Makali ya tozo yalianzia hapa

Muktasari:

  • Wakati Serikali ikiahidi kufanyia kazi malalamiko ya wananchi kuhusu tozo za benki, wadau wamewanyooshea kidole wabunge wakihoji sababu za wawakilishi hao kuruhusu sheria hiyo kupitishwa bungeni.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikikiri kupokea maoni mbalimbali kuhusu tozo za miamala ya simu na kuahidi kuyafanyia kazi ndani ya kipindi kifupi, wadau wamelinyooshea kidole Bunge kwa kupitisha sheria ya fedha yenye marekebisho ya kodi na tozo, ambazo sasa zimezua malalamiko kwa wananchi.

Kwa takribani wiki mbili zilizopita, kumekuwa na mjadala mpana kuhusu tozo za miamala ya kielektroniki ambapo wananchi na wadau wengine wamekuwa wakipinga baadhi ya tozo zinazoanzishwa na Serikali.

Juzi, mawaziri wanne walikiri kupokea maoni tofauti ya wananchi kuhusu ukali wa tozo walipozungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

“Tulikuwa kimya tukisikiliza maoni ya wananchi na hii si mara ya kwanza kupokea maoni ya wananchi…moja kubwa ambalo tumeona ni kutozwa mara mbili, Serikali imesikia hiyo hoja na ni hoja ya msingi kweli kweli,” alisema Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba katika maelezo yake.

“Tozo hii si kodi ya biashara wala si kodi inayotokana na faida ya biashara, bali chimbuko lake ni ushirikiano wa pamoja kuunganisha nguvu ili tuweze kupata rasilimali tutekeleze majukumu hayo ambayo ni ya lazima,” aliongeza.

Mbali na Mwigulu, wengine waliojitokeza ni pamoja na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Tamisemi), Innocent Bashungwa, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Joyce Ndalichako na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), George Simbachawene.


Bunge lawamani

Wakizungumza na Mwananchi jana kwa nyakati tofauti, baadhi ya wadau walilikosoa Bunge kwa kushindwa kuzuia makali ya tozo wakati wa kupitisha Sheria ya Fedha ya mwaka 2020.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, alisema ndani ya Bunge kuna wabunge wenye uwezo wa kuchangia katika masuala mbalimbali, lakini baadhi yao wanashindwa kwa kuhofia kutopata uteuzi au kushughulikiwa na chama.

“Nashauri kuwepo mfumo wa mgombea huru au binafsi, pili Spika au naibu wasiwe wanatokana na chama cha siasa, bali wapatikane kwa utaratibu maalumu.

“Turudi watu kuwa huru katika kuchangia mawazo, ikitokea amefukuzwa basi anahamia chama kingine, hii itasaidia kurudisha nguvu ya Bunge,” alisema.

Kwa upande wake, Mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini na kada wa Chadema, John Heche alielekeza hoja zake kwa Serikali kabla ya kulifikia Bunge, akisema mapendekezo ya tozo yalitoka huko.

“Chanzo cha matatizo ya hizi tozo ni Serikali kwa upande mmoja, kwa upande mwingine ni Bunge kushindwa kutimiza wajibu wake. Hapa tunaangalia, tuna Bunge la aina gani, ni Bunge lililochaguliwa na wananchi, lina uwezo wa kupinga mapendekezo ya Serikali na likawa salama? Je, linaheshimu umma?” alihoji.

Heche alimnukuu waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Margareth Thatcher aliyewahi kusema: “Hakuna nchi iliyowahi kuendelea kwa kuwatoza wananchi wake kodi kuliko kiwango chao cha kuweza kulipa.”

Alisema Serikali imeanzisha tozo nyingi kwa wananchi kwa sababu zinatozwa hata kwenye maeneo ambayo wananchi hawatakiwi kutozwa. Alitolea mfano kodi kwenye miamala ya kibenki, huku benki hizo zikilipa kodi ya makampuni na kodi ya zuio.

Heche alidai wapo wabunge wasiosoma na kuchambua miswada ya sheria pamoja na mambo mbalimbali yanayopelekwa na Serikali.

Maoni ya wadau hao kuhusu Bunge yamekuja wakati juzi Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana akiwa mkoani Kigoma aliwaagiza viongozi na watunga sheria kuwarahisishia maisha wananchi wa kipato cha chini, ikiwamo kuondoa sheria kandamizi.

Alisema kuna wakati watu wanashindwa kufanya shughuli zao, jambo alilosema linamkera hata Rais Samia Suluhu Hassan.

“Sheria nyingine ni mbovu, zinaumiza na hazifai kuwepo, lakini Rais wakati anawaapisha mawaziri alisema wakaangalie sheria zote kandamizi ili zifutwe, sasa nashangaa sijui ngapi zimefutwa,” alisema Kinana.


Wenye benki

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Benki Tanzania (TBA), Tuse Mwaikasu alisema tozo ni pato la Serikali, hivyo wenye mamlaka ya kuiondoa ni Serikali na siyo benki.

Kauli yake hiyo imekuja siku moja baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kueleza nia ya kukutana nao.

Akizungumzia utayari wa benki kuondoa tozo hizo kama watakutana na Waziri wa Fedha, Mwaikasu alisema wao kama sekta ya benki wanatamani kuwahudumia na kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa huduma nafuu.

“Ila zaidi sana tunatamani wananchi wengi watumie huduma za kifedha kwa njia ya kielektroniki na kidijitali, hivyo tozo ikiondolewa italeta unafuu wa huduma za kibenki na kuleta fedha zaidi kwenye mfumo rasmi,” alisema.

“Tukiondoa tozo kwenye huduma za kibenki, itaongeza uhuru wa wananchi kufanya malipo kupitia benki na miamala ya fedha kielektroniki ambayo ni njia ya haraka na salama,” alisema.

Mbali na hayo, alisema kuwa tozo ikiondolewa, mzunguko wa fedha kwenye mifumo rasmi ya fedha utaongezeka.

Mwaikasu alisema malipo kwa mifumo ya kielektroniki yanaongeza uwazi kwenye malipo na kufanya ukusanyaji wa kodi mbalimbali uwe rahisi zaidi.


Sheria ya Fedha ilivyopitishwa

Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za Bunge, muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2022 ulisomwa kwa mara ya pili bungeni Juni 20, mwaka huu ambapo pia maoni ya Kamati ya Bajeti nayo yaliyosomwa siku hiyo.

Alipoulizwa kwa simu na Mwananchi Agosti 20, 2022, Mwenyekiti wa kamati ya Bajeti ya Bunge, Daniel Sillo alisema walitambua kuwepo kwa tozo hiyo na walikubaliana nayo, hivyo wananchi walipe tu.

“Sisi tulipitisha ile sheria, siyo kwamba hatukuona, sheria inapitishwa na Bunge.

“Kilichofanyika, Serikali ilipunguza tozo ya miamala ya simu peke yake kwa asilimia 60, baada ya hapo ikaongeza mawanda, kwa sababu wanaofanya miamala ya simu, siyo simu peke yake, bali hata benki wanafanya kuweka na kutoa fedha,” alisema.

Alisema tozo iliyokuwa inakatwa kwenye miamala ya siku ambayo pia ililalamikiwa na wananchi, ilipunguzwa, lakini benki nazo zikawekewa tozo mpya.

Alipoulizwa maoni yake kuhusu malalamiko ya wananchi, Sillo alisema: “Hakuna kodi inayofurahiwa, kodi hiyo ni ngumu, lakini ndiyo inajenga vituo vya afya na inaleta maendeleo. Malalamiko ni baada ya watu kukatwa lakini, mara nyingi tozo haifurahiwi.’’

Miongoni mwa wabunge waliochangia muswada huo ni pamoja na Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda aliyesifu mjadala wa muswada huo, akisema hakukuwa na misuguano katika kuujadili.

“Naunga mkono hoja tupitishe mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Fedha, ambayo ndio tunaitegemea itumiwe na vyombo vyetu, ikiwamo TRA kuhakikisha Sh28.02 trilioni inapatikana.

“Kama tutaanza kukwamisha baadhi ya vipengele basi itaathiri kupata Sh28.02 trilioni (makusanyo ya TRA). Tunaweza kujikuta tukikwamisha utekelezaji wa baadhi ya miradi muhimu tuliyopitisha,” alisema.

Wabunge wengine waliochangia mjadala huo ni pamoja na mbunge wa viti maalumu (Pwani), Subira Mgalu aliyeipongeza Serikali kwa kufanya marekebisho katika mifumo ya malipo sura 437, punguzo la ukomo wa juu wa kiwango cha kutuma na kupokea miamala kutoka Sh10,000 hadi Sh4,000.

Naye Neema Lugangira katika mchango wake alionyesha wasiwasi kuhusu uwezo wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kutekeleza ‘blue print’ katika eneo la urahisishaji wa biashara na utoaji viwango.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kinondoni, Tarimba Abbas alihoji sababu ya Serikali kuweka kodi ya awali ya Sh20 kwa kila lita ya mafuta wakati kamati ilishauri kodi hiyo iondolewe.

Juzi, alipoulizwa kuhusu jukumu la Bunge la kuwalinda wananchi kupitia sheria kandamizi, Naibu Spika Mussa Azan Zungu alimtaka mwandishi kurejea kauli ya Waziri Mwigulu.

“Waziri wa Fedha ameshasema. Wamewasikiliza wananchi wanavyosema na wamechukua kilio cha wananchi. Yeye ndiye mwenye instruments (mamlaka) ya masuala yote ya fedha,” alisema.


Wadau

Licha ya kulikosoa Bunge, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema Serikali ndiyo imesababisha mzozo wa tozo, kwa sababu haikuchanganua kupata vyanzo vingine vya mapato, wao wakaona ni bora kumkamua mwananchi wa kawaida anayeishi chini ya dola moja.

“Huyu mtu anayeishi chini ya dola moja wanamkamua ili waweze kupata mapato, shida ni wao kutobuni vyanzo vya mapato, lakini kwa kuwa wamesema wanakwenda kupitia baadhi ya tozo, tusubiri kuona utekelezaji wake,” alisema.


Sheria zilizolalamikiwa

Mbali na Sheria ya Fedha ya 2022, Bunge limewahi kuingia lawamani kwa kupitisha sheria zinazoonekana kuwakandamiza wananchi.

Mei 29, 2021 aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai alishikwa na butwaa kwa kuona Bunge lilivyopitisha sheria ya utaifishaji mifugo inayoingia kwenye hifadhi akisema ni mbaya. Akahoji huenda ilipitishwa wakati wabunge wakiwa wamelala.

Ndugai alisema kama wabunge hawakuwa wamelala, huenda yeye (Ndugai) alikuwa safarini, kwani haiwezekani kuwa na sheria ya namna hiyo.

“Mheshimiwa Waziri wa Mifugo, hii migongano ya wafugaji na hifadhi, ambapo ile sheria sijui ilipita wapi, tulikuwa tumelala sijui ilikuwaje!

“Ile kwamba ng’ombe wakiingia hifadhi halafu wanataifishwa wote? Aah hapana, hii kitu sijui ilikuwaje? Sijui nilikuwa nimesafiri, sijui nilikuwa nimeenda wapi, sikumbuki vizuri, lakini ilipoanza utekelezaji wake, tumepiga kelele muda mrefu kwa kweli kwamba hii sheria ni tatizo, ni sheria dhulmati kabisa,” alisema.


Sheria ya Takwimu

Sheria nyingine iliyozua malalamiko miongoni mwa wadau ni ya takwimu iliyopitishwa mwaka 2016.

Hata hivyo, Juni 2019 Bunge kwa kuzingatia malalamiko ya wadau, ilirekebisha vifungu vilivyokuwa vikilalamikiwa kupitia muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2019.

Ndani yake ukiwa na marekebisho ya Sheria ya Takwimu (sura ya 351) ambayo yanatoa ruhusa kwa mtu yeyote kutoa takwimu zinazotofautiana na zilizotolewa na Serikali.

Kwa uamuzi huo, kifungu cha 37(4) kinachotoa adhabu kwa mtu anayetoa taarifa za kitakwimu bila kupata kibali cha Ofisi ya Taifa ya Takwimu, kilifutwa.

Kabla ya kufutwa, kifungu hicho kilitoa adhabu kwa makosa hayo ya jinai katika Sheria ya Takwimu ambayo ilikuwa ni jela miezi sita au faini isiyopungua Sh2 milioni au vyote viwili.

Hata hivyo, mtoa takwimu anatakiwa kuzingatia misingi iliyowekwa katika miongozo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Wakati Serikali ikiwasilisha marekebisho hayo, waliokuwa wabunge, wakiwamo Zitto Kabwe (Kigoma Mjini) na Ally Salehe (Malindi) walisema Serikali ilifanya marekebisho hayo, baada ya kubanwa na nchi wahisani zilizogoma kutoa msaada kutokana na ubaya wa awali wa sheria hiyo.


Imeandikwa na Elias Msuya, Peter Elias, Baraka Loshilaa na Bakari Kiango