Fanya haya kuepuka ugonjwa wa macho

Muktasari:

 Baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam yamekumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa macho unaoambukiza

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wameshauri jamii kujenga tabia ya kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka kushikana au kugusa vitu ili kujikinga na ugonjwa wa macho.

Baadhi ya maeneo ya mkoa wa Dar es Salaam yamekumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa macho unaoambukiza.

Mkazi wa Buguruni, Nancy John amesema, “macho yanauma, watu wengi yamevimba wanalalamika kuwashwa, kwetu nyumba nzima macho mekundu.”

Mkazi wa Kinondoni, Hafsa Omary amesema, “ni kama ‘red eyes’ inaambukiza pia, kama kuna mtu yupo ndani anaumwa basi na mwingine ajiandae kupokea kijiti, yanauma jamani.”

Alipoulizwa jana kuhusu mlipuko huo, Kaimu Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Dk Pius Gerald amesema bado hawana taarifa kamili kuhusu chanzo chake na kwamba wanafuatilia.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Januari 13,2024, wataalamu wa afya ya macho wamesema kwa ugonjwa uliopo sasa wamekuwa wakiwashauri wagonjwa kuhakikisha wanaepuka kugusana ili kutousambaza zaidi.

Daktari Bingwa wa Macho kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Anna Sanyiwa amesema mara nyingi magonjwa ya macho ya kuambukiza yamekuwa yakidhibitiwa kwa kuzingatia kanuni za usafi.

“Kunawa mikono na sabuni, magonjwa ya macho hayaambukizi kwa hewa hata mkisogeleana ila unatakiwa kujikinga kwa kunawa mikono mara kwa mara,” amesema Dk Sanyiwa.

Mtaalamu wa afya ya jamii, Dk Paul Masua amesema, “kwa mwenendo huu utakuwa mlipuko wa ugonjwa wa macho ambao bila shaka unasababishwa na virusi ‘Viral Conjunctivitis,’ bahati mbaya kama ni mlipuko wa virusi huwa hakuna dawa.

“Ni kuzingatia usafi, osha macho kwa maji safi, epuka kutumia dawa ya mtu mwingine na mgonjwa anawe mikono yake; pia asiende kazini ili kuepuka kuambukiza wengine, shuka na mito zifuliwe kila asubuhi,” amesema Dk Masue.

Daktari bingwa wa macho Muhimbili-Upanga, Neema Moshi amesema wanashauri zaidi kutogusa macho mara kwa mara na kunawa mikono wakati wote kwa kuwa ugonjwa huo unaambukiza kwa kugusana au kugusa kitu kilichoguswa na mwenye maambukizi.

“Inahusisha kugusana, mtu ana vimelea kwenye mikono halafu anajishika kwenye jicho, akifanya hivyo anapeleka yale maambukizi ambayo ni virusi machoni,” amesema.

Akielezea chanzo chake, Dk Moshi amesema mara nyingi magonjwa ya macho yanaweza kutokea kutokana na virusi na hayo huambukiza, huku akisisitiza kuwa madhara yake ni macho kuuma, kuwasha na kuwa mekundu pekee na mara nyingi hupona yenyewe.

“Chanzo chake huwa mlipuko tu inaweza kuwa ni virusi wamekuwa kipindi hicho hivyo unaposalimiana na mtu kwakushikana ukapata maambukizi, ukishika sehemu ambayo kirusi yupo hivyo muhimu kuepuka kugusa macho,” amesema.

Dk Moshi amesema kwa sasa baadhi ya watu wameugua ugonjwa huo kwa takribani wiki mbili, “kuna mtu wangu wa karibu sana alipata hiyo nikajikinga, sikupata maambukizi jamii inapaswa kufahamu namna ya kujikinga, usiguse meza, vitu, vyuma na hata wale wanaolazimika kushika kwenye daladala hakikisha husugui macho kabla hujanawa mikono yako vizuri.”

Hata hivyo Dk Moshi ameshauri watu kufika katika vituo vya afya kwa ajili ya matibabu pindi wanapobaini kupata maambukizi.

“Mgonjwa asitumie dawa bila ushauri wa daktari, kuna dawa mbaya ambazo zinaweza kusababisha jicho kuharibika au kuharibu mboni ya jicho na zingine zinaingiza ndani zaidi ukikosea ukapewa isiyo sahihi.

“Tunashauri kufuata ushauri wa daktari akuone maana unatakiwa kutumia dawa zenye antibiotiki peke yake na si vinginevyo, kama una uwezo wa kuonwa na daktari wa macho ni vizuri zaidi,” amesema Dk Moshi.