Tamwa: Bado kuna unyanyasaji katika vyumba vya habari

Muktasari:

  • Asilimia 77 ya wanawake 137 waliohojiwa wamekiri kukumbana na unyanyasaji wa kingono katika vyumba vya habari nchini.

Dar es Salaam. Wakati jamii ikiwa kwenye jitihada za kupambana na unyanyasaji na ukatili, imebainika kuwa bado kuna unyanyasaji wa kingono katika vyombo vya habari.

Utafiti wa hali ya usalama wa wanahabari wanawake kwenye vyumba vya habari 22 uliofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) ndiyo umebaini kuendelea kwa hali hiyo.

Matokeo hayo yameelezwa leo Jumanne, Novemba 28, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Tamwa, Dk Rose Reuben aliposoma muhtasari wa utafiti huo, wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 36 ya kuanzishwa kwa chama hicho.

Amesema kati ya wanahabari hao waliokumbwa na unyanyasaji wa kijinsia, asilimia 27 wamekumbana nao kutoka kwa vyanzo vyao vya habari.

Ameeleza asilimia 59, wamekumbana na kadhia hizo kutoka katika vyumba vyao vya habari na hasa watendaji wakubwa wakiwemo wahariri, mameneja na wamiliki wa vyombo hivyo.

"Unyanyasaji wa kijinsia na rushwa ya ngono unaathiri ubora na uaminifu wa waandishi wa habari iwapo changamoto hizo zitakaa kwa muda mrefu," amesema Dk Rose.

Hata hivyo, amesema utafiti huo umefanywa kati ya Julai hadi Septemba mwaka huu katika mikoa kadhaa nchini.

Akizungumzia utafiti huo, Mkurugenzi wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya amesema kinachofanywa na umoja huo ni kukusanya kanzidata ya matukio na kuvifuata vyombo vya habari kimoja kimoja.

Amesema umoja huo umekuwa ukipokea taarifa nyingi za unyanyasaji katika vyumba vya habari na jukumu inalotarajia kufanya ni kuelimisha vyumba vya habari.

"Kwa sasa tunaunda kanzidata ili tutoe ripoti na kuona namna ya kuvifikia vyumba vya habari kwa kuwa yapo mambo yanayohitaji kuelimishana tu," amesema.

Hata hivyo, amesema pamoja na kuwepo mwongozo wa kuanzishwa kwa madawati ya jinsia katika vyombo vya habari, lakini kwa sehemu kubwa hayakuanzishwa.

Ameeleza wakati hilo likitarajiwa kufanyika ni vema elimu ianze kutolewa ili wanahabari wasione aibu kuyatumia madawati hayo.

"Watu wasione aibu kuwa wanapokwenda kuripoti watajidhalilisha au pengine wamewahi kuona waliripoti na hakuna hatua iliyochukuliwa," amesema.

Akichangia mjadala kuhusu hali ya rushwa katika vyumba vya habari, Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dorothea Mrema amewasisitiza wanaokumbwa na madhila watoe taarifa kwa taasisi hiyo.

Amesema mapambano dhidi ya aina hiyo ya rushwa na nyingine ni jukumu la wananchi wote, hivyo kila mmoja na kila taasisi inapaswa kuonyesha juhudi za mapambano hayo.

"Kila taasisi inapaswa kushiriki mapambano dhidi ya rushwa kwa kuwa mkakati wa mapambano dhidi ya rushwa wa kitaifa unataka kila taasisi ipambane na rushwa, huu ni wajibu na jukumu la kila mmoja," amesema.

Hata hivyo, amesema Takukuru imekuwa ikipokea taarifa kuhusu matukio hayo na aghalabu huwachukulia hatua kwa kuwapeleka mahakamani baada ya kuthibitika.