Prime
Pombe, 'energy drink' zinavyomaliza vijana

Pombe kali nayo...
Akielezea athari za pombe kwenye figo, Dk Gyunda anasema pombe kali husababisha moyo kwenda mbio na hivyo kuzalisha shinikizo la juu la damu na vyote ni hatari na huleta athari kwenye figo.
“Pombe kali husababisha mwili kupoteza maji mengi, shinikizo la juu la damu linaleta kisukari na matatizo ya ini na figo huchuja sumu nyingi bila kupumzika.
“Ukinywa kinywaji kikali ni kama umekunywa sumu. Inapopita kwa wingi, inasababisha madhara, vishipa vya damu ndani ya figo vinakwanguliwa na vinywaji vikali vinavyonywewa mara kwa mara kwa muda mrefu,” alisema.
Changamoto hii inabainishwa kipindi ambacho nchi ina vituo vya afya 59 pekee vinavyotoa huduma za usaidizi wa kuchuja damu, vikiwemo 29 vya umma na 30 binafsi, kwa takwimu za Januari 2024 mwaka huu.
Gharama changamoto
Wakati tatizo hilo likiongezeka, Serikali hutumia kati ya Sh88.1 bilioni mpaka Sh110.2 bilioni kila mwaka kwa wagonjwa wasio na uwezo, wanaopata tiba ya kuchuja damu kwa utaratibu wa misamaha.
Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kati ya asilimia 30 mpaka 40 ya wanaolipia huduma ya kusafisha damu ,wapo kwenye misamaha ya kiwango tofauti, kuanzia wanaolipia Sh20,000 mpaka Sh100,000 kwa mzunguko mmoja, huku asilimia 10 kati yao hawalipi chochote.
Kwa wastani mgonjwa hulipia Sh1,320,000 kwa ajili ya vipimo kwa mwaka na gharama za huduma ya kusafisha damu ya wastani kati ya Sh31,200,000 hadi 46,800,000 kwa mwaka, bila kuhusisha usafiri na gharama nyingine.
Takwimu hizo zinaonyesha kifurushi kimoja cha vifaa vinavyotumika kwa wagonjwa kinagharimu kati ya Sh180,000 hadi Sh184,320, gharama hizo hazijumuishi nyingine za uendeshaji kama umeme, maji, sterilizers, mashine za kufulia na nyinginezo.
Hadi kufikia Machi 2023, Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) ilikuwa imekamilisha ununuzi wa mashine za dialysis 140 na tayari zimesambazwa kwenye vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya nchini.
Gharama za mashine moja ya dialysis ni kati ya Sh20.8 milioni mpaka Sh28.9 milioni na zinaponunuliwa huambatana na mfumo wa mashine unaofungwa pembeni kwa ajili ya kusaidia kuchuja maji, zinazouzwa kwa Sh39.3 milioni kwa kila moja.
Hadi Januari 2024 takwimu zinaonyesha jumla ya wagonjwa 3,500 wanapata huduma ya dialysis ikilinganisha na wagonjwa 1,017 ambao walikuwa kwenye huduma hiyo Agosti 2019, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 70 ndani ya miaka mitano.
Taarifa za Juni, 2023 zinaonyesha jumla ya wagonjwa 113 wamepandikizwa figo, 78 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na 35 katika Hospitali ya Benjamini Mkapa.
Utafiti uliofanyika Kisarawe mwaka 2018 ulionyesha kati ya watu 100, watu 12 wana shida ya figo katika hatua tofauti tofauti.
Energy drink, pombe kali
Si katika figo tu, vinywaji hivyo vimetajwa mara kwa mara kuwa madhara mwilini, lakini vimebaki kuwa pendwa na jamii, hasa vijana, japo vinatajwa kuwa na madhara ya moyo.
Wakizungumza na Jarida hili kwa nyakati tofauti, wataalamu wameonya kuhusu vinywaji hivi wakisema energy drinks zinaweza kuleta madhara ya mishipa ya moyo kuziba ghafla na hata vifo vya ghafla.
Kutokana na hilo, inashauriwa mtu asizidishe kikopo (chupa) kimoja (mililita 250) cha kinywaji hicho kwa saa 24, huku wakisisitiza itapendeza zaidi mtu asipokunywa kabisa kwa kuwa matokeo hasi yake hayatabiriki.
