Zombe agoma kuhojiwa badala yake DCI amwamuru aandike maelezo yeye mwenyewe (52)

Tuesday April 06 2021
zombepic

Katika sehemu ya 51 ya simulizi hii ya kesi ya Zombe, shahidi wa 35 ambaye ni mlinzi wa amani aliieleza mahakama jinsi mshtakiwa wa 11 alivyofikishwa mbele yake na kutoa maelezo ya ungamo akielezea tukio zima la mauaji ya wafanyabiashaa hao.

Hii ni simulizi ya kina ya kesi ya Zombe, kesi ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi (RCO) Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe, Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OC-CID) ya Kinondoni, Mrakibu wa Polisi (SP), Christopher Bageni na askari polisi wengine 11.

Washtakiwa hao walidaiwa kuwaua kwa makusudi wachimba madini watatu kutoka Mahenge wilayani Ulanga huko mkoani Morogoro ambao ni Sabinus Sabinu Chigumbi maarufu kama Jongo pamoja na mdogo wake Ephraim Chigumbi, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, dereva teksi wa jijini Dar es Salamaa aliyekuwa akiwaendesha.

Walikuwa wakidaiwa kuwapiga risasi katika Msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam. Tukio hilo lilitokea Januari 14 mwaka 2006 baada ya kuwatia mbaroni huko Sinza Palestina, nyumbani kwa mchimbaji mwenzao, walikokuwa wamempelekea mkewe fedha wakihusishwa kupora pesa katika gari la kampuni ya Bidco.

Leo tunaangalia ushahidi wa shahidi wa 36 katika kesi hiyo. Kumfahamu alikuwa ni nani na alisema nini...endelea kufuatilia sehemu hii ya 52.

Mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, ACP Abdallah Zombe mara kadhaa kwenye maswali ya mawakili wake kwa mashahidi wa Jamhuri (upande wa mashtaka) alikuwa akilalamikia kukamatwa na kushtakiwa kwa mauaji hayo bila kupewa nafasi ya kusikilizwa kwa maana ya kuandika maelezo yake.

Advertisement

Mbali na mawakili wale, Zombe mwenyewe aliwahi kuwashtumu waendesha mashtaka na kulalamika kuonewa kwa kukamatwa na kushtakiwa bila kuandika maelezo yake akisema ni kinyume cha sheria na Katiba ya nchi ambavyo vyombo vya ulinzi na usalama vinailinda na kuifuata katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Lakini Septemba 24 mwaka 2008, shahidi wa 36 alijibu hoja na madai hayo ya Zombe pamoja na mambo mengine akibainisha kuwa mshtakiwa huyo alikataaa kuhojiwa kuhusiana na mauaji hayo.

Shahidi huyo wa 36, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Sidney Mkumbi alikuwa kiongozi wa timu ya upelelezi wa mauaji hayo iliyoundwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Adadi Rajab.

DCI aliunda timu hiyo kutokana na mapendekezo ya Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Kipenka iliyopendekeza katika ripoti yake ya uchunguzi wa mauaji hayo kuwa askari waliowatia mbaroni wachimba madini hao ndio wanawajibika kwa vifo vyao na ikapendekeza upelelezi zaidi ufanyike kuwahusu ili ukweli ujulikane.

Katika ushahidi wake akiongozwa na mkuu wa jopo la waendesha mashtaka, wakili wa kujitegemea Revocatus Mtaki, shahidi huyo kutoka makao makuu ya upelelezi alikokuwa akishughulika makosa dhidi ya binadamu yakiwamo mauaji, pamoja na mambo mengine, alisema Zombe alikataa kuhojiwa walipomfuata.

SACP Mkumbi aliieleza mahakama kuwa Februari 18 mwaka 2006 mkuu wake wa kazi, DCI Adadi Rajabu alimpa jukumu la kuongoza timu ya upelelezi wa mauaji hayo.

Kwa mujibu wa ushahidi wake, walianza upelelezi kwa kuwahoji kwanza maofisa wanane wa polisi kati ya 15 waliokuwa wamependekezwa na Tume ya Jaji Kipenka ambao walikuwa tayari wametiwa mbaroni.

SACP Mkumbi aliwapa jukumu wakaguzi kuchukua maelezo ya watuhumiwa saba ambao walikuwa mahabusu katika kituo kikuu cha polisi huku yeye na shahidi wa 30, ACP Emson Mmari wakienda Kituo cha Polisi Selander Bridge alikokuwa mshtakiwa SP Bageni, mmoja wa washtakiwa katika kesi hiyo.

Watuhumiwa wote waliokuwa kituo kikuu cha polisi walichukuliwa maelezo yao lakini SP Bagen alimweleza SACP Mkumbi na mwenzake kuwa alikuwa amefiwa na dada yake na kwamba kwa hali aliyokuwa nayo hakuwa tayari kutoa maelezo yake hasa kama wakili wake hatokuwapo hivyo wakamwacha bila kuchukua maelezo yake.

Timu hiyo ilienda maeneo yote yaliyokuwa yakihusishwa katika kesi hiyo ikiwamo Sinza Palestina, mahali wachimba madini hao walikokamatiwa wakiwa wamempelekea mke wa mchimbaji mwenzao fedha za matumizi.

Maeneo mengine ni waliyoenda ni Barabara ya Sam Nujoma ulikofanyika uporaji wa fedha kwenye gari la makusanyo ya mauzo ya bidhaa za kampuni ya Bidco, tukio ambalo washtakiwa ambao ni askari polisi waliwahusisha wachimba madini hao.

Vilevile, timu hiyo ilitembelea ulipo ukuta wa Posta mahali ambako washtakiwa walidai kuwa yalitokea mapambano yaliyohusisha kurushiana risasi kati yao na waliowaita majambazi (wachimba madini).

Katika eneo hilo, timu hiyo ilifanya mahojiano na watu wanaoishi nyumba zilizopo jirani waliosema hawakuwahi kusikia mapambano ya risasi Januari 14 ya mwaka 2006.

Machi 6 mwaka 2006, aliyekuwa kamanda wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi (CP), Alfred Tibaigana alimpigia simu SACP Mkumbi kumweleza kuwa kulikuwa na mtuhumwa mwingine aliyekuwa tayari kujisalimisha. Huyo alikuwa Koplo Rashid Lema (mshtakiwa wa 11).

Alipoulizwa kuwa alikuwa wapi na kwa nini ameamua kujisalimisha, Koplo Rashid alijibu kuwa alikuwa mafichoni lakini ameamua kujisalimisha kwa kuwa roho ilikuwa inamsuta na kwamba kule mafichoni alikokuwa walitaka kumlisha nguruwe.

Hivyo alipelekwa kwa mlinzi wa amani, hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kinondoni, Omar Mohamed Abdallah aliyekuwa shahidi wa 35 ambako alieleza ukweli wa tukio zima tangu wachimba madini wale walipokamatwa Sinza Palestina kisha kupelekwa Sam Nujoma mahali palipodaiwa kuporwa fedha za Bidco.

SACP Mkumbi aliieleza mahakama kuwa baada ya mahojiano hata mshtakiwa wa pili, SP Bageni aliridhika kuwa hawakuwa na hatia lakini baada ya kuzungumza na kiongozi mwandamizi aliyekuwa akimuita afande, aliwaeleza askari wale kwamba afande wake huyo ameagiza wauawe.

Hivyo, waliwapeleka Msitu wa Pande kwa msaada wa askari polisi kutoka katika kituo kidogo cha polisi Mbezi Luis aliyewaongoza kwenda Msitu wa Pande ambako waliwaua wafanyabiashara hao kwa kupigwa risasi yeye na Koplo Saad.

Alieleza kuwa baadaya hapo miili hiyo ilipakiwa kwenye gari na mshtakiwa wa 11 kisha ilipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Shahidi huyo aliendelea kuileza mahakama kuwa siku iliyofuata, mshtakiwa wa 11, Koplo Rashid aliiwapeleka yeye na timu yake katika Msitu wa Pande mahali mauaji yalikofanyika, wakachukua sampuli ya damu iliyokuwa imeganda kwenye udongo na kuipeleka kwa mkemia mkuu wa Serikali kwa uchunguzi, na wakaokota maganda mawili ya risasi eneo hilo.

Kutoka katika msitu huo wa Pande, SACP Mkumbi aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa huyo wa 11 aliwapeleka Bunju mahali ambako yeye na Koplo Saad walifyatua risasi tisa walizozielekeza ardhini.

Kwa mujibu wa SACP Mkumbi, baadaye, Julai 2006, Koplo Rajabu Bakari (mshtakiwa wa 12) naye alijisalimisha mwenyewe na alipohojiwa walibaini maelezo yake yalikuwa yakifanana na yale ya mshtakiwa wa 11, Koplo Rashid.

Kuhusu ACP Zombe, SACP Mkumbi aliieleza mahakama kuwa kutokana na maelekezo ya Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP), alimwita ACP Zombe ili atoe maelezo yake lakini hakuwa tayari kufanya hivyo akidai kuwa alikuwa ameshatoa maelezo yake kwa IGP kujibu mashtaka ya kinidhamu.

Baadaye aliitwa na DCI, Adadi Rajab ambaye alimwamuru ACP Zombe kuandika maelezo yake naye akatekeleza hilo kisha jalada la upelelezi wa kesi hiyo likapelekwa kwa DPP ambaye alimuunganisha kwenye kesi.

SACP Mkumbi alisema kati ya watuhumiwa 15 ambao Tume ya Kipenka ilipendekeza washtakiwe, watatu kati yao, yaani Frank, James na Saad walikuwa hawajulikani walipo.

SACP Mkumbi aliileza mahakama kuwa katika upelelezi wao wote wa kesi hiyo walibaini kuwa tukio la uporaji wa fedha za Bidco ulifanywa na Ramadhani Manyanya (shahidi wa 25) na kundi lake.

Shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa walizingatia maelezo ya washtakiwa wa 11 (Koplo Rashid) na wa 12 (Koplo Rajabu) na matokeo ya uchunguzi wa Mkemia Mkuu wa Serikali kuhusu sampuli nne za damu kuwa ni za binadamu.

Zaidi alieleza kuwa kulikuwa na ushahidi kutoka Sinza Palestina kuwa washtakiwa walitiwa mbaroni wakiwa wazima na bastola yao ikawa imechukuliwa, hivyo madai ya kuwepo kwa tukio la kurushiana risasi kama washtakiwa hasa viongozi walivyodai, hayawezi kuibuka.

Pia alieleza kuwa vitabu vya kumbukumbu za silaha (armoury registers) za vituo vya polisi Chuo Kikuu na Urafiki vilionyesha hapakuwa na risasi zilizokuwa zimetumika kutoka kwa silaha walizokuwa wamepewa askari polisi wa vituo hivyo siku hiyo ya tukio.

SACP Mkumbi alieleza mahakama kuwa ni kitabu kimoja tu cha kumbukumbu za silaha cha Kituo cha Polisi Oysterbay ndicho kilionyesha kutumika kwa risasi tisa kati ya 30 za silaha aliyokuwa amepewa Koplo Saad.

ITAENDELEA KESHO

Advertisement