Wizi wa simu na Sh 880,000 vyampeleka jela miaka 30

Wizi wa simu na Sh 880,000 vyampeleka jela miaka 30

Muktasari:

  • Mahakama ya Wilaya ya Temeke leo Jumatano Agosti 4, imemuhukumu mkazi wa Mtongani jijini Dar es Salaam, Joakim Komba maarufu Domo la Mbwa au Pilato (21) kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kuiba kiasi cha Sh880,0000 na simu yenye thamani ya Sh350,000.

Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Temeke leo Jumatano Agosti 4, imemuhukumu mkazi wa Mtongani jijini Dar es Salaam, Joakim Komba maarufu Domo la Mbwa au Pilato (21) kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kuiba kiasi cha Sh880,0000 na simu yenye thamani ya Sh350,000.

Pia mahakama hiyo imeamuru mshtakiwa huyo kuchapwa viboko 10 kabla ya kuanza kutumikia kifungo hicho.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Jimson Mwankenja akisema mahakama hiyo imezingatia adhabu iliyoanishwa katika kifungu cha 227A ya kanuni ya adhabu unyang'anyi wa kutumia silaha haitakiwi kuwa chini ya miaka 30 jela.

Akisoma hukumu hiyo, Mwankenja amesema Julai 21, 2020 maeneo ya Charambe Magengeni mshtakiwa huyo aliiba kiasi cha Sh880,000 na simu aina Sumsung 350,000 jumla Sh211,000 mali ya Juma Swalehe na kabla na wakati alifanya wizi huo alimtishia na kumkata na panga ili apate mali hizo.

Alisema mashahidi watatu wa upande wa mashtaka walitoa ushahidi huku upande wa utetezi mashahidi wanne walitoa ushahidi wao.

Mwankenja amesema kwa ushahidi uliotelewa na Swalehe alidai  Julai 21, 2020 kwamba saa 2 usiku alikuwa kwenye kijiwe cha kahawa akinywa kahawa na rafiki yake alivamiwa na watu wawili mmoja akifahamika kwa jina la Domo la Mbwa au Pilato.

Amesema baada ya kuvamiwa alisikia mshtakiwa huyo akisema ndiye huyu hapa na ndipo alimpiga mapanga na kuchukua simu pamoja na fedha hizo  kisha kuikimbia.

Shahidi huyo alisema aliweza kumtambua kwa kuwa kulikuwa na mwanga wa taa na alikuwa amenyoa  kiduku

Mwankenja amesema baada ya Mahakama hiyo kulidhika na ushahidi wa upande wa mashtaka hivyo imemtia hatiani mshtakiwa huyo.

Amesema mahakama hiyo ilizingatia uzito wa kosa na maslai ya umma,maslai ya mshtakiwa aina ya kosa na uwepo kwa kosa hilo katika wilaya hiyo pamoja na shufaa iliyowasilishwa na Wakili wa serikali ili iwe funzo.

Mwankenja amesema kutokana na kosa hilo mahakama hiyo imempa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela na  kabla ya kuanza kutumikia kifungo hicho mshtakiwa huyo apewe adhabu ya viboko 10.