Baadhi ya vinywaji hivyo ambavyo ndani yake kuna maji, sukari, ladha, caffein, mitishamba, tauline (amino acid), protini, vitamini, madini na virutubisho, utafiti wa kisayansi uliofanywa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ulivihusisha na matatizo ya moyo na mishipa kuziba ghafla.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo JKCI, Pedro Palangyo aliwahi kunukuliwa na gazeti hili akisema matumizi ya vinywaji hivyo yamekuwa makubwa katika jamii na kuwa vijana wengi hawatumii kwa sababu ya kujipa nguvu, bali kwa kupenda ladha yake.
Alisema takwimu za hivi karibuni za taasisi hiyo zinaonyesha wanapata wagonjwa wengi wa mishipa kuziba kwa watu wenye umri mdogo, ambao katika hali ya kawaida ya ugonjwa huo, umri mdogo ni mtu yeyote chini ya miaka 45.
Wakati pombe zikitajwa kuchangia tatizo hilo, pombe zisizo na ubora ambazo zimekuwa zikiuzwa kwa bei rahisi zinaelezwa kuwa hatari kwa watumiaji.
Akizungumzia kuhusu pombe kali feki Mkurugenzi wa Kudhibiti Bidhaa Bandia kutoka Tume ya Ushindani FCC, Hadija Ngasongwa anasema ukamataji wa pombe hizo umekuwa mgumu kwani unategemea wamiliki halali kutoa taarifa za bidhaa feki.
“Ni ngumu kukamata kwa sababu hizo biashara zinafanyika kwa siri ila pale tunapopata taarifa, ndio tunafanya ufuatiliaji, mfano mwaka jana tulipata taarifa kutoka kwa wamiliki wa Konyagi, tukafuatiliaji na kukamata vinywaji hivyo feki huko Simiyu,” anasema Hadija.
Anasema kesi hiyo iliyofunguliwa mwaka jana, inaendelea mahakamani na kwamba udhibiti wa bidhaa bandia utafanikiwa kupitia ushirikiano baina ya wazalishaji wa pombe zenye viwango, jamii na FCC.
“Hapa lazima tutumie ule mfumo wa utatu ambao ni mmiliki, mlaji na Serikali, tukishiriana kwa pamoja tutaweza kutokomeza bidhaa feki,” anasema Hadija.
Mmiliki wa moja duka la vinywaji jijini Dar es Salaam, Hana Alfred anasema amezoea kununua pombe kali kwenye maduka ya jumla na ndizo anavyokwenda kuziuza kulingana na bei aliyonunulia.
“Nauza kulingana na nilivyonunua, nikinunua Konyagi Sh8,000 nitauza Sh10,000 au zaidi ya hapo.
Lakini kwa sasa pombe feki zipo, binafsi nazijua feki gharama ni ndogo na kwa sasa ni nyingi, hawa watu wanaharibu soko,” anasema Hana.
Mhudumu mmoja wa baa maarufu Tabata anasema, “niliwahi kufanya kazi Manzese huko pombe kali feki zilikuwa nyingi na bei rahisi. Lakini huwezi amini nimekuja Tabata huku nako zinapenya.”
Mambo ya kuepuka
Figo ni kiungo chenye kazi ya kuchuja takamwili na kuzitoa nje kwa njia ya mkojo na kupunguza kiasi cha maji kilichozidi mwilini, lakini kuna vitu vinavyoweza kuiharibu ambavyo wataalamu wanavitaja viepukwe.
Hata hivyo figo linaweza kushindwa kufanya kazi hiyo kutokana na sababu mbalimbali, mojawapo ikiwa ni mtindo wa maisha, kama anavyoeleza Dk Shija.
Anasema uvutaji sigara, kula sana vyakula vya haraka kama chipsi, wanga au chakula kingi, kutofanya mazoezi na kutumia chumvi kwa wingi ni vitu vinavyochangia kuleta madhara kwenye figo, hivyo vinapaswa kuepukwa.
“Mgonjwa anapoingia kwenye hatua ya kuchuja damu ni kwa maisha yake yote na gharama zake ni kubwa. Wataalamu wanapaswa kutumia nguvu kubwa kuelimisha jamii. Wajue afya zao, wapime mara kwa mara,” anasema.
Dk Shija anashauri kupima uzito mara kwa mara, kufanya mazoezi, kuepuka vitu vya starehe kama sigara, pombe kali, dawa za kulevya, bangi na matumizi makubwa ya sukari kwani hivyo vyote vina madhara.
Mbali na hayo, Daktari bingwa wa magonjwa ya figo BMH, Sabina Mmbali anaeleza umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya kwa magonjwa yasiyoambukiza, hasa uchunguzi wa kisukari au shinikizo la damu angalau mara moja kwa mwaka na kupata matibabu sahihi, iwapo utagundulika kuwa na shinikizo la juu la damu au ugonjwa wa kisukari.