia damu ili tuokoe maisha kwa sababu ukichangia chupa moja unaokoa maisha ya watu wawili ya mama na mtoto," amesema Sela.

Amesema bado kuna mikoa ambayo ipo chini kwenye suala zima la uchangiaji damu, na kwamba ukusanyaji wake ni wa asilimia 20, jambo ambalo linaonyesha mikoa hiyo kuwa na uwezo wa kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji wa damu kwa asilimia 20 huku asilimia 80 ikikosa huduma hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Nacongo, Mwantumu Mahiza amesema pamoja na kukutana kwa ajili ya mkutano wa baraza lakini wamejipanga kufanya shughuli zingine za kijamii kama vile kupanda miti, kuchangia damu na kutembelea kituo cha watoto yatima lengo likiwa ni kurudisha fadhila kwa jamii inayowazunguka.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Nelson Bukuru ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kuchangia damu kwenye kituo cha damu salama cha kanda ya kati pamoja na kituo cha afya cha Makole ambapo huduma hiyo ipo kila siku za kazi kwa ajili ya kuokoa maisha