Wizara ya Ardhi yataja chanzo cha migogoro ya ardhi

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2023/24 leo. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetaja mambo matatu kuwa chanzo cha matatizo ya migogoro ya ardhi.

Dodoma. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetaja mambo matatu kuwa chanzo cha matatizo ya migogoro ya ardhi.

Mambo hayo ni watumishi wanaojitolea, ulipaji wa fidia na umilikishaji ardhi kwa watu zaidi ya mmoja ambapo mikoa iliyoathirika zaidi ni Dar es Salaam na Dodoma.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Alhamisi Mei 25, 2023 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti 2023/24.

Waziri amesema matatizo hayo hukolezwa zaidi na watumishi wanaofanya kazi za kujitolea bila kuwa na mishahara lakini maeneo mengine wanakabidhiwa mifumo licha ya kuwa hawana hata mikataba ya utumishi.

Ametolea mfano wa Jiji la Dodoma ambapo hivi karibuni alikwenda kuwatimua watumishi 126 waliokutwa wanafanya kazi bila kuwa hata na mikataba lakini wanaendesha maisha yao vizuri na wanaijua mifumo kama waajiriwa wengine.

“Watumishi wengi wanafanya kazi za kujitolea, hawana mikataba lakini wanaendesha maisha yao vizuri tu, Dodoma peke yake tuliwakuta 126 lakini tulipowahoji ilionekana wapo kwenye mfumo,” amesema Dk Mabula.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Dodoma ilikuwa na migogoro ya ardhi 815 ambayo ilipaswa kupatiwa ufumbuzi lakini hadi sasa 429 ndiyo imeshughulikiwa huku migogoro 386 ikiwa katika hatua za utatuzi.

Katika hatua nyingine waziri amesema kuanzia sasa hakuna ruhusa kwa kampuni au mtu binafsi kuchukua ardhi ya mwanakijiji ikiwa hajajipanga kwenye malipo.

Waziri amesema mtu yeyote anayechukua ardhi ya mwananchi alipe si zaidi ya miezi sita tangu tathimini ilipokubaliwa na ikizidi hapo riba itahusika lakini muda ukienda zaidi inapaswa uthamini ufutwe na uanze upya.