Zamaradi anavyomzungumzia Ruge, michango ya matibabu

Muktasari:

Mtangazaji Zamaradi Mketema amesema Babu Tale ndiye aliyemkutanisha kwa mara ya kwanza na Ruge Mutahaba ambaye ni baba wa watoto wake wawili.


Dar es Salaam. Mtangazaji maarufu nchini, Zamaradi Mketema amesema Babu Tale ndiye alimkutanisha kwa mara ya kwanza na mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba.

Zamaradi ni mzazi mwenzie na Ruge ambaye wamezaa naye watoto wawili wanaoitwa Juju na Shuby, ameyasema hayo leo Alhamisi Februari 21, 2019 katika kipindi cha 360 kinachorushwa na kituo cha Clouds TV.

Kipindi hicho kwa siku ya nne sasa kimekuwa kikiwaita watu mbalimbali walio na mahusiano ya karibu na Ruge ambaye yupo chini Afrika Kusini kwenye matibabu miezi minne sasa.

Akielezea namna walivyokutana kwa mara ya kwanza, Zamaradi amesema ilitokea baada ya Babu Tale ambaye ni meneja wa msanii Diamond kumuona akiwa anatangaza kituo cha televisheni cha C2C na kumtambua ana kipaji ambacho anatakiwa awe sehemu nyingine watu wakione zaidi.

“Nakumbuka siku hiyo Babu Tale alinipa namba ya Ruge nimtafute na akaniambia nisiseme kama ni yeye kanipa na mwisho wa siku tukaonana nikamueleza nia ya kwenda kufanya kazi Clouds.”

“Haikupita muda alinipigia na nikajikuta ni mfanyakazi wa Clouds na ndiye aliyetaka niwe katika kipindi cha filamu ambacho wakati huo kilikuwa kikiitwa Movie leo,” amesema.

Akielezea namna walivyoingia kwenye mahusiano naye, amesema ilitokea tu kama binadamu japokuwa anakiri ilikuwa kazi ngumu kumkubalia kwa kuwa alikuwa amejiwekea malengo yake.

Hata hivyo, mwisho wa siku walijikuta wakikubaliana na ikatokea hivyo wakazaa hadi watoto wawili.

Kuhusu watoto kujua kama baba yao anaumwa, amesema wanajua na wameshaenda kumuona Afrika Kusini.

Akizungumzia Ruge ni baba wa aina  gani, Zamaradi amesema anashukuru ni mtu ambaye anatekeleza wajibu wake kwa watoto na pia amekuwa akipata muda huenda kushiriki shughuli mbalimbali za shuleni kwao.

Wakati kwa upande wake ameshamwambia kuwa ni mwanamke ambaye ana akili na anamuona hajawahi kutumia hata nusu ya akili zake hususani alipowahi kushuhudia akiombwa na baba wa miaka 55 amshauri kuhusu mtoto wake wa kike ambaye alijiingiza kwenye mapenzi.

Ushauri wake nini kifanyike katika kuchangia matibabu ya Ruge, amesema kungeitishwa harambee tena ya haraka kwa kuwa baba watoto wake huyo anahitaji msaada wa haraka.