Zaidi ya watu 3,000 wahitaji ‘dialysis’ kila mwaka

Muktasari:

  • Idadi ya watu wenye matatizo ya figo wanaopata huduma ya usafishaji damu ‘dialysis’ katika vituo vinavyotoa huduma hiyo nchini imeongezeka kutoka 1,017 mwaka 2019 hadi 3,231, Desemba mwaka jana.

Mwanza. Idadi ya watu wenye matatizo ya figo wanaopata huduma ya usafishaji damu ‘dialysis’ katika vituo vinavyotoa huduma hiyo nchini imeongezeka kutoka 1,017 mwaka 2019 hadi 3,231, Desemba mwaka jana.

Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 68.5, huku tafiti zikionyesha wastani wa watu 10 kati ya 100 nchini sawa na asilimia 10 wanaumwa magonjwa ya figo.

Takwimu hizo zimetolewa leo na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Maulid Sulumbu wakati wa kilele cha Siku ya Figo duniani iliyoadhimishwa kitaifa wilayani Musoma Mkoa wa  Mara.

Katika hotuba yake, Ummy amesema wagonjwa 2,585 sawa na asilimia 80 ya wagonjwa wa wote wanaopatiwa huduma ya kusafisha damu nchini, matibabu yao yanagharimiwa na Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF) katika vituo 47 vinavyotoa huduma hiyo jambo linalosababisha mfuko huo kuelemewa.

"Mgonjwa anahitaji kulipia wastani wa Sh1.3 milioni kwa ajili ya vipimo na gharama za kusafisha damu ni kati ya Sh31.2 milioni hadi Sh46.8 milioni kwa mwaka, gharama hizi hazijahusisha gharama za usafiri na gharama nyingine ambazo mgonjwa na wasindikizaji wataingia," amesema.

Amesema kutokana na gharama za matibabu kuwa kubwa wagonjwa wamekuwa wakishindwa kupata huduma kwa wakati hasa kwa wale ambao sio wanachama wa NHIF na kwa wale wanaojitahidi kulipia hujikuta wakiishia kufilisika.

Kufuatia hali hiyo amezindua waraka wa muongozo wa matibabu ya kusafisha damu nchini ili kuongeza tija, kudhibiti na kuepusha usafishaji wa damu unaoweza kuepukika ama kuahirishwa lengo likiwa ni kuboresha matibabu kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo.

"Pia tutahakikisha tunaongeza upande wa vifaa tiba na dawa kwa ajili ya tiba ya ugonjwa wa figo.Niwaombe wananchi tuendelee kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyokuwa ya kuambukizwa kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu ikiwemo suala la lishe, mazoezi na kupunguza matumizi ya pombe," amesema.

Akitoa takwimu za mkoa huo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Kwangwa), Dk Osmund Dyegura amesema wagonjwa 80 wanapatiwa huduma ya kusafisha damu katika hospitali hiyo.

"Hawa wagonjwa wanatakiwa kufika hospitalini mara tatu kwa wiki na kutokana na ongezeko la wagonjwa wa figo tumeanza mikakati kadhaa ili kuhakikisha kasi hii inapungua ikiwemo kuanzisha kliniki za magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza kuanzia ngazi ya vituo vya afya hadi hospitali ya rufaa,” amesema Dk Dyegura.


Hali ilivyo Bugando

Wakati wagonjwa wa figo wakitajwa kuongezeka nchini, wastani wa wagonjwa 6,000 wenye matatizo hayo wanahudumiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kila mwaka sawa na wagonjwa 500 kila mwezi.

Daktari Bingwa Bobezi wa Magonjwa ya Figo Bugando, Dk Said Kanenda alisema miongoni mwao, wagonjwa 61 wanapatiwa huduma ya kusafisha damu kila siku katika hospitali hiyo ili kupunguza kiwango cha sumu mwilini mwao.

Dk Kanenda amesema Bugando inakamilisha maandalizi ya miundombinu ili kuanza upandikizaji wa figo kwa wagonjwa wenye uhitaji ili kuwapunguzia gharama na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kutoka Kanda ya Ziwa kwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma kupatiwa huduma hiyo.

“Kwa mwezi tunapokea wagonjwa wa figo kati 400 hadi 600 wakiwemo wapya na wanaojirudia. Tuko kwenye maandalizi tunataka tuanze upandikizaji wa figo hii ni kutokana na dhamira ya Serikali ya kusogeza huduma kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa na tayari maandalizi yamefikia asilimia 90.

“Wakati wowote mambo yakikamilika tukishirikiana na wenzetu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, tayari rasilimali watu tunayo na wengine wako kwenye mafunzo ndani na nje ya nchi. Pia hospitali ya Benjamin Mkapa tumekuwa tukishirikiana nao kufanya huduma za upandikizaji huo,” amesema Dk Kanenda.

Alitaja baadhi ya visababishi vya magonjwa hayo kuwa ni matumizi mbogamboga zenye dawa za viuatilifu, matumizi holela ya dawa tiba, pombe, sigara huku akidokeza kuwa kuna ongezeko la wanawake wanaougua matatizo ya figo wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.

Muuguzi bingwa wa magonjwa ya figo Bugando, Frank Rwihula amesema ili mgonjwa anayesumbuliwa na tatizo la figo katika hatua kuanzia ya tatu hadi tano, apate nafuu anahitajika kusafisha damu angalau mara tatu kwa wiki jambo ambalo amesema linagharimu kiasi kikubwa cha fedha.

Rwihula amewataka wananchi kujiunga NHIF kabla ya kuugua ili kupata unafuu pindi wanapougua magonjwa mbalimbali yakiwemo ya figo ambayo matibabu yake ni gharama kubwa.


Wagonjwa wanena

Mkazi wa Shibula, James Kabadi ambaye anafanyiwa ‘dialysis’ katika hospitali hiyo ameeleza kuridhishwa na huduma inayotolewa hospitalini hapo huku akiiomba Serikali kusisitiza jamii kujiunga NHIF kwa kile alichodai ni ngumu kwa mtu asiye na bima hiyo kumudu gharama za matibabu hayo.

“Gharama ya kusafisha damu kwa awamu moja ni zaidi ya Sh300,000 na mgonjwa ili awe sawa mwilini anatakiwa asafishwe angalau mara tatu kila wiki. Ninamudu kufanya hivi kwa sababu nina bima. Hata wakati hospitali za binafsi wamesitisha kupokea bima tulishtuka sana kwa sababu tulihofia kuwepo msongamano hapa Bugando,” amesema Kabadi.

Mgonjwa mwingine, Raphael Otieno (82) amesema baada ya kubainika kuugua figo miaka miwili iliyopita,  alianza kukata tamaa ya kuishi akiamini hatopona hadi pale alipoanza matibabu ya kusafisha damu na kuanza kuona afya yake ikiimarika.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuboresha miundombinu ya utoaji wa huduma ya afya hasa huduma za kibingwa. Awali tulikuwa tunasafiri kwenda Muhimbili lakini sasa hivi wakazi wa Kanda ya Ziwa tunahudumiwa hapa Bugando tu,” amesema Otieno.