ZRA yataja sababu nne mafanikio makusanyo ya kodi 2022/23

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Yusuph Juma Mwenda akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya kukusanya kodi kwa ufanisi mwaka wa fedha 2022/23 ofisini kwake. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Yusuph Mwenda amezungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya ukusanyaji mapato kwa mwaka wa fedha 2022/23 (Julai 2022- Juni 2023) ambayo yamefikia kwa asilimia 97.65.

Unguja. Wakati Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) ikifikia makusanyo kwa asilimia 97.65, mambo manne yametajwa kuchangia ufanisi huo ikiwa ni pamoja na kukua kwa uchumi wa Zanzibar.

Kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23, ZRA imefanikiwa kukusanya Sh565.8 bilioni kati ya lengo la kukusanya Sh579.5 bilioni ambao unatajwa kuwa ufanisi mkubwa ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka 2021/22 ambayo ilikuwa Sh374.2 bilioni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Julai 2, 2023 kuhusu mafanikio hayo ofisini kwake Mazizini Unguja, Kamishna Mkuu wa ZRA, Yusuph Mwenda ametaja sababu nyingine ni kuimarika kwa matumizi ya mifumo katika ukusanyaji wa kodi.

“Kuongezeka makusanyo ya kodi kwa asilimia 51 ambacho ni kiasi cha Sh191.5 bilioni katika mwaka wa fedha 2022/23 umechangiwa kwa kiasi  kikubwa na mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa ufanisi na utendaji wa mamlaka na kuimarika kiwango cha huduma kwa walipa kodi,” amesema Mwenda

Sababu nyingine iliyotajwa na kamishna huyo ni kuongezeka kwa uwajibikaji wa hiari kwa baadhi ya walipa kodi na ZRA kuongeza walipa kodi wengine kwani imesajili walipa kodi wapya 5,504 kati ya walipa kodi 6,000 ambacho ni kiwango cha ufanisi wa asilimia 92 ya usajili.

Hata hivyo, akizungumzia kuhusu kutofikia makusanyo ya asilimia 100, Kamishna Mwenda amezitaja sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi huku wengine wakiwasilisha malipo ambayo sio sahihi.


Pia, amesema baadhi ya wafanyabiashara wakiagiza mizigo wanapunguza idadi hiyo huku kwa wenye mahoteli wakidanganya idadi ya wageni wanaofika na muda wanaokaa jambo ambalo makisio ya makusanyo.

Hata hivyo, amesema katika malengo ya makusanyo ya mwaka wa fedha 2023/24 imani yao watafikia malengo ya kukusanya Sh675 bilioni kwa asilimia zote kwasababu tayari wamejipanga na mifumo imeimarishwa zaidi hivyo itakuwa inasomana kila sehemu.

“Kama tukifikia ulipaji kodi wa hiari tukakusanya kinachotakiwa basi tutashawishi hata Serikali kupunguza gharama na italeta ufanisi mkubwa zaidi,” amesema


Amempongeza Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi na viongozi wengine wa Serikali kwa uungwaji mkono, uhamishaji na miongozo wanayoitoa ambayo inarahisisha ulipaji kodi wa hiari.


Kuhusu kusitisha utoaji wa motisha iliyoanzishwa na ZRA kwa wananchi wanaodai risiti za kieletroniki, Kaimu Meneja Uhusiano na Huduma kwa walipakodi ZRA, Makame Khamis Moh’d amesema jambo hilo kwa sasa limesitishwa baada ya kubaini wafanyabaishara wengi walikuwa wanadanganya

“Badala ya kuweka namba za mteja mfanyabiashara anaweka namba zake mwenyewe anajifanya kama yeye ndio mteja kwahiyo ilinoekana isitishwe ili kuangalia mazingira mazuri ya kufanya jambo hilo lakini bado linaendelea kwasababu inahamasisha wananchi kudai risiti za kielektroniki,” amesema Makame