LHRC yafungua shauri kupinga tozo, Serikali yapewa siku 14

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba

Muktasari:

Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC), kimefungua shauri la kupinga tozo za miamala ya kielektroniki, Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu ya Dar es Salaam dhidi ya Waziri wa Fedha na Mipango na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Singida. Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC), kimefungua shauri la kupinga tozo za miamala ya kielektroniki, Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu ya Dar es Salaam dhidi ya Waziri wa Fedha na Mipango na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Felista Mauya akizungumza na Mwananchi Digital, leo Jumatatu Septemba 5, 2022 amesema shauri hilo limefunguliwa Septemba 1, 2022 na kupewa namba 42/2022.

Mauya amesema katika shauri hilo, LHRC inaiomba Mahakama Kuu iruhusi kituo kiwasilisha maombi ya kufanya mapitio ya kimahakama ili kutengua kanuni za tuzo.

"Tunaomba kanuni zitenguliwe kwa kuwa zilitungwa bila kufuata utaratibu ulioainishwa ndani ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano ya mwaka 1977 kuhusu upitishwaji wa sheria ya tozo kwa njia ya ya kielekroniki," amesema

Amesema LHRC imeomba Mahakama kuweka zuio la muda (temporary Injection) kuendelea kutumika kwa kanuni hizo hadi kesi ya msingi itakapofika mwisho.

Amesema kwa upande wake Serikali imeomba Mahakama kuipa siku 14 kujibi hoja za mleta maombi ambapo majibu hayo yatawasilishwa Septemba 14, 2022.

"Baada ya mahakama kupokea majibu hayo LHRC itaruhusiwa  kuwasilisha Hoja za ziada  na shauri hilo limepangwa kitajwa kusikilizwa September 20 mwaka huu," amesema.

Hata hivyo, Mauya amesema baada ya kupitishwa shauri hilo wataweka wazi jopo la mawakili ambao wamejitokeza kutetea kupinga tozo hizo.

"Tunamawakili wetu wa LHRC na wengine ambao ndio watasimamia kesi hiyo kwa sasa hatupendi kuwaweka wazi," amesema

Wakati huo huo, LHRC leo Jumatatu imeanza kutoa msaada wa kisheria unaotembea (mobile legal Aid) kwa wananchi wa Mkoa wa Singida.

Mkuu wa LHRC Mkoa Arusha, Hamis Mayombo amesema huduma inatolewa bure na imeanza wilaya ya Ikungi na Singida mjini na jana Jumapili mashauri mengi yalikuwa ni migogoro ya ardhi.

"Tutakuwa katika huu kwa wiki moja tukitoa msaada wa kisheria," amesema.