Zungu atoa neno mgambo kunyanyasa mamalishe, machinga

Naibu Spika, Mussa Zungu akizungumza wakati wa kipindi cha maswali na majibu Bungeni leo Jumanne Aprili 16, 2024. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

Utoaji mikopo kwa wajasiriamali wadogo kuzinduliwa hivi karibuni.

Dodoma. Naibu Spika, Mussa Zungu ameagiza Serikali kushughulikia changamoto ya mamalishe na machinga kunyanyaswa na mgambo kwa kuchukuliwa mali na vyakula vyao.

Zungu amesema hayo leo Jumanne Aprili 16, 2024 baada ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima kujibu swali la mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu.

Mbunge huyo aliiomba wizara kuwapatia mikopo wamachinga mkoani Iringa.

Akijibu, Dk Gwajima amesema tayari mpango wa kuwainua wamachinga kiuchumi umeiva.

Amesema Sh18.5 bilioni ambazo Rais Samia Suluhu Hassan alielekeza zitolewe ziko mbioni kwa kuwa mkataba na benki husika umeshaingiwa.

Amesema mwongozo wa usajili umekamilika, kazi ya usajili ikiendelea, wakitarajia ndani ya wiki nne watazindua utoaji wa mikopo.

Baada ya majibu hayo, Zungu amesema mamalishe na machinga wanakopeshwa, lakini bado wananyanyaswa na mgambo, hivyo kushindwa kulipa mikopo yao.

“Wananyang’anywa vyakula vyao na mali zao, hawa watu ni wa mazingira magumu na si kwa Dar es Salaam tu, ni nchi nzima. Waambieni wakurugenzi wa halmashauri waache kunyanyasa watu waliojipanga,” amesema Zungu.

Amesema kuna watu wamejipanga na wanafuata sheria, lakini bado wananyanyaswa na mgambo.

Katika swali la msingi, Jesca amehoji ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Rais ya kuwasaidia machinga wa Iringa Mjini Sh700 milioni kwa ajili ya kuboresha mazingira yao ya kazi.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis, amesema wizara inatambua umuhimu wa kutekeleza ahadi iliyotolewa na Rais ya kutoa Sh700 milioni kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kazi ya wafanyabiashara wadogo wa Iringa Mjini.

Amesema wizara inaendelea kuwasiliana na Ofisi ya Rais ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Fedha kwa lengo la kutekeleza ahadi iliyotolewa na Rais.