Rais Samia kuongoza maadhimisho miaka 36 Tamwa

Muktasari:

  • Tamwa yaadhimisha miaka 36 tangu kuanzishwa kwake, Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi katika shughuli hiyo ya kihistoria.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya miaka 36 ya Chama cha Wanabari Wanawake Tanzania (Tamwa).

Maadhimisho hayo yatakayofanyika kwa siku mbili kati ya Novemba 28 na 29 yatabebwa na kauli mbiu ‘Uongozi bora na mchango wa wanawake ni chachu kuelekea Tanzania yenye maendeleo endelevu’.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 26 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Tamwa Dk Rose Reuben amesema maadhimisho hayo yataenda sambamba na uzinduzi wa ripoti ya rushwa ya ngono na ukatili wa kijinsia ndani ya vyombo vya habari.

Sambamba na hilo Dk Rose amebainisha kuwa katika maadhimisho hayo litazinduliwa jarifa la Sauti ya Siti ambalo ni tolea maalum kuhusu rushwa ya ngono.

“Maadhimisho ya mwaka huu yanaakisi safari ya miaka 36 ya Tamwa ambayo imeendelea kujikita katika kuhamasisha upatikanaji wa haki za wanawake na watoto wa kike nchini.

“Siku hii pia tunatarajia kutoa tuzo kwa mwanahabari aliyefanya vizuri katika masuala ya afya na uzazi na kutoa zawadi maalum kwa kutambua na kuthamni mchango wa waasisi 13 wa Tamwa,” amesema Dk Rose.

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa mafanikio ya Tamwa hayapo katika utekelezaji wa miradi pekee bali kuwapa elimu wanahabari hapa nchini pamoja na kuhamasisha kuwekwa kwa sera ya jinsia ndani ya vyombo vya habari.

 “Kwa miaka 36 ambayo tumekuwa tukifanya kazi ya kupinga ukatili wa kijinsia tumeona azimio la waasisi wetu la kutumia kalamu zao kuwafanya watu wazungumze kwa uwazi kuhusu ukatili limetimia.

“Miaka ya 90 wanawake walikuwa wanapigwa lakini wanasema wameuanguka, watoto walifanyiwa ukatili lakini ilikuwa haizungumzwi lakini sasa vyombo vya habari vinatoa taarifa za ukatili na watu wanaukataa na kuupinga hadharani,” amesema.

Dk Rose pia amegusia wimbi la unajisi kwa watoto wa kiume akiwataka wazazi na jamii kwa ujumla kuongeza ulinzi dhidi ya watoto ili kuwaepusha na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

 “Tunaamini watoto ni taifa la kesho, sasa kama taifa la kesho linafanyiwa ulawiti hatuwezi kuwa na watoto wenye utimamu wa afya ya akili na mwilli,” ameongeza.

Tamwa ilianzishwa mwaka 1987 na wanawake 13 wakiwamo Fatma Alloo, Edda Sanga, Leila Sheikh, Rose Haji, Ananilea Nkya, Valerie Msoka, Pili Mtambalike, Elizabeth Marealle, Rose Kalemera, Jamilla Chipo, Nellie Kidela, Halima Shariff na  Chemi Kidete.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, mmoja wa waasisi wa Tamwa, Elizabeth Marealle amesema, “Tulifanya kazi kwa kujitolea kwa hali zote ili kufanikisha malengo yetu. Tulijitoa kwa muda na mali kwa kuchangia kifedha. Tulianza katika sebule ya marehemu Nelly Kidela ambaye alikuwa miongoni wa waanzilishi.

“Tamwa  tuliyoitaka sio ya kujiangalia sisi wadau pekee, bali ilikuwa ni kukazia macho hali iliyopo katika jamii kwa ujumla wake tulitaka kuwa na jamii ya Kitanzania iliyo na amani na inayo heshimu haki za binadamu kwa mtazamo wa kijinsia,” anasema Marealle.