Zanzibar kutumia Sh2 bilioni kwenye maji

Muktasari:

  •  Kabole amewasisitiza Watanzania kutumia vizuri maji na kutunza vyanzo vyake kwani vinaonekana kuanza kupungua

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejiwekea mkakati wa kutumia Sh2  bilioni mwaka huu kwa ajili  ya maji safi na salama na usafi wa mazingira.

Fedha hizo hutengwa kila mwaka kwa ajili ya kukabiliana na kipindupindu. Waziri wa Afya Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo ameyasema hayo leo Jumatatu, Julai 31 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa mkakati wa miaka mitano wa shirika la WaterAid.

Amesema Zanzibar imefanikiwa kukabiliana na kipindupindu hivyo imeamua kuchukua hatua stahiki kuhakikisha ugonjwa huo haurudi tena.

Miongoni mwa hatua hizo ni kuhakikisha wakazi wanapata maji safi na salama na kutunza mazingira yao.

"Wenzetu wa Water Aid wametusaidia sana kule Zanzibar, maana hapo awali ilikuwa mgonjwa ukienda hospitalini unaweza kurudi na maradhi mengine kutokana na kukosekana maji," amesema.

"Tumefanikiwa kumaliza kipindupindu ila tumejipanga kuhakikisha hakirudi tena ndiyo sababu nasema hata fungu lililokuwa likitengwa kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo kila mwaka tutalitumia kuleta maji safi,"amesema Kombo.

Mkurugenzi Mkazi wa WaterAid Tanzania, Dk Ibrahim Kabole amesema suala la upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira unapaswa kuwa ajenda ya kitaifa.