Wanywaji wa ‘Energy’ mnalijua hili?

Dar es Salaam. Kama unapenda kunywa kinywaji cha kuongeza nguvu, maarufu kama 'Energy drink' unatakiwa kufikiri upya.

Kwa mujibu wa wataalamu, kinywaji hicho kimetajwa kuwa na madhara hasi katika ogani ya moyo, figo na pia kikitajwa kusababisha damu kuwa nzito isivyo kawaida.

Inashauriwa angalau mtu asizidishe chupa mbili kwa wiki na kama atashindwa kabisa, basi asizidishe kopo moja lenye ujazo wa 250mls kwa saa 24, huku ikisisitizwa chaguo sahihi ni kuachana nayo kabisa.

“Madhara yanaweza kutokea hata mtu akinywa moja, ingawa visa vingi vya madhara vinahusishwa na unywaji mkubwa na endelevu. Uwezekano wa kupata madhara makubwa kwa anayekunywa chupa mbili kwa wiki ni mdogo, ila sio kwamba haupo.

“Suala la kuacha ni maamuzi binafsi, ila kwa mtu ambaye tayari ana uraibu na hawezi kuacha anahitaji matibabu ya kisaikolojia kama inavyokuwa kwenye kuacha pombe na sigara,” anasema Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, Pedro Palangyo.


Hali halisi

Ukizunguka katika maeneo ya kutupa takataka na vyanzo vya maji, chupa nyingi zinazoonekana ni za vinywaji hivyo vya kuongeza nguvu.

Hii inatoa picha namna unywaji wa kimiminika hicho unavyoongezeka kwa kasi kubwa kwa Watanzania, huku watumiaji wakiwa ni wa rika zote kwa kuwa wengi hawajui madhara, hasa vijana wenye miaka kuanzia 18.

Mara nyingi kinywaji hicho pia hupendwa na wafanyakazi wanaotumia akili na nguvu, wakiwamo pia madereva na wanaokimbia.

Mkazi wa Ubungo, Hamisi Zawadi anasema hutumia kinywaji hicho anapofanya kazi zake za kusafirisha abiria. Yeye ni dereva bodaboda, anasema asipokunywa hukosa hamu ya kufanya kazi.

“Hakuna siku imepita bila kunywa, naona kabisa kama nimepungukiwa kitu mwilini na ili niwe sawa, nakunywa kidogo na kuendelea na shughuli zangu za kila siku,” anasema.

Zainabu Kapili, mkazi wa Tabata Dampo anasema kutokana na kuzoea kunywa kinywaji hicho, amekuwa kama mlevi wa pombe, hata kama hana fedha atakopa ili tu apate kinywaji hicho.

“Mtu akinikataza nahisi kama amenipeleka polisi bila sababu, hata kipindi nilipokuwa na ujauzito nilihisi kama naonewa baada ya kuambiwa nisitumie hicho kinywaji kwamba ni hatari kwa afya ya mtoto,” anasema na kuongeza kuwa alishindwa hivyo alitumia angalau kidogo akae sawa.

Selemani Njovu, kuli katika soko la Mabibo, anasema bila kunywa kinywaji hicho anahisi hataweza kufanya kazi yoyote na wakati mwingine huangusha mizigo ya watu.

Yohana Kazimoto, ambaye ni dereva wa magari ya masafa marefu, anasema anatumia kinywaji hicho ili kukata usingizi anapokuwa njiani kwa kuwa kuna wakati anajikuta analala hata kama ametoka kuamka, hiyo yote ni kutokana na uchovu.

Mwanafunzi wa kidato cha tatu, Ramadhani Mohamed amekuwa muathirika kwa madai kuwa alitumia kwa muda mrefu kipindi alipokuwa kidato cha pili akikesha kwa ajili ya mitihani na tabia hiyo amekuwa nayo hadi sasa.

“Kama nataka kusoma au nina sinema nataka kutazama nakunywa kwanza energy drink, hapo sitolala wala kusikia kuchoka hadi nitakapoona nimemaliza,” anasema Ramadhani.


Maelezo ya wataalamu

Kwa mujibu wa wataalamu, kinywaji hicho kimetengenezwa kwa caffeine nyingi, pamoja na kemikali nyingine ambazo zina madhara kwenye kila kiungo cha mwili wa binadamu.

Kwa jumla hazifai kwa matumizi ya kila siku kwa binadamu, kwani kuna vimelea vya uraibu, hali ambayo inaweza kusababisha mtu kuihitaji wakati wote.

Dk Pedro, ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Utafiti Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), anasema unywaji wa vinywaji vya kuongeza nguvu huathiri mifumo yote kwenye mwili.

“Ukianzia juu kwenye mwili husababisha kufeli ghafla kwa figo, kukosa usingizi, kuharisha na kutapika, kichwa kuuma, mfumo wa chakula kuathirika, pia kutokea vifo vya ghafla na kuwa na mawe kwenye figo,” anasema.

Anasema kwa mujibu wa tafiti, matumizi ya vinywaji hivyo kwa watoto, huwakosesha usingizi na kusababisha kusikia vitu ambavyo havipo, matokeo yake wanachukua maamuzi ya kujiua.

Pia Dk Pedro anasema matukio ni mengi, lakini JKCI walichapisha kisa kimoja ambacho kilimhusisha kijana mwenye umri wa miaka 28 aliyeziba mshipa wa moyo kutokana na kutumia kiasi kikubwa cha kinywaji hicho kwa kunywa kopo tano ndani ya saa nne.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Dk Hanson Mwakifuna, anasema kuna madhara kwa wajawazito kutumia kwa sababu ya wingi wa caffeine ambayo ni hatari kwao.

“Huwa hatushauri kwa mjamzito kutumia vinywaji au vitu vyenye asili ya caffeine kwa ajili ya kumlinda mtoto, kwani inaweza kusababisha maumivu ya kichwa, mapigo ya moyo kwenda mbio, kujifungua mtoto kabla ya wakati, kujifungua mtoto aliyefariki na kujifungua mtoto chini ya uzito,” anasema.