Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yaliyojiri kesi ya wanafunzi 17 wanaotuhumiwa na HESLB

Wakili wa utetezi Peter Madeleka anayewatatea wanafunzi wanaodaiwa kughushi nyaraka, akiwafafanulia jambo baada ya kesi yao kuahirishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkuu. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya kati ya Juni 2024 hadi Novemba 2025 katika Jiji la Dar es Salaam, ambapo kwa nia ovu na ya kudanganya waliandaa nyaraka za uongo kuonyesha kuwa wazazi wao ni ulemavu kupitia mfumo wa maombi ya mkopo ya elimu ya juu (OLAMS).

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeagiza upande wa Jamhuri kuwapatia nyaraka za maelezo ya mashahidi na vielelezo wanafunzi 17 na mhitimu mmoja wanaodaiwa kughushi na kutoa nyaraka za uongo na kujipatia mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwa njia ya udanganyifu.

Washtakiwa hao kutoka vyuo vikuu hapa nchini, wakikabiliwa na mashtaka 47 yakiwemo ya kughushi nyaraka za mkopo wa HESLB na kujipatia fedha.

Maelekezo hayo yametolewa leo Alhamisi, Julai 9, 2026 na Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya, baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa wameshindwa kuwapatia nyaraka na orodha ya mashahidi na vielelezo washtakiwa hao, kutokana na kukosekana kwa anuani zao.

Washtakiwa katika kesi hiyo jinai namba 13088 ya mwaka 2026 ni wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Frank Kayamba, Eline Urio, Brian Kessy na Loveness  Mrutu;  mwanafunzi wa Chuo cha Biashara (CBE) ni Sophia Macha, Elias Kasiga na Silass Daniel pamoja na Clara Nyarusai, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Pia, mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Eva Namjuzi; mwanafunzi wa Taasisi ya Bahari Dar es Salaam (DMI) Nyasilu Magadula na Badru Lenga; na wanafunzi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), ambao ni Aziza Bashiru, Anitha Godfrey, Cyprian Champunga na Elneth Nyagawa.

Wengine ni mhitimu wa (NIT) Idrisa Omary; mwanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Mohamedi Sefu, na mwanafunzi wa Kairuki University (KU) Michael Shoide.

Hakimu Mbuya amefikia hatua hiyo, baada ya Wakili wa washtakiwa, Peter Madeleka kukataa ombi la Jamhuri la kuahirisha kesi hiyo kwa sababu hawajawapatia nyaraka za maelezo ya mashahidi washtakiwa hao.

Awali, kabla ya kutoa maelekezo hayo wakili wa Serikali, Titus Aron alidai kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa hoja za awali (Ph) lakini kutokana na Jamhuri kutowapatia nyaraka zenye maelezo ya mashahidi na vielelezo, aliomba ahirisho fupi ili waweze kuwapatia nyaraka hiyo.

"Mheshimiwa hakimu, utaratibu tunatakiwa kuwapatia nyaraka hizi siku nne kabla ya kuja kuwasomewa hoja za awali, ili waweze kuzisoma na kuzipitia, hivyo kutokana na sababu hiyo, tunaomba mahakama itupe ahirisho fupi ili tuweze kuwapatia" aliomba Wakili Aron.

Aron baada ya kutoa sababu hiyo, wakili Madeleka alipinga ombi hilo kwa madai kuwa ni ukiukwaji wa haki za watuhumiwa.

"Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 107A, Mahakama hatakiwi kuchelewesha haki ya washtakiwa na wala upande wa Jamhuri hawajaeleza sababu ya wao kushindwa kuwapatia nyaraka hizo," alisema Wakili Madeleka.

Akijibu hoja hiyo, wakili Aron alisema kuwa wameshindwa kuwapatia nyaraka hizo kwa sababu hawakuwa na anuani za washtakiwa hao.

Kutokana na majibu hao, hakimu Mbuya alihoji Jamhuri, kwa kuwa uliza kuwa wamekosaje anuani zao wakati ni wanafunzi na wanasoma katika vyuo vinavyotambuliwa kisheria.

Pia washtakiwa hao walidhaminiwa na kwamba wakihitajika muda wowote wanapatikana, hivyo alisema kama akikufuata kesi hiyo, bado washtakiwa watakamatwa na kufunguliwa kesi hiyo.

"Sababu ya kukosekana kwa anuani za washtakiwa sio sababu ya kuahirisha kesi hii na kama leo nikiamua kutupilia mbali hii kesi kutokana na hoja zenu kutokuwa na mashiko, haitasaidia kwa wanafunzi hawa kwa sababu watakamatwa na hawataachiwa" alisema Hakimu Mbuya na kuongeza

"Natoa agizo kwa upande wa mashtaka, ndani ya siku nne kuanzia kesho, muwe mmewapatia nyaraka zote ili siku ya kuwasomea hoja za awali pasiwe na jambo lolote la kukwamisha," alisema Hakimu Mbuya na kisha kuahirisha kesi hadi Julai 29, 2026.

Katika kesi ya msingi, Inadaiwa kuwa mshtakiwa wa kwanza hadi wa 15 kila mmoja akikabiliwa na mashtaka matatu; mshtakiwa Shoide na Omary wakabiliwa na mashtaka manne, huku Sefu akikabiliwa na mashtaka 16.

Inadaiwa kuwa kati ya Juni 2024 hadi Novemba 2025 washtakiwa wote wakiwa na nia ovu ya kudanganya waliandaa nyaraka za uongo za ulemavu kupitia mfumo wa maombi ya mkopo ya elimu ya juu (OLAMS).

Inadaiwa walifanya hivyo kwa lengo la kuonyesha kuwa wao na wengine wazazi wao wana ulemavu, wakati wakijua si kweli.

Pia ilidaiwa kuwa kati ya tarehe hizo mshitakiwa Kayamba, Sophia , Clara, Eline , Kessy, Loveness, Kasiga, Eva , Silass, Magadula, Lenga, Aziza, Anitha, Champunga, Elneth na Shoide waliwasilisha nyaraka hizo kwa lengo la kuinesha wao na wengine wazazi wao  ni walemavu.

Katika mashitaka ya kujipatia mkopo kwa njia ya udanganyifu, Kayamba anadaiwa kupata mkopo wa Sh5.85milioni kwa kudai kuwa baba yake ana ulemavu, huku Champunga akidaiwa kupata Sh5.89 milioni kwa madai kama hayo.

Mshtakiwa Sophia, Eline , Kessy , Loveness , Eva , Magadula na Lenga wanadaiwa kila mmoja kujipatia Sh2.2 milioni kupitia mikopo hiyo kwa kutumia taarifa za uongo.

Iliendelea kudaiwa kuwa Urio anadaiwa kujipatia Sh2.8 milioni,  Daniel Sh2.217 milioni, Anitha Sh2.195milioni, Elneth, Jonathan, Nyagawa Sh2.15 milioni, Clara Sh1.8 milioni na Aziza Sh1.785 milioni, baada ya kuwasilisha nyaraka hizo za uongo.

Washitakiwa hao wanadaiwa kufanya vitendo hivyo kwa nia ya kudanganya na kujinufaisha kwa kupata mikopo kutoka HESLB.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Juni 12, 2026 na kusomewa mashtaka yao.  Hata hivyo wako nje kwa dhamana.