Zanzibar, Bara kushirikiana uwezeshaji wananchi

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Being'i Issa (kulia) akikabidhiana hati ya makubaliano na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Juma Amour Mohammed Leo Mei 11 Jijini Dodoma.
Muktasari:
- Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) zimeingia makubaliano ya kushirikiana katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali kwa kipindi cha miaka mitatu.
Dodoma. Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), zimeingia makubaliano ya kushirikiana katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali kwa kipindi cha miaka mitatu.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo, alhamisi Mei 11, 2023; Jijini hapa na Katibu Mtendaji wa NEEC Being'i Issa na Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA,Juma Amour Mohammed.
Kwa upande wa NEEC Being'i amesema watashirikiana kwenye utafiti wa sera za uwezeshaji pamoja na kufanya tathmini kwenye mambo ambayo watashirikiana.
"Sisi ni Baraza wao ni Wakala, tupo tofauti tutaangalia mapungufu tuliyonayo yasijitokeze kwao, lakini kubwa ni kuhakikisha wanafanikiwa kwenye shughuli mbalimbali wanazofanya," amesema Katibu Mtendaji huyo.
Naye Mohammed amesema wakala wa uwezeshaji wananchi kiuchumi Zanzibar ni taasisi mpya ambayo ina umri wa mwaka mmoja, na kwamba katika kipindi hivgo ZEEA imefanikiwa kutoa mafunzo na mikopo kwa zaidi ya wananchi 18,493.
"Naomba nitoe shukrani za dhati kwa mashirikino makubwa mliyotupatia na miongozo ya kiutendani inayotuwezesha kutekeleza majukumu yetu ya kitaifa ya kuwawezesha wananchi kiuchumi," amesema Mohammed.