Yatimia miaka 12 bila Michael Jackson

Muktasari:

  • Leo Juni 25, 2021 imetimia miaka 12 tangu nguli wa muziki wa Pop duniani Michael Jackson kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 50.

Dar es Salaam. Leo Juni 25, 2021 imetimia miaka 12 tangu nguli wa muziki wa Pop duniani Michael Jackson kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 50.

 Kifo cha Michael kilitangazwa  Juni 25, 2009 huko Los Angeles, California nchini Marekani ambapo inaelezwa alipata mshutuko wa moyo ambao ulikatisha uhai wake.

Inaelezwa kuwa alizidisha kiasi cha dawa aina ya Propofol na Lorazepam katika mwili wake wakati anajiandaa na Tamasha lake 'This Is It' ambalo lilitakiwa lianze kati kati ya mwaka 2009 jijini London, Uingereza.

Michael atakumbukwa kwa kuachia albamu kali kama ‘Thriller’ iliyotoka mwaka 1982 ambayo iliuza nakala zaidi millioni 65 na hadi sasa imebaki kuwa albamu yenye mauzo bora kwa muda wote duniani, huku ikikadiriwa kuwa ameuza nakala za kazi zake zaidi ya milioni 750.

Albamu alizotoa ni kama ‘Got to Be There’ (1971), ‘Ben’ (1972), ‘Music & Me’ (1973), ‘Forever’, ‘Michael’ (1975), ‘Off the Wall’ (1979), ‘Thriller’ (1982), ‘Bad’ (1987), ‘Dangerous’ (1991), ‘HiStory’ ‘Past’, ‘Present and Future’, ‘Book I’ (1995) na ‘Invincible’ (2001).

Hadi anafariki alikuwa ameshinda tuzo nyingi zikiwemo 17 za Grammy, tano za Billboard Music n.k.

Maisha yake binafsi yaligonga vichwa kwenye vyombo vya habari, mwishoni mwa miaka ya 1970 alianza kubadilisha mwonekano wake ambapo alifanikiwa kubadili pua na rangi ya ngozi yake ingawa mwenyewe alidai kubadilika rangi kulisababishwa na ugonjwa.