Yesu amefufuka kwelikweli, Pasaka ni ushindi wetu
Mchungaji Gasper Madumla anapatikana +255 781 001 002
Muktasari:
- Wakristo duniani kote leo wanaadhimisha Sikukuu ya Pasaka ambayo ndiyo msingi wa imani ya Kikristo ambayo mwanadamu aliokolewa kupitia damu ya Yesu Kristo iliyomwagika msalabani.
Wapendwa katika Kristo, Bwana Yesu asifiwe! Ninaitwa Mchungaji Gasper Madumla, leo tunaadhimisha siku ya ushindi Sikukuu ya Pasaka. Hii siyo siku ya kawaida, bali ni siku inayotukumbusha kwamba kaburi halikumuweza Yesu Kristo.
Alikufa, akazikwa, lakini siku ya tatu akafufuka, na sasa yu hai milele. Huu ndiyo msingi wa imani yetu. Kama Yesu asingefufuka, basi imani yetu ingekuwa bure. Lakini ukweli ni kwamba amefufuka na ushindi wake juu ya mauti umetuletea sisi uzima wa milele.
Bwana Yesu alijidhihirisha mara nyingi ili hata wasioamini wapate kuamini. Nami nataka na wewe leo upate picha hii ujue kwamba Yesu alijidhihirisha mara nyingi katika nyakati tofauti tofauti.
Yesu ajidhihirisha kwa Mariamu Magdalene (Marko 16:9-11; Yohana 20:11-18; Luka 8:2)
Baada ya kufufuka, Yesu alimjia Mariamu Magdalene ambaye alikuwa amekombolewa kutoka kwa pepo saba, akimpa heshima ya kuwa wa kwanza kumwona na kumtuma kuwapelekea mitume habari njema za ufufuo.
Kaburi liko wazi (Mathayo 28:1-10; Marko 16:1-8; Luka 24:1-12; Yohana 20:1-9)
Kaburi lililokuwa wazi ni ushahidi mkubwa uliothibitishwa na injili zote nne kwamba Yesu hakubaki maiti bali alifufuka, likiwa ni ujumbe kwa wote wanaomtafuta kwamba hayupo kaburini tena.
3. Yesu ajidhihirisha kwa wanawake wengine (Mathayo 28:9-10)
Yesu alikutana na wanawake walipokuwa wakitoka kaburini, wakamshika na kumsujudia, akionyesha wazi kwamba wao pia walikuwa mashahidi muhimu wa ufufuo wake.
Kwa watu wawili njiani kwenda Emausi (Marko 16:12-13; Luka 24:13-32)
Yesu alijidhihirisha kwa wanafunzi wawili waliokuwa njiani kwenda Emausi lakini hawakumtambua mara moja hadi macho yao yalipofumbuliwa waliposhiriki naye meza.
Yesu ajidhihirisha kwa Petro (Luka 24:34; 1 Wakorintho 15:5)
Baada ya Petro kumkana Yesu, Bwana alimjia binafsi kama ishara ya rehema na urejesho, akionyesha kwamba Mungu hakatishi tamaa wale waliokosea bali huwapa nafasi mpya.
Kwa wanafunzi 11 ghorofani (Marko 16:14;)
Yesu aliwatokea wanafunzi wake waliokuwa na mashaka na mioyo migumu, akimjibu Tomaso aliyekuwa na mashaka kwa kumruhusu kuona ushahidi.
Kwa wanafunzi 10 wakiwa na hofu (Luka 24:36-43; Yohana 20:19-25)
Wanafunzi walipokuwa wamejifungia kwa hofu, Yesu aliingia katikati yao na kuwapa amani, akithibitisha kuwa yeye si roho bali yu hai kweli.
Kwa wanafunzi 7 katika ziwa Galilaya (Yohana 21:1-23)
Yesu alijidhihirisha kwa wanafunzi waliokuwa wamerudi kwenye uvuvi, akiwapa samaki na kuwatia moyo warudi kwenye wito wao.
Kwa wanafunzi 11 mlimani Galilaya (Mathayo 28:16-20; Marko 16:15-18)
Katika mlima wa Galilaya, Yesu aliwapa wanafunzi wake agizo kuu la kuhubiri injili kwa mataifa yote, akiwapa mamlaka na wajibu wa kuendeleza kazi yake.
Yesu ajidhihirisha kwa watu zaidi ya 500 (1 Wakorintho 15:6)
Yesu alionekana na zaidi ya watu mia tano kwa wakati mmoja, jambo linalotoa ushahidi mkubwa na wa wazi kwamba ufufuo wake haukuwa hadithi bali ukweli ulioshuhudiwa na wengi.
Kwa Yakobo na mitume wengine (1 Wakorintho 15:7)
Yesu pia alijidhihirisha kwa Yakobo na mitume wengine, akiwathibitishia utume wao na kuwaimarisha katika imani.
12. Kwa wanafunzi katika mlima wa Mizeituni (Luka 24:44-49; Matendo 1:3-11; Matendo 2:4)
Siku arobaini baada ya kufufuka, Yesu aliwafundisha wanafunzi wake kuhusu ufalme wa Mungu na kuwaahidi Roho Mtakatifu, akiwapa nguvu ya kuanza kazi ya injili.
13. Yesu ajidhihirisha kwa Paulo (Matendo 9:1-9)
Hatimaye Yesu alijidhihirisha kwa Sauli njiani kuelekea Dameski, akimbadilisha kutoka mtesi wa kanisa kuwa mtume mkuu.
Funzo kwa wanadamu juu ya ufufuko wa Yesu Kristo
Ufufuo wa Yesu ni ushindi juu ya dhambi na mauti
Ufufuo wa Yesu Kristo ni uthibitisho kwamba nguvu ya dhambi imevunjwa na mamlaka ya mauti imeangushwa. Kabla ya Kristo kufufuka, dhambi ilikuwa na nguvu ya kumtenga mwanadamu na Mungu, na mauti ilikuwa mwisho wa kila kitu. Lakini Yesu alipofufuka, alibeba ushindi kamili.
Yesu yu hai na anafanya kazi hata leo
Yesu si historia, ni uhalisia wa sasa. Yeye yupo hai, anasikia maombi, anajibu, anaponya, na anaokoa. Watu wengi hufikiri Yesu alikuwepo zamani tu, lakini ukweli ni kwamba anaendelea kujidhihirisha katika maisha ya watu kila siku.
Kila mmoja wetu anaweza kutumiwa na Mungu bila kujali historia yake.
Hii ni faraja kubwa kwetu leo: haijalishi umetoka wapi au umefanya nini, Mungu anaweza kukutumia. Anachotafuta ni moyo ulio tayari, si maisha yaliyo kamili. Ukijitoa kwake, anaweza kufanya mambo makubwa kupitia wewe.
Hatupaswi kuishi kwa hofu, bali kwa imani na ujasiri
Baada ya kufufuka, Yesu aliwakuta wanafunzi wake wakiwa wamejifungia kwa hofu. Lakini aliwaletea amani na ujasiri. Hii ni picha ya maisha ya Mkristo—hatuitwi kuongozwa na hofu, bali na imani. Hofu huleta mashaka na kutuzuia kusonga mbele, lakini imani hutuwezesha kumwamini Mungu hata pale ambapo hatuoni njia.
Tuna wajibu wa kueneza injili kwa wengine
Ufufuo wa Yesu haukuwa kwa ajili yetu tu, bali kwa ulimwengu wote. Ndiyo maana Yesu aliwapa wanafunzi wake agizo la kwenda kuhubiri injili kwa mataifa yote. Hii ni kazi ya kila Mkristo, si wachungaji pekee. Kila mmoja ana nafasi ya kushuhudia kwa maneno na matendo.
Hivyo, Pasaka siyo kumbukumbu tu ya tukio la kale, bali ni ushuhuda hai kwamba Yesu anaishi hata sasa. Anaweza kuingia katika maisha yako, kubadilisha hali yako, na kukupa tumaini jipya. Ubarikiwe na uwe na sikukuu njema. Amina
Ushauri na maombezi wasiliana na Mchungaji Gasper Madumla anapatikana +255 781 001 002