Zitto aomba Tume ya Rais kumaliza migogoro ya ardhi

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe

Muktasari:

  • Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuunda Tume maalum kushughulikia na kumaliza migogoro ya ardhi nchini.

Kasulu. Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuunda Tume maalum kushughulikia na kumaliza migogoro ya ardhi nchini.

Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Kasulu jana, Zitto alisema pamoja na kusikiliza maoni na ushauri kutoka kwa wananchi, tume hiyo pia inapaswa kutoa kupitia na kutoa mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya ardhi ili iendane na mahitaji ya sasa na wakati uliopo.

‘’Rais Ali Hassan Mwinyi aliwahi kutumia mfumo wa kuunda tume kushughulikia masuala ya ardhi, namshauri Rais Samia kuiga mfano huo kumaliza migogoro ya ardhi inayoshuhudiwa maeneo mbalimbali nchini,’’ amesema Zitto

Amesema sheria ya sasa ya ardhi ilitokana na maoni ya wananchi na mapendekezo ya Tume ya Rais iliyoongozwa na Profesa Issa Shivji mwaka 1991, hivyo kuna haja ya kuipitia upya ili iendane na wakati.

Zitto ambaye yuko kwenye ziara ya kichama katika majimbo yote ya uchaguzi ya Mkoa wa Kigoma alitaja eneo lingine muhimu la kuangalia na tume anayopendekeza iundwe kuwa ni mipaka kati ya maeneo ya Uhifadhi na vijiji ili kumaliza migogoro ambayo inayorudisha nyuma siyo tu masuala ya uhifadhi, bali pia maendeleo na ustawi wa watu.

‘’Sote tunatambua na kukubaliana umuhimu wa uhifadhi kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo; lakini hiyo haiondoi ukweli kwamba jukumu la kwanza la Serikali ni ustawi na maendeleo ya watu. Hatuba budi kuangalia hili kwa umakini mkubwa,’’ amesema

Akifafanua, Zitto alisema wakati wa kutenga na kuweka mipaka ya maeneo ya hifadhi, idadi ya watu na mahitaji ya ardhi kwa shughuli za kibinadamu ilikuwa ndogo kulinganisha na sasa, hivyo ni vema Serikali kupitia maoni ya wananchi na ushauri wa kitaalam iangalie namna ya kuendeleza uhifadhi bila kuathiri maisha na mahitaji ya watu.

Awali, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kigoma, Sendwa Ibrahim alitaja migogoro ya mipaka kati ya vijiji na maeneo ya hifadhi kuwa miongoni mwa kero ya ardhi inayowakabili wananchi mkoani humo.

‘’Mipaka ya vijiji na pori la Makere Kusini maarufu kama Kagera Mkanda Wilaya ya Kasulu ambako kitongoji kizima cha Katoto kinafutwa kupisha uhifadhi ni kati ya mgogoro unaohitaji ufumbuzi kurejesha amani kati ya wananchi na uhifadhi,’’ amesema Sendwa

Alitaja vijiji vya Kiirirani, Songambele na Rukoma vilivyoko Wilaya ya Uvinza kuwa baadhi ya maeneo yenye migogoro ya mipaka kati ya vijiji na hifadhi na kumwomba Zitti kupitia uwezo na ushawishi wake kusaidia ufumbuzi.

Mwenyekiti huyo alitaja madai ya uongozi wa magereza mkoa wa Kigoma kujiongezea ardhi kinyemela kutoka hekari 600 iliyotolewa na uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Ilagala hadi kufikia zaidi ya hekari 10, 000 kuwa ni mgogoro mwingine unaotakiwa kutafutiwa ufumbuzi mkoani Kigoma.