Serikali yafuta tozo...

Serikali yafuta tozo...

Muktasari:

  • Serikali imefuta tozo ya miamala ya kielektroniki ya kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu na miamala ya simu kwenda benki.

Dodoma. Hatimaye Serikali imesikia kilio cha Watanzania kwa kufuta na kupunguza kiwango cha tozo za miamala ya kieletroniki.

Uamuzi huo umetangazwa leo Jumanne Septemba 20, 2022 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba bungeni baada ya kipindi cha maswali na majibu.

Amesema Serikali imepunguza wigo wa tozo, kuchochea matumizi ya miamala kwa ajili ya kupunguza fedha taslimu, kurahisisha utozaji na kuzuia kutoza tozo husika mara mbili.

“Marekebisho yaliyofanyika ni kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu (pande zote) na kufuta tozo ya kuhamisha fedha ndani ya benki moja (pande zote),”amesema.

Dk Mwigulu ametaja marekebisho mengine ni kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda benki nyingine (pande zote).

Amesema pia wafanyabiashara (merchants) hawatahusishwa kama ilivyo kwenye kanuni za sasa.

Amesema pia wamesamehe tozo ya miamala kwenye utoaji wa fedha taslimu kupitia wakala wa benki na ATM kwa miamala yenye thamani isiyozidi Sh30,000.

“Kupunguza gharama ya miamala kwa asilimia 10 hadi asilimia 50 kufuatana na kundi la miamala. Ikumbukwe kuwa tozo hizo ambapo viwango vya tozo vilishushwa kwa asilimia 30 kutoka kiwango cha juu cha Sh10,000 hadi kiwango cha juu cha Sh7,000,”amesema

Dk Mwigulu amesema marekebisho haya yataanza kutumika Oktoba Mosi mwaka huu.

Aidha, amesema Serikali inafuta utaratibu wa kodi ya zuio inayotokana na pango kukusanywa na mpangaji na badala yake jukumu hilo linarejeshwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa utaratibu utakao bainishwa kwenye kanuni.

“Napenda kusisitiza kuwa kodi ya zuio ya pango siyo ya mpangaji bali inapaswa kulipwa na mpangishaji ambaye ndiye anapokea mapato kutokana na uwekezaji au biashara ya kupangisha,”amesema.

Dk Mwigulu ameelekeza fedha hizi zifidiwe kutokana na kubana matumizi mengineyo ndani ya Serikali ambayo hayataathiri utekelezaji wa majukumu ya Msingi ya mafungu husika.

Amemwelekeza Mlipaji Mkuu wa Serikali kukaa na maofisa Masuuli wote kuyaangalia upya mafungu ya matumizi mengineyo ili miradi ya maendeleo yote isiathirike kwa hatua hii.

“Tukate kwenye chai, vitafunwa, misafara kwenye safari za ndani na nje kwa maafisa wa wizara zetu kama Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) alivyoelekeza, tukate mafunzo, semina, matamasha, warsha,”amesema.

SOMA ZAIDI: Wamekubali

Amesema fedha hizo pia zikatwe kwenye makundi yanayokwenda kukagua mradi uleule kwa nyakati tofauti au makundi yanayokwenda eneo lilelile kila mtu na gari lake (Mfano, Wilaya ileile kila ofisa na gari peke yake, mkoa uleule kila Kiongozi) na gari yake pekee yake.