Zitto azungumzia uhusiano wa ACT Wazalendo na Lowassa

Muktasari:

  • Mwaka 2015, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliachana na CCM na kutimkia Chadema. Hata hivyo, kabla ya kutoka CCM alikuwa akihusishwa na ACT Wazalendo kwamba alikuwa nyuma ya kuanzishwa kwa chama hicho kwa lengo la kwenda kugombea urais.

Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amezungumzia uhusiano uliokuwepo kati ya chama chake na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

 Lowassa alifariki dunia jana, Februari 10, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alipokuwa akipatiwa matibabu.

Akizungumzia kifo cha Lowassa leo, Februari 11, 2024 jijini Dar es Salaam, Zitto amesema mwaka 2015, ACT Wazalendo ndiyo kilikuwa kimeanza na yaliibuka maneno kutoka kwa watu wakisema chama hicho kimeanzishwa na Lowassa, ili akikatwa CCM akagombee huko.

Amesema baada ya Lowassa kukatwa CCM, alikwenda kujiunga na Chadema ambako alipata fursa ya kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho.

Zitto ameeleza kuwa Lowassa alimweleza kwamba watu wake wamefanya uchunguzi na uchambuzi, wameona ili kuwa na kampeni ya uhakika, ni vema vyama vyote vya siasa vikaungana na iwapo atajiunga na ACT Wazalendo, Chadema hawatakubali yeye kuwa mgombea wa vyama vyote vya upinzani Tanzania.

“Kwa hiyo, alilazimika kwenda Chadema, hakuweza kujiunga na ACT Wazalendo na mimi nilimwelewa na nilikuwa na Profesa Kitila Mkumbo…tukakubaliana kwamba yeye atagombea kupitia Chadema, lakini sisi tumpatie orodha ya majimbo ambayo tunadhani tunaweza tukashinda na yeye atatusaidia kuhakikisha tunashinda. Tuliandaa na mkataba kabisa.

“Na kweli alitusaidia kwa njia tofauti tofauti, tukashinda jimbo moja na yeye hakufanikiwa kushinda urais,” amesema Zitto.

Amesema uamuzi Lowassa wa kutoka CCM kwenda upinzani ulikuwa wa kukomaza demokrasia, ingawa baadaye iliporomoka, lakini wakati wake ilipiga hatua kubwa na ilikuwa ni wajibu wa upinzani kushikilia nguvu ile.

Amesema ulifika wakati upinzani ulikuwa na mawaziri wakuu wawili wastaafu (Lowassa na Fredrick Sumaye) na waziri kiongozi mstaafu (Hayati Maalim Seif Shariff Hamad).  Amesema wakati ule ulikuwa mzuri na kama wangetumia uzoefu wa watu hao, leo kungekuwa na siasa imara, lakini hawakuweza.

“Leo mzee wetu (Lowassa) ametangulia mbele za haki, tumpe hiyo heshima yake anayostahili,” amesema Zitto alipohojiwa na Mwananchi Digital.

Ataja alama ya Lowassa Udom

Zitto amesema Lowassa ni mtu wa kufanya uamuzi, hakuwa analegalega na kwamba Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kwa mfano, ni matokeo ya utendaji wake. Amesema si yeye aliyetoa wazo la kujenga chuo hicho, ni Rais Jakaya Kikwete, lakini yeye alisimamia utekelezaji wake.

“Rais Kikwete alikuja bungeni Desemba 30, 2005 akasema tunahitaji kuwa na chuo kikuu cha tatu kikubwa baada ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua). Baadhi yetu tulipinga, tukasema kwanini tusiimarishe vyuo vingine, lakini Kikwete alitamka kwamba ifikapo Septemba, Chuo Kikuu cha Dodoma kianze.

“Waziri Mkuu Lowassa akasimamia na ikawa. Haikuwa kazi rahisi, wakikuhadithia watu waliokuwa kwenye huo mchakatio, utaona ni namna gani Lowassa alikuwa ni tofauti na wanasiasa wengine,” amesema.

Amesema Lowassa aliibana mifuko ya hifadhi ya jamii kuhakikisha vinabeba jukumu la ujenzi wa chuo hicho ambacho sasa kimesimama na kuwa moja ya vyuo vikuu vikubwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na kaskazini mwa Mto Limpopo.

“Natoa wito kwa Serikali, namshauri Rais wa Tanzania, kwamba pamoja na kuwa kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma ulikuwa ni uamuzi wa Rais, lakini aliyesimamia utekelezaji huo ni Edward Lowassa, kwa hiyo tupate kitu pale Udom kama kumbukumbu ya Lowassa.

“Ningeshauri kwa heshima ya Lowassa, ukumbi mkubwa pale Udom wa Chimwaga uitwe ‘Edward Lowassa Chimwaga Hall’ iwe kumbukumbu ya juhudi zake za kuhakikisha chuo hicho kinakamilika,” amesema Zitto.

Mwanasiasa huyo amesema kipindi hicho mradi wa Udom ulikuwa wa pili kwa ukubwa baada ya reli ya Tanzania – Zambia (Tazara), hata hivyo ulikuwa ni mradi mkubwa uliojengwa kwa fedha za ndani tofauti na Tazara ambao ulikuwa ni mkopo kutoka China.

Alimuahidi Uwaziri Mkuu

Zitto amesema Lowassa alikuwa akimtania kwa kumwita “Mr Prime Minister”, kwani alimwahidi kwamba akishinda urais atamteua kuwa Waziri Mkuu na wakati wote aliokuwa akikutana naye alikuwa akimwita “Mr Prime Minister” kwa maana ya Waziri Mkuu.

“Alikuwa anapenda kunitania kwamba yeye atakapokuwa Rais, ataniteua mimi kuwa Waziri Mkuu wake. Kwa hiyo, tulikuwa tunataniana, tulipokuwa bungeni nikienda kumsalimia kwenye kiti chake, anasimama na kusema Mr Prime Minister au nikienda kwenye ofisi yake binafsi, nikiingia anasimama, anasema Mr Prime Minister,” amesema.