Zanka, kata ndogo iliyokithiri vitendo vya mauaji, ubakaji
Bahi. Kata ya Zanka wilayani Bahi, imegubikwa na matukio ya mauaji na ubakaji, huku wananchi wakilalamika hatua stahiki kutochukuliwa na mamlaka husika.
Zanka ni kata ya siku nyingi inayoundwa na vijiji vya Zanka, Mayamaya na Mkondai, ikiwa na vitongoji sita vya Zamahero, Halo, Lulunde, Mkong'oni, Mtungutu na Mtita.
Kitongoji cha Zamahero kuna makazi ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.
Tukio la hivi karibuni lilitokea Mei 26 mwaka huu katika Kijiji cha Mayamaya, kilichopo umbali wa kilomita 41 kutoka Dodoma mjini, barabara iendayo Arusha.
Simulizi
“Ilikuwa saa moja usiku nilitoka kunywa pombe kilabuni, wakati narudi nikakutana na… (anamtaja mmoja wa vijana kijijini hapo), akanikaba kisha kunipeleka kwenye pagale lile na kuanza kunibaka akiwa na wenzake,” anasema Zawadi (si jina halisi).
Anasema alibakwa na watu wanne, pia alipigwa kichwani na kitu kizito kilichosababisha avuje damu puani, mdomoni na masikioni.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 34 ni mkazi wa kijiji hicho kwa kuzaliwa. Ana watoto wanne katika ndoa ambayo sasa imesambaratika.
Akizungumza na Mwananchi kijijini hapo, alisema tukio hilo lililotokea Mei 26, mwaka huu, akidai wahusika ni jirani zake.
Anasimulia kwamba siku hiyo baada ya shughuli zake za kujitafutia kipato, saa 11 jioni alikwenda kilabuni kunywa pombe.
Mwanamke huyo anasema saa moja usiku aliondoka kurudi nyumbani na kwamba huo ulikuwa utaratibu wake wa kawaida.
Hatua chache kutoka kilabuni anasema alikutana na jirani yake na alipompisha alishtukia akikabwa koo na kubebwa kwa nguvu.
“Alirudi nyuma kidogo kwenye nyumba ya mtu, aliniingiza kwenye pagale akaanza kunivua nguo. Wakati huo walishafika wenzake watatu (anawataja) wakaanza kunibaka kwa zamu,” anasema.
Anasema tukio hilo lilitokea mita 40 kutoka kilabuni ambako kwa wakati huo watu walijaa.
Mwanamke huyo anayetembea kwa shida huku sauti yake ikiwa ya chini kutokana na maumivu ya koo, anasema hakukumbuka kitu hadi alipojikuta amezungukwa na watu akiwa nje na amevishwa nguo zisizo zake.
Anasema wakati wa tukio hilo alimng’ata kwa meno mmoja wa watu hao na anaamini akipatikana atakuwa na alama kutokana na nguvu alizotumia kumng’ata. Pia anasema alichana shati la mmoja wao.
Mashuhuda
Asha Makula, muuza pombe kilabuni hapo alisema alimhudumia ‘kitochi’ kimoja (lita moja) mwanamke huyo saa 11.30 jioni na alikaa muda mfupi akaondoka akiongozana na mtu aliyetajwa pia na mama huyo.
“Muda wa kama saa moja tangu waongozane, alikuja tena mwanaume kuendelea kunywa pombe, lakini tukamuona nguo zake zimelowa damu na alipoulizwa aliwaambia wenzake kuwa alikuwa amebakwa, lakini hakufunga zipu ya suruali yake,” anasema Asha.
Kauli hiyo anasema iliwashtua, hivyo walitaka kujua ukweli, lakini dakika chache baadaye waliitwa na mmoja wa wazee kijijini hapo aliyekuwa akipita njia na kusikia mtu akikoroma kwenye pagale.
Anasema walipofika eneo hilo walimkuta mama huyo na kumsaidia kwa kumpatia huduma ya kwanza.
Katika eneo la pagale hilo anasema kulikuwa na chupi ya kiume ukutani ambayo mtu anayetajwa kuwa na shati lililokuwa na damu aliichukua na hajaonekana tena kijijini hapo.
Taarifa ofisi ya kijiji
Mhudumu wa ofisi ya kijiji, Amina Mikidadi alisema saa mbili usiku wa siku ya tukio alipokea simu kutoka kwa Asha kwamba kulikuwa na mtu amejeruhiwa kwenye pagale jirani na nyumbani kwake.
Alisema aliwasiliana na Mwenyekiti wa kijiji, Jonathan Chibalangu ambaye kwa wakati huo alikuwa mgonjwa ili atoe maelekezo ya nini kifanyike.
“Mwenyekiti aliniagiza kwenda eneo la tukio nikiwa na mgambo na balozi wa eneo husika, kweli alikuwa na hali mbaya huyu dada. Alikuwa amelowa damu mwilini, tulipeleka taarifa Polisi na baadaye tulimpeleka kituo cha afya kupata huduma ya kwanza,” alisema.
Mwenyekiti Chibalangu alisema taarifa zilisambaa kijijini na wanaendelea kuwasaka watuhumiwa waliokimbia kusikojulikana baada ya tukio.
Chibalangu alisema matukio ya uhalifu ni mengi katika Kata ya Zanka na yamekuwa yakiripotiwa Polisi, ingawa kwa sehemu kubwa ufuatiliaji huwa mdogo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno alipoulizwa na Mwananchi kuhusu tukio hilo alisema bado hajapata taarifa lakini atafuatilia.
Pia aliahidi kufuatilia matukio mengine yanayotokea kujua ukweli wake, ndipo ajue nini kifanyike.
Matukio mengine
Tukio la awali la ubakaji lilitokea mwaka 2020, mwanamke mmoja alibakwa na kuuawa lakini hakuna aliyekamatwa.
Katika kata hiyo pia kumeripotiwa matukio yenye kushabihiana ya watu kuuawa ndani ya nyumba.
Tukio la kwanza lilitokea katika kitongoji cha Zamahelo ambako familia ya baba, mama na mtoto waliuawa ndani ya nyumba yao.
Wakati wa tukio hilo lililotokea mwaka 2018 waliohusika na mauaji hawakuchukua chochote, zikiwemo Sh6 milioni zilizokutwa ndani ya nyumba.
Tukio hilo lilitajwa kuhusishwa na ugomvi wa kifamilia na kwamba baba wa marehemu alilalamika awali akitaka Serikali kuchukua hatua hata kama waliokuwa wakihusika na ugomvi ni wanafamilia.
Mwaka 2017 mwananchi kutoka jamii ya wafugaji aliuawa mchana kwa kuchinjwa akitokea kwenye kesi ya mgogoro wa shamba kati yake na aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Rister Chedego.
Mfugaji huyo alikutwa ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali.
Polisi walipokwenda kuuchukua mwili kulikutwa simu iliyotambuliwa kuwa ni ya Chedego, alikamatwa na kuachiwa baadaye kwa kukosekana ushahidi.
Januari 15, 2022 iligundulika miili ya watu watano wa familia moja katika kijiji cha Zanka baada ya watoto waliokuwa wakicheza kusikia harufu na kuona inzi wakizengea katika nyumba hiyo.
Waliokutwa wamefariki dunia ni wanandoa Hosea Kapande na Paulina Kalonga na watoto wao (Agnes na Isaka) na mjukuu wao Heltone. Vifo hivyo vilihusishwa pia na migororo ya kifamilia, lakini mauaji ya kutumia vitu vizito kichwani yalikuwa kama ilivyokuwa kwenye vifo vya watu watatu.
Katika tukio hilo hakuna kilichokuwa kimechukuliwa ndani, ikiwemo mifugo nje ya boma ambayo wanafamilia waliendelea kufungulia na kupeleka machungaji, huku ndani kukiwa na maiti za watu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Zanka, Yohana Japhet alisema tukio hilo lilikiweka katika wakati mgumu.
Makamu wa Rais, Dk Mpango alifika katika familia hiyo na kuagiza vyombo vyote nchini kufanyia kazi mauaji hayo mara moja na taarifa rasmi ya kazi hiyo iwasilishwe kwa Rais, Samia Suluhu Hassan ndani ya siku saba.
Wananchi walia na usalama
Aliyekuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Dodoma, Ismal Jama ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mayamaya, alisema hali ya usalama kwa sasa ni tishio. Jama alisema zamani katika kijiji hicho hakukuwa na mauaji wala matukio ya kutisha, lakini inashangaza kwa sasa kusikia matukio katika kata hiyo.
Alisema matukio mengi yanatokea na vijana wanaotajwa kutoka kijiji au kwenye kata hawachukuliwi hatua.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mayamaya, Chibalangu alisema kumekuwa na shida ya mawasiliano kati ya uongozi wa kijiji na kituo kidogo cha Polisi Zamahero kwa kuwa kila wanapotoa taarifa za matukio inachukua muda kuchukua hatua.
Kituo cha Zamahero kipo ndani ya kata hiyo, umbali za kilomita moja kutoka Mayamaya na kilomita nne kutoka Zanka, lakini wanadaiwa hawafiki kwa wakati kwenye matukio na wakati mwingine hawafuatilii kabisa.
Chibalangu alisema yanapotokea matukio kama hayo, mara nyingi wamekuwa wakichukua hatua za haraka, lakini wanashindwa kwenda zaidi, hasa matukio yanapokuwa yameripotiwa vituo vya Polisi.