Zungu aibua mapya suala la tozo

Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Hassan Zungu

Muktasari:

  • Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Azzan Zungu amesema kuna utamaduni unaojengwa wa kuipiga dongo Serikali kuhusu tozo za miamala ya kieletroniki wakati kuna watu wanachukua fedha nyingi kuliko Serikali.


Dodoma. Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Azzan Zungu  amesema kuna utamaduni unaojengwa wa kuipiga dongo Serikali kuhusu tozo za miamala ya kieletroniki wakati kuna watu wanachukua fedha nyingi kuliko Serikali.

Akizungumza leo Jumatano Septemba 21, 2022 kabla ya kuahirisha kikao cha Bunge, Zungu amesema jana Serikali imetangaza kupunguza tozo za miamala lakini wananchi wengi wanalalamikia makato yanayokatwa na Serikali lakini sio makato yanayokatwa na benki na kampuni za simu nchini.

“Lazima kudhibiti, benki unatuma fedha wanachukua nyingi sana zaidi ya Serikali kwa asilimia kubwa sana lakini Serikali imejenga madarasa na vituo vya afya ndio inayolaumiwa.”





“Kwa hiyo kuna-syndicate ambacho kinajengwa kuipiga dongo Serikali wakati pesa wanachukua watu wengine,”amesema.

Ameitaka Serikali kuhakikisha hilo wanalitazama kwa kuangalia ni namna gani watadhibiti mapato ya mabenki na kupunguza gharama za huduma (service charge) zao pamoja na gharama za simu.

“Niwaombe wananchi unapotuma fedha tazama break down inavyoandikwa, unaona mapato wanayochukua makampuni ya simu na mabenki yako juu zaidi ya mapato ya Serikali,”amesema.