Zaidi ya wakulima 40,000 kunufaika na soko la mhogo

Muktasari:

Bodi ya mazao mchanganyiko Nchini Tanzania (CPB), imeingia makubaliano na kampuni ya nchini China kwa ajili ya kuwauzia mihogo mikavu tani milioni 1.2 , zaidi ya wakulima 40,000 mkoani Mtwara watanufaika na fursa hiyo.

Dodoma. Zaidi ya wakulima 40,000 mkoani Mtwara  watanufaika na kilimo cha mihogo baada Bodi ya Mazao Mchanganyiko (CPB) kuingia makubaliano na Kampuni ya China ya kuiuzia mihogo mikavu.

Akizungumza leo Oktoba 21 2020, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Valerian Mablangeti amesema kila mwezi watakuwa wakipeleka mihogo mikavu tani 100,000.

Amefafanua kuwa tani moja ya mhogo mkavu ni sawa na tani 350000 ya mhogo mbichi.

Amesema tayari usajili wa wakulima hao wataingia katika kilimo cha mkataba na bodi hiyo unaendelea.

Pia, amesema watumishi wa bodi hiyo wanashirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Naliendele kwa kwa ajili ya maandalizi ya mbegu na kutoa utaalam wa kilimo bora.