Tamwa yataka taarifa za afya ya uzazi zenye kuleta mabadiliko

Muktasari:

Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Dk Rose Reuben amesema ombwe lililopo kati ya waandishi wa habari na watafiti, linasababisha tafiti nyingi ambazo zingeleta tija kwa jamii kufungiwa kwenye mkabati.

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Dk Rose Reuben amesema ombwe lililopo kati ya waandishi wa habari na watafiti, linasababisha tafiti nyingi ambazo zingeleta tija kwa jamii kufungiwa kwenye mkabati.

Dk Rose ameyasema hayo leo Alhamisi Julai 20, 2023 wakati akifungua warsha ya siku tatu inayowaunganisha waandishi wa habari, wanatafiti na wadau wengine wa masuala ya haki za afya ya uzazi kupitia mradi wa uchechemuzi wa masuala ya haki ya afya ya uzazi kwa wanawake wa mijini na vijijini kupitia vyombo hivyo.

"Vyombo vya habari ni nyenzo muhimu ya kuunganisha jamii, watunga sera na kuleta mabadiliko, lakini bado taarifa nyingi zinazotolewa kuhusu afya ya uzazi, hazifanywi kwa kina ili kuhakikisha haki ya afya ya uzazi inafuatwa," amesema Dk Rose na kuongeza;

"Watafiti wengi pia wanaishia kufanya kazi zao na kuzifungia ili wapate vyeo na kupanda kitaaluma lakini si kwa ajili ya jamii na hawatumii vyombo vya habari kwa kuwa bado hawajajua umuhimu wa machapisho yao kwa vyombo hivyo, lakini pia vyombo hivyo haviwafuati watafiti hao.”

Mkurugenzi huyo wa Tamwa ameongeza kusema kuwa bado kuna kazi haijafanywa vyema na wanahabari kwani wanawake bado wanakumbwa na changamoto ya haki za uzazi nchini.

"Watu wengi wanatamani kuwa na watoto wengi, tena watoto wakue wakiwa na usalama na wapate mahitaji ya msingi lakini bado kuna vikwazo vingi ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia, urahisi wa kuzitumia huduma na changamoto nyinginezo," amesema Dk Rose Reuben.

Mtafiti wa masuala ya afya ya uzazi kutoka Tamwa, James Mlali amesema "Vyombo vya habari visiishie kueleza tu au kuripoti matukio pekee lakini kuwashawishi watunga sera waweze kuchukua hatua."

Mradi huo unalenga kuwajengea uwezo wanahabari namna nzuri ya kuandika na kuchapisha habari zinazohusu haki za afya ya uzazi zinazoweza kuleta mabadiliko kijamii na kimifumo nchini.