Yowe latetekeza watafiti
Muktasari:
Watafiti hao waliuawa juzi kwa kukatwa katwa mapanga na minde, kisha kuchomwa moto. Gari la Serikali aina ya Toyota Hillux, pia liliteketezwa.
Dodoma/Arusha. Yowe la kuvamiwa na wanyonya damu, lililopigwa na wanawake waliokuwa wakichimba chumvi Kijiji cha Iringa-Mvumi wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma, ndilo lililosababisha kuuawa kwa watafiti wa Chuo cha Utafiti wa Udongo na Maendeleo ya Ardhi cha Selian, mkoani Arusha.
Watafiti hao waliuawa juzi kwa kukatwa katwa mapanga na minde, kisha kuchomwa moto. Gari la Serikali aina ya Toyota Hillux, pia liliteketezwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba, wanawashikilia watu kadhaa akiwamo mwenyekiti wa kijiji. Alisema mwenyekiti wa kitongoji alipigiwa simu na mmoja wa wanawake waliokuwa eneo la tukio kuwa, kuna wanyonya damu wamevamia kijiji.
Mambosasa alisema kwa sababu mwenyekiti huyo alikuwa mbali, alimpigia simu mwenyekiti wa kijiji aende eneo la tukio kujua kilichotokea.