Zaidi ya 4,000 waugua ugonjwa wa macho mekundu Zanzibar

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Hassan Khamis Hafidh akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Januari 30, 2024, Picha na Zuleikha Fatawi

Muktasari:

  • Dalili za ugonjwa huo zinaanza kwa kuvimba mifuniko ya macho, kutokwa machozi, kuwashwa na macho kuwa mekundu

Unguja.  Imeelezwa kuwa, watu 4,579 wanaugua ugonjwa wa macho mekundu (red eye) visiwani Zanzibar.

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Hassan Khamis Hafidh amesema hayo leo Januari 30, 2024 na kuongeza kuwa, wagonjwa hao wameripotiwa katika hospitali na vituo vya afya vya Serikali na binafsi.

Amesema ugonjwa huo husambaa na kusababisha maambukizi ya kirusi kwenye ngozi nyembamba inayozunguka gololi la jicho na kioo cha jicho.


Hafidh amesema dalili za ugonjwa huo zinaanza kwa kuvimba mifuniko ya macho, kutokwa machozi, kuwashwa na macho kuwa mekundu.

"Wataalamu wanasema maradhi hayo hayana tiba maalumu, hivyo wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari," amesema Hafidh.

Amesema kwa kuwa hakuna dawa maalumu ya kutibu maradhi hayo, wananchi wanapaswa kujiwekea tahadhari kujikinga kwa kuosha mikono na uso mara kwa mara.

Pia, amesema dawa za asili zinazotumiwa na baadhi ya wananchi kutibu maradhi hayo sio sahihi badala yake waende katika vituo vya afya ili kupata ushauri wa wataalamu.

Mratibu wa Huduma za Afya Msingi ya Matibabu ya Macho, Rajab Mohammed Hilali ameonya kuwa athari za ugonjwa huo ni kupunguza uoni wa macho, kwa kuwa virusi hivyo vinaathiri milango ya macho.