Machinga Arusha wadai kudhalilishwa na mgambo

Muktasari:

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha amesema walioporwa mali zao na kuharibikia zikiwa stoo atawalipa fidia ya Sh100,000 kila mmoja

Arusha. Wafanyabiashara ndogondogo (machinga) wameibua tuhuma dhidi ya mgambo wa Jiji la Arusha, wakidai huwaomba rushwa ya ngono ili wasiwabughudhi katika maeneo ya biashara yasiyo rasmi.

Tuhuma hizo zimetolewa jana, Jumatatu Januari 23, 2024 kwenye mkutano uliohutubiwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda katika eneo la stendi ya daladala ya Kilombero jijini Arusha.

Wafanyabiashara hao wamedai wamekuwa wakiteseka na kudhalilishwa na mgambo, ambao pia huwapora mali zao kwa maelezo ya kufanya biashara maeneo yasiyoruhusiwa.

Zaituni Swai, amedai baadhi ya mgambo wamekuwa wakiwakagua maungoni na kuwashika maeneo nyeti wanapotaka kupora mali zao.

"Tusaidie kutoa neno kwa udhalilishaji huu wanawake tunaofanyiwa, hasa jioni huko pembezoni mwa barabara. Wakifanikiwa kuchukua bidhaa zetu ukiwafuata kwenye gari wanalokusanyia vitu wanatulazimisha kuwapa …ndipo waturejeshee," amedai Zaituni.

Asha Lema, amedai wameshafikisha malalamiko kwa uongozi wa Jiji la Arusha ulioahidi kushughulikia  lakini bado wanateseka.

Amemuomba Makonda afikishe kero hiyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

"Suala hili limekithiri hapa, kuna wengine tumeshanusurika kubakwa, tumelifikia jiji lakini hakuna utatuzi. Tunakuomba mwenezi hebu mwambie Rais Samia hivi ndivyo alivyotuma watu wake kututendea au wanatuchonganisha?" amehoji Asha.

Awali, mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo amesema mgambo wamekuwa wakiwaonea wafanyabiashara hao kwa kuwachukulia bidhaa zao na kwenda kuzirundika stoo maalumu ya Jiji la Arusha, hivyo kusababisha kuozea huko.

"Wanawanyang'anya matunda, vyakula, vyombo na nguo, wanaenda kurundika stoo ambako vinaharibikia huko. Bahati mbaya hata wakijaribu kuzifuata kwa majadiliano inakuwa mwanya wa kuombwa 'utamu' na ukikataa basi na vitu vimepotea," amesema.

Makonda katika mkutano huo alimuita Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha, Jumaa Hamsini kujibu tuhuma hizo.

Hamsini amesema wamekuwa katika utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kudhibiti ufanyaji biashara katika maeneo yasiyo rasmi kwa kutumia mgambo wa jiji.

Amesema machinga wote walio nje walipewa vibanda kwenye masoko mapya yaliyojengwa.

"Suala la kufukuza machinga katika maeneo yasiyo rasmi nalifahamu, hasa pembezoni mwa barabara. Huu ni utekelezaji wa maelekezo ya majiji,” amesema.

 “Tulifanya tathimini awali na machinga wote waliobainika kuwa hawana maeneo ya kufanyia kazi walipewa vibanda kwenye masoko yaliyojengwa, lakini tatizo hawataki kwenda na jioni wanarudi kuziba barabara."

Mkurugenzi huyo amekana kufahamu vitendo vya udhalilishaji vinavyofanywa na mgambo, ameahidi kufuatilia kwa ukaribu.

"Suala la rushwa ya ngono ndiyo kwanza nasikia leo, naomba muda wa kufuatilia na kuchukua hatua kwa wote watakaobainika kufanya kazi kinyume cha sheria na utaratibu," amesema.

Hamsini amesema, "Naomba wanawake wote ambao wametendewa vitendo hivyo waje ofisini kwangu kuanzia Alhamisi Januari 25, 2024 tuanze kufanyia kazi suala hilo, wale ambao wameporwa vitu vyao na kumwagwa stoo vikaharibikia huko, nitawapa fidia ya Sh100,000 kila mmoja."

Makonda kwa upande wake amewataka viongozi wa mkoa na wilaya kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Arusha kutatua kero hiyo.

"Haya mambo yanatia doa harakati za Rais wetu katika kuwahudumia wananchi wake na kuhakikisha wanaishi vema, hivyo naomba mkashirikiane kutatua kero hii kwa busara kubwa," amesema Makonda.