Zindiko la Magufuli si hirizi, talasim wala tunguri

Thursday February 11 2021
zindikopic

Rais John Magufuli

By Mwandishi Wetu

Zindiko ni kinga dhidi ya ubaya unaoweza kumpata mtu, familia au jamii. Kwa mfano inatafutwa chanjo – zindiko dhidi ya Covid-19 ili kuikinga jamii dhidi ya maambukizo, madhila na madhara yanayotokana na corona. Katika makala hii nimetumia istilahi hii ya zindiko kama istiari.

Katika demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchi ni mali ya umma na dola ni nyenzo ambayo umma unatoa ridhaa kwa njia ya kura kwa chama cha siasa, kitakachokidhi mahitaji, matakwa na matarajio yake. Wenye matamanio ya kisiasa wanauunda chama cha siasa kisheria kama mtaji pia ni dhamana ya utumishi kwa umma.

Wanachama kindakindaki wa vyama hivyo huwa ni wachache kuliko wasio na chama. Wanakuwa na mashabiki pande zote ambao wakikutana na wapinzani wao basi huwa ni kindumbwendumbwe-chalia. Hii ni demokrasia ya wengi kuwapa ridhaa wachache waendeshe dola.

Wakati tunapata uhuru vilikuwepo vyama vingi vya siasa kama Tanu, ANC, UTP, AMNUT, ASP, ZNP na ZPPP. Katika mabadiliko ya Katiba ya 1965 ikabaki Tanu na ASP.

Waasisi wetu waliona mbali busara ya kuwa na chama kimoja ili kujenga taifa na utaifa kwanza. Kwa miaka mingi Tanu/ASP ambavyo vilikuja unda CCM, vilipata ridhaa ya umma kuongoza dola.

Baada ya itikadi zenye mrengo wa ujamaa kupigwa vita, itikadi ya kibepari na mifumo ya uliberali-mpya ikajiimarisha kwa jina la utandawazi. Maana iliyojificha ilikuwa kutoa kibali kwa makampuni makubwa kutawala dunia na kufanya watakavyo bila vipingamizi serikalini. Tuliaminishwa ubebari utatuletea utajiri; Serikali nyingi Afrika zikatii masharti kutoka Shirika la Fedha Duniani na Benki ya Dunia.

Advertisement

Soko huria liliruhusu mitaji, huduma na bidhaa bila vikwazo lakini si watu; tukafundishwa demokrasia, ubinafsishaji wa makampuni ya Serikali, utawala bora na si uongozi bora! Sera, na sheria za kisiasa, kiuchumi na kijamii zikibadilishwa kukidhi mahitaji ya utandawizi. Sasa ikawa hadithi ya Alfu lela ulela, kuduria ufukara usiyo kwisha.

Februari 1991 ikaundwa Tume ya Nyalali kupata maoni kuhusu demokrasia ya vyama vingi. Wengi walikataa, muafaka ukawa maoni ya wachache yaheshimiwe. Waafrika tunajitahidi kuelewa mantiki ya vyama vingi lakini bila muafaka wa kitaifa kuhusu itikadi itakayoongoza maisha yetu kama taifa moja, tutakuwa kama nazi ndani ya pakacha, sokoni kila mtu na bei yake. 1967 tulipania kujenga taifa letu kwa misingi ya ujamaa kama falsafa itakayotuongoza kisiasa na kujitegemea katika kujenga uchumi unazingatia haki.

Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi 1995 ulisisimua na umma ulifuatilia. Kwenye kampeni wagombea ngazi zote walijitokeza na mdahalo wa kwanza kwa wagombea urais ulifanyika. Alikuwepo Mkapa-CCM, Mrema-NCCR, Cheyo-UDP na Lipumba-CUF. Umma uliipa ridhaa CCM.

Katika uchaguzi wa 2015 JPM hakuwa anajulikana sana nje ya nchi na wengi tulimjua kama askari wa mwamvuli na Waziri wa Kitoweo. Baada ya JPM kutangazwa kuwa mshindi hakulaza damu ikawa hapa kazi tu! Wengi hatukuelewa namna alivyokuwa anaendesha Serikali na nchi lakini tulianza kuona matokeo. Kama kawaida kwenye mabadiliko kuna wanaofaidika na wanaoumia.

Uchaguzi wa 2020 ambao ulikuwa mfupi bila mbwembwe nyingi ndio ulitarajiwa uwe msemakweli. Inaelekea wapiga kura wengi waliridhika na mabadiliko waliyoyashuhudia katika miaka mitano. Zindiko la kwanza la JPM likawa elimu ya uraia kwa vitendo, kwamba kila kitu kinawezekana. Ukiwa na dhamira safi ya kubadilisha mtazamo na vitendo vyako hata beberu atabadilika.

Zindiko la pili imethibitika nchi yetu na watu wake ni matajiri kwani tuna watu na ardhi. Tunachohitaji ni kuwa na “itikadi ya jamii” itakayotuunganisha kama taifa na uongozi thabiti unaosimamia maslahi ya wengi. Kwa hakika hakuna nchi inayoweza kujitegemea mia kwa mia lakini unapotambua thamani yako hawatakunyonya.

Zindiko la tatu tumejifunza huduma zinazoonekana, zinazoshikika, zinazohesabika ni jukumu la Serikali hata bila chama cha siasa. Kazi kubwa ya Serikali ni kutoa huduma kwa haki na usawa iwe katika afya, maji, elimu, miundombinu au sheria. Chama cha siasa kinaelekeza utekelezaji kwa kuzingatia itikadi yake.

Changamoto kubwa 2025 kwetu sote ni kufanya tathmini ya mafanikio tuliyopata na changamoto zake. Ili Chama cha siasa kijenge utaifa na kusimamia utekelezaji wa maendeleo kinatakiwa kielewe maono sahihi ya umma na kuyatafsiri kwa vitendo. Chama ni roho faida zake hazionekani kwa macho.

Kabla ya 2025 tuwe na muafaka ndani ya Katiba tunataka taifa la kijamaa na kujitegemea au ubinafsi na utegemezi?

Vyama vipewe Ilani ya Wananchi ili vijieleze vitakayotekeleza katika muktadha wa Katiba na muungano wa Afrika. Wakati wa kila chama na itikadi yake umekwisha, nguo za kuazima hazisitiri mwili. Tusonge mbele; rasilimali zinazotumika ni jasho letu!

Imeandikwa na Marie Binti Shaba

Advertisement