Wachumi wafichua mapya ya tozo benki

Wasomi: Tozo mpya ya benki ni batili, ifutwe

Muktasari:

  • Wadau wa masuala ya uchumi wamesema tozo za miamala ya benki na simu zitawarudisha wananchi kwenye mifumo ya zamani ya kutembea na fedha taslimu.

Dar es Salaam. Wadau wa masuala ya uchumi wamesema tozo za miamala ya benki na simu zitawarudisha wananchi kwenye mifumo ya zamani ya kutembea na fedha taslimu.

Hayo yanajiri wakati asilimia 75 ya wananchi wakisema, viwango vya kodi kwenye miamala ya simu na benki ni vikubwa kulingana na ripoti ya utafiti ya Taasisi ya Twaweza iliyozinduliwa juzi, jijini hapa.

Utafiti huo umebainisha kupungua kwa utumaji wa fedha kwa njia ya simu tangu Julai, 2021 kwa asilimia 44 kuliko wale wanaoripoti kutuma fedha kwa njia hiyo kuwa asilimia 15.

Hata hivyo, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa alisema utafiti huo si rasmi, Serikali inaufanyia kazi na itakuja na taarifa rasmi.

“Idadi ya wanaopokea fedha kwa njia ya simu imepungua tangu Julai, 2021 kwa asilimia 46 kuliko wale wanaoripoti kupokea zaidi asilimia 14,” inasema sehemu ya ripoti ya utafiti huo wa Twaweza.

Juni mosi 2022, Sheria ya Fedha imepitisha tozo ya miamala ya benki na kuanza kutekelezwa, huku gharama ya kutuma na kutoa fedha ikiongezeka zaidi.

Tozo hizo zilizolenga miamala kwa njia ya kieletroniki, zimeendelea kukosolewa na wananchi, wanasiasa na wachumi wakisema zinaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Wadogo Tanzania, Stephen Lusinde, akizungumza jana na Mwananchi alisema hatari ya tozo hizo ni kudhoofisha kipato kwenye jamii na kuondoa matumaini ya huduma za kidijitali zikiwamo za benki kufika vijijini.

Kupitia muongozo wa tozo kwa njia ya miamala ya benki uliyotolewa na Serikali, wataalamu wanasema makato hayo ni zaidi ya mara mbili kutoka chanzo kimoja mfumo wanaoutaja kutokuwa rafiki kwenye ukusanyaji kodi kwa Serikali.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, kinachotozwa katika tozo hizo mpya ni makato yanayofanywa katika kila hatua mtu anapotaka kutumia mapato yake, jambo ambalo halishauriki kwenye kodi.

Kwa msingi huo, Lusinde alieleza badala ya kuwatumia ndugu fedha kwa njia ya benki au simu, ili kuepusha makato, mtu ataamua kufunga safari kuzipeleka fedha hizo kuepusha makato.

“Tozo ya miamala ya fedha kwa njia ya simu na benki zinakwenda kinyume na mpango wa Serikali wa kupanua wigo wa taasisi za kifedha,” alisema.

Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Stephen Chamle alisema tozo zilizopo hazina afya kwa uchumi wa nchi kwa sababu upo uwezekano mkubwa kuwaondoa wafanyabiashara katika shughuli rasmi za kifedha, akishauri tozo hizo ziondolewe.

Kwa upande mwingine, Chamle alitolea mfano mfanyakazi ambaye mshahara wake unapitia benki na kukatwa PAYE, atakapohamishia fedha zake kwenye simu hukatwa tozo na anapotoa pia hukatwa.

Mwaka 2021, siku nne baada ya Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kieletroniki, Sura Na. 306 kuanza kutekelezwa, Chama cha Watoa Huduma za Mtandao (Tamnoa) walisema biashara zilidorora na kuitaka Serikali kufanya mabadiliko ya tozo hiyo.

“Wateja wanalalamika hususani vijijini, japokuwa bado tunawapatia huduma, tukiamini huduma za kifedha kwa njia ya simu ni muhimu kwa jamii,” alisema Hisham Hendi aliyekuwa Mwenyekiti wa Tamnoa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania Plc.


Mawakala

Tozo ya miamala ya fedha kupitia benki ni mwendelezo wa mikakati ya Serikali kukusanya kodi na Julai 15, 2021, watumaji na watoaji fedha kupitia simu za mkononi, walianza kulipa kodi ya uzalendo,

Mawakala hao walisema wateja walianza kupungua Julai 15, mwaka jana wakati kodi hiyo ilipoanza na kadri siku zinavyokwenda ndivyo wanazidi kupungua.

Josiah Lairumbe, wakala anayetoa huduma Soko Kuu jijini Arusha katika moja ya mahojiano na Mwananchi alisema mbali ya idadi ya wateja kupungua, malipo ya bidhaa za kielektroniki kupitia simu za mkononi nayo yalishuka.


Ripoti ya TCRA

Takwimu za mawasiliano ya robo mwaka iliyoishia Juni 2022 iliyochapishwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zilionyesha mwenendo wa miamala ya fedha kwa njia ya simu za mkononi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuanzia 2019/21 iliongezeka.

Pia, ripoti ya TCRA inaonyesha mwaka 2019 thamani ya miamala ya fedha kwa watoa huduma wote ilifikia Sh101.8 trilioni.

Kiwango hicho kinatajwa kuongezeka hadi kufikia Sh127.9 trilioni na Sh137. 216 trilioni mwaka 2020 na 2021 hivyo hivyo.

Kutokana na malalamiko ya wananchi, Serikali ilipunguza gharama kwa asilimia 30 ilipofika Septemba 2021 na kama hiyo haitoshi, tozo hizo zikapunguzwa tena Julai 2022, hivyo kufanya punguzo la jumla la asilimia 60 ya kiwango cha kilichowekwa awali.

Pamoja na punguzo hilo, Serikali kupitia Sheria Fedha ya mwaka 2022 iliweka tozo ya miamala ya benki, ambayo nayo imezua mjadala upya.

Pamoja hayo, Septemba 2021 Rais Samia Suluhu Hassan aliposimama njiani eneo la Tegeta, Dar es Salaam akielekea Bagamoyo kurekodi kipindi cha Royal Tour cha kutangaza utalii alisema tozo za miamala ya simu zitaendelea kuwepo na hataki kudanganya kuwa zitaondolewa, huku akiweka bayana tozo za Septemba na Oktoba kujenga madarasa 500.
“Nataka niwaambie tozo zitaendelea kuwepo na sitaki kuwaficha kwa sababu tozo zile miezi miwili tuliyoanza nayo tumekusanya Sh60 bilioni hivi na zimepelekwa kujenga vituo 220 vya afya, hivyo tunajenga wenyewe,”alisema.

Agosti 20 2021, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema katika kipindi cha wiki nne tangu kuanza kukata tozo ya miamala, Serikali ilikusanya Sh48.4 bilioni huku zaidi ya Sh22 bilioni zikipelekwa katika vituo vya afya.