Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yaliyojiri kortini wanaodaiwa kusafirisha meno ya tembo

Washtakiwa wanaodaiwa kusafiri vipande 19 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh983 milioni, wakiwa chini ya ulinzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi na Mei 2026 katika mikoa ya Mtwara na Dar es Salaam, na walikutwa wakimiliki vipande 19 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh983 milioni.

Dar es Salaam. Mshtakiwa Faki Shaal (54) na wenzake watatu wanaokabiliwa na mashtaka matatu, likiwemo la kumiliki vipande 19 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh983 milioni, wataendelea kusota rumande hadi Julai 10, 2026.

Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa shauri hilo kutokukamilika.

Wakili wa Serikali, Erick Mabagala, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo, Juni 30, 2026, wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Mbali na Shaal, washtakiwa wengine ni Khamis Hassan (40), Kenneth Twelve (54) na Mohamed Suleiman (43).

Wafanyabiashara hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 10770/2026 yenye mashtaka matatu, ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kujihusisha na nyaraka za Serikali na kumiliki meno ya tembo yenye thamani ya Sh983 milioni, mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Mheshimiwa Hakimu, washtakiwa wote wanne wapo mbele ya mahakama yako na kesi hii imeitwa leo kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo upelelezi wake umekamilika, lakini kwa taarifa tulizonazo bado haujakamilika, hivyo tunaiomba mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai Wakili Mabagala mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga.

Upande wa utetezi, ukiongozwa na Faraji Yahaya akishirikiana na Abdurazack Kamwaga na Meshack Dede, ulikubaliana na ombi la Jamhuri la Mahakama kuwapangia tarehe nyingine kwa ajili ya kujua hali ya upelelezi.

Hakimu Ruboroga, baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Julai 10, 2026 kwa kutajwa.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Juni 10, 2026 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kuwa kati ya Machi na Mei 2026, katika mikoa ya Mtwara na Dar es Salaam, kwa makusudi waliongoza genge la uhalifu kwa kukusanya, kumiliki na kupatikana na vipande 19 vya meno ya tembo vyenye thamani ya dola za Marekani 38,000, ambazo ni sawa na Sh983,233,052, mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Shtaka la pili ni kujihusisha na nyaraka za Serikali, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Aprili 30, 2026 na Mei Mosi, 2026 katika Jiji la Dar es Salaam, ambapo walijihusisha na kusafirisha vipande 19 vya meno ya tembo vyenye thamani hiyo bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.

Pia, Mei 11, 2026, eneo la Goba, wanadaiwa kumiliki vipande hivyo bila kuwa na kibali.