Waziri Silaa ajitosa migogoro ya ardhi, aomba ushirikiano

Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa

Muktasari:

  • Maswali ya kuhusu migogoro ya ardhi toka kwa wabunge na wananchi kwa ujumla, yamekuwa ni mengi, na mara nyingi wabunge wanahoji kwa nini Serikali isijikite kutafuta suluhisho la kudumu juu ya migogoro hiyo, na hapa sasa ndipo waziri mwenye dhamana na ardhi, anaomba ushirikiano ili kuimaliza migogoro hiyo.

Dodoma. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa, amejitosa kushughulikia migogoro ya ardhi, huku akiomba ushirikiano toka kwa wabunge, na kwamba atazunguka nchi nzima lengo likiwa ni kuhakikisha migogoro hiyo inakwisha.

Silaa ametoa kauli hiyo bungeni leo Septemba 6, 2023, wakati wa majibu ya swali la nyongeza la Mbunge wa Mbomba (CCM), Condester Sichalwe, ambaye ameuliza ni lini migogoro ya ardhi itakwisha nchini.

“...Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani hizo nawaomba wabunge wawe watulivu na watupe ushirikiano, baada ya bunge hili, kuanzia wiki ijayo tutaanza ziara nchi nzima kwa ajili ya kuangalia na kutatua migogoro ya ardhi na kuimaliza,” amesema Silaa.

Waziri huyo pia ameagiza wakuu wa mikoa kote nchini kuendelea kutatua migogoro ya ardhi kama ilivyoagizwa na Kamati ya Mawaziri nane, ili wananchi waendelee na shughuli zao.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum, Stela Fiyao, ameuliza Serikali ina mpango gani wa kutoa hati kwa maeneo yote ya umma katika halmashauri za Mkoa wa Songwe ili kuondoa migogoro.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Gofrey Pinda, amesema katika halmashauri tano za Mkoa wa Songwe, jumla ya maeneo ya umma 1, 679 yanatumika kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo shule, zahanati, vituo vya afya na hospitali.

Matumizi mengine katika maeneo hayo ni vyuo, ofisi, vituo vya polisi, mahakama, maeneo ya majeshi, hifadhi za misitu na wanyama na maeneo ya makumbusho yanayotumiwa na Serikali au taasisi.

“Aidha, maeneo 892 yameshapimwa ambapo kati ya hayo, maeneo 637 yameshamilikishwa na kutolewa hatimiliki. Ili kuongeza kasi ya umilikishaji wa maeneo ya matumizi ya umma, Serikali imefanya jitihada madhubuti ikiwemo kuondoa au kupunguza baadhi ya gharama za umilikishaji wa maeneo hayo,” amesema Pinda.

Hata hivyo amesema baadhi ya taasisi za Serikali, zikiwemo halmashauri zimeshindwa kutenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya umilikishwaji wa maeneo yao, na akatoa rai kwa viongozi wa Serikali na wakuu wa taasisi nchini wakiwemo viongozi wa halmashauri za Mkoa wa Songwe, kuhakikisha wanatenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya kugharamia upimaji na umilikishwaji